• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Real Madrid yang’oa Man-City na kufuzu kuvaana na Liverpool kwenye fainali ya UEFA

Real Madrid yang’oa Man-City na kufuzu kuvaana na Liverpool kwenye fainali ya UEFA

Na MASHIRIKA

REAL Madrid watakutana na Liverpool kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kutoka nyuma na kusajili ushindi wa 3-1 uliodengua Manchester City kwa jumla ya mabao 6-5 mnamo Jumatano usiku ugani Santiago Bernabeu.

Fainali ya UEFA msimu huu itachezewa jijini Paris, Ufaransa mnamo Mei 28, 2022.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walishuka dimbani wakijivunia ushindi wa 4-3 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa nusu-fainali uwanjani Etihad.

Riyad Mahrez aliwaweka Man-City kifua mbele katika dakika ya 73 kabla ya Rodrygo kutokea benchi kujaza nafasi ya Toni Kroos katika dakika ya 68 na kufungua Real mabao mawili ya haraka mwishoni mwa kipindi cha pili.

Mabao hayo yalifanya mechi hiyo kuingia muda wa ziada na Karim Benzema akafunga penalti katika dakika ya 95 baada ya kukabiliwa visivyo na Ruben Dias ndani ya kijisanduku. Goli hilo la Benzema lilikuwa lake la 43 ndani ya jezi za Real katika mashindano yote ya msimu huu.

Ushindi wa Real sasa utarejesha kumbukumbu za 2018 ambapo walikutana tena na Liverpool kwenye fainali ya UEFA. Wakiwa chini ya kocha Zinedine Zidane wakati huo, Real walisajili ushindi wa 3-1 jijini Kyiv, Ukraine baada ya kufunga mabao yao kupitia kwa Benzema na Gareth Bale aliyecheka na nyavu za Liverpool mara mbili kutokana na masihara ya kipa Loris Karius.

Kwa Man-City, macho yao sasa yataelekezwa kwa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambalo wanapigiwa upatu wa kulihifadhi. Kufikia sasa, miamba hao wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 83, moja pekee mbele ya Liverpool wanaofukuzia mataji manne msimu huu.

Zaidi ya EPL na UEFA, Liverpool wanaonolewa na kocha Jurgen Klopp wanawania pia Kombe la FA na walitawazwa wafalme wa Carabao Cup mwishoni mwa Februari 2022 baada ya kupepepta Chelsea kwa penalti 11-10 ugani Wembley. Watakutana tena na Chelsea uwanjani Wembley mnamo Mei 14 kwa fainali ya Kombe la FA.

Man-City wamejizolea mataji matano ya EPL na wanasalia na kibarua cha kushinda mechi nne zijazo ili kunyanyua taji la sita tangu umiliki wao utwaliwe na mabwanyenye wa Abu Dhabu mnamo 2008.

Ingawa hivyo, taji la UEFA ndilo limekuwa likikwepa Man-City katika historia yao. Kikosi hicho kilipokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Chelsea kwenye fainali iliyofanyika jijini Porto, Ureno.

Real ndio wanaoshikilia rekodi ya kushinda mataji mengi zaidi katika UEFA na fainali ya msimu huu inawapa nafasi maridhawa ya kunyanyua ubingwa wa kipute hicho kwa mara ya 14. Katika safari yao ya kutinga fainali, Real walikomoa Paris Saint-Germain (PSG) kwa mabao 3-2 katika hatua ya 16-bora kabla ya kung’oa Chelsea kwa jumla ya magoli 5-4 katika robo-fainali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Sicily Kariuki adinda kumfanyia kampeni gavana Kimemia

Jezi ya ‘Hand of God’ ya Maradona yazoa Sh1.1...

T L