• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 8:50 AM
Sonko aanza kusuasua

Sonko aanza kusuasua

NA FARHIYA HUSSEIN

ALIYEKUWA gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, ameanza kupanga mikakati upya baada ya uwezekano wake kuwania ugavana Mombasa kuzidi kukumbwa na vikwazo chungu nzima.

Bw Sonko alikuwa ametua Mombasa kwa mbwembwe wiki chache zilizopita kuzindua kampeni za kutaka urithi wa kiti cha Gavana Hassan Joho.

Hata hivyo, sasa ameamua kurai wakazi wa Mombasa kuunga mkono mgombea mwenza wake, Bw Ali Mbogo, endapo yeye atazuiliwa kuwania ugavana kwa sababu ya kesi za kimaadili zinazomkumba.

Awali, Bw Mbogo ambaye ni Mbunge wa Kisauni ndiye alikuwa ametarajiwa kuwania ugavana Mombasa kupitia Chama cha Wiper lakini baadaye akashawishiwa kuwa mgombea mwenza wa Bw Sonko.

Akiendeleza kampeni zake Jumapili, Bw Sonko alisema iwapo itafikia hatua ya yeye kulazimika kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho, nafasi yake inastahili kuchukuliwa na Bw Mbogo.

“Tumekaa na chini na mwenzangu na kukubaliana kwamba nikilazimika nisiwanie, atachukua nafasi hiyo na kuwa kwenye kinyang’anyiro cha ugavana. Aliniamini na kuniunga mkono na ninarudisha fadhila kwa kumteua,” akasema.

Kauli hii yake ni tofauti na awali ambapo alikuwa akisisitiza atapigania haki yake hadi kuhakikisha atakuwa debeni katika uchaguzi wa Agosti.

Pingamizi dhidi ya nia yake kuwania ugavana Mombasa zilitoka pande tofauti ikiwemo kwa wapinzani wake katika vyama vya ODM na UDA.

Mbali na wanasiasa, kuna wapigakura na mashirika ya kijamii ambayo yaliwasilisha kesi mbalimbali mahakamani kumpinga kwa vile alibanduliwa mamlakani kwa sababu za kimaadili.

Agizo la muda lilitolewa na mahakama kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) isikubaliwe kumruhusu awanie kiti chochote cha kisiasa katika uchaguzi ujao.

Jaji Mkuu Martha Koome, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji, na mwenzake wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), pia walitoa maoni yao kwamba mwanasiasa aliyebanduliwa mamlakani kwa makosa ya kimaadili na ufisadi hafai kushikilia nafasi yoyote ya uongozi serikalini.

Gavana huyo wa zamani wa Nairobi aliwarai wakazi kujitokeza kwa wingi wakati wa uchaguzi ili kuleta mabadiliko Mombasa.

“Nyinyi ndio watu mtakaoamua mabadiliko wa Mombasa. Kura zenu ndizo zitakazochagua na kuamua kiongozi atakuwa nani. Hakikisha mumepiga kura ya mabadiliko,” Bw Sonko aliwahimiza wakazi.

Hata hivyo, uwezekano wa Bw Mbogo kuwa debeni iwapo Bw Sonko atazuiwa kuwania utategemea uamuzi wa IEBC kwani muda wa wanasiasa kuwasilisha wagombeaji ugavana ulishapita.

Bw Mbogo aliyekuwa katika msafara wa Bw Sonko, alikubali wito wa kutwaa usukani kupeperusha bendera ya Wiper na kuahidi kuendeleza ajenda waliyoanzisha kuhusu kuleta mabadiliko Mombasa.

“Nitaendelea kusisitiza kwamba tutabadilisha Mombasa. Watu hawa wametutawala kwa miaka 10, ni wakati sasa tubadili itikadi hiyo,” akasema Bw Mbogo.

Kinyang’anyiro cha kurithi kiti cha Bw Joho kimevutia pia Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir (ODM), aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar (UDA), na Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi.

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Kisukari chapofusha idadi kubwa ya wazee Lamu

Kylian Mbappe asema angali na ndoto ya kuchezea Real Madrid...

T L