• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
SHINA LA UHAI: Kisukari chapofusha idadi kubwa ya wazee Lamu

SHINA LA UHAI: Kisukari chapofusha idadi kubwa ya wazee Lamu

KALUME KAZUNGU NA VALENTINE OBARA

KWA muda sasa, wataalamu wa afya katika Kaunti ya Lamu wamekuwa wakishuhudia ongezeko la magonjwa ya macho hasa miongoni mwa wazee.

Hali hii iliwasababisha baadhi yao kuanzisha uchunguzi ambao ulionyesha kuna uhusiano wa ugonjwa wa kisukari uliokithiri katika eneo hilo la Pwani na matatizo ya macho.

Kulingana na takwimu za wizara ya Afya ya Kaunti ya Lamu, wagonjwa wa macho kati ya 10 na 20 hupokewa katika hospitali kuu kila siku na wengi wao ni wazee kuanzia umri wa miaka 50.

“Takwimu za kliniki yetu ya macho hapa zinaonyesha idadi kubwa ya wazee wenye matatizo ya macho wana lile tatizo linalofahamika kama cataract au mtoto wa macho,” aeleza Dkt Roba Duba, Mkuu wa Matibabu ya Macho katika hospitali kuu ya King Fahd, mjini Lamu.

Dkt Duba asema juhudi za kupata matibabu ya haraka huwa ni changamoto katika hospitali hiyo kwa sababu ya ukosefu wa vifaa vya kisasa vya upasuaji wa macho.

Hali hii mara nyingi huwa inawalazimu madaktari kuwapa wagonjwa wao rufaa za nje ya Lamu au hata kuwaomba kusubiri hadi pale kambi za matibabu ya bure ya macho zitakapoandaliwa mjini humo.

Imebainika kuwa, baadhi ya wazee wamegeuka vipofu, hasa baada ya kuathirika kwa muda mrefu bila matibabu.

Mtaalamu wa afya akitekeleza upasuaji wa macho kwenye hospitali ya King Fahd mjini Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Wataalamu wa masuala ya afya eneo hilo wanakiri kuwa, takwimu za maradhi ya macho zimekuwa zikilingana na zile za kisukari miongoni mwa wazee hivyo kuibua uwezekano wa uhusiano baina ya magonjwa haya.

Ripoti ya hivi majuzi kutoka wizara hiyo iliashiria kuwa idadi kubwa ya wakazi hasa wale wa kuanzia umri wa miaka 40 na zaidi wanaugua kisukari na shinikizo la damu.

Kulingana na ripoti hiyo jumla ya wagonjwa 2,509 wa shinikizo la damu na wengine 1,067 wa kisukari walipatikana Lamu katika kipindi cha mwaka mmoja.

Waziri wa Afya katika Kaunti ya Lamu, Dkt Anne Gathoni, anawahimiza wakazi kufanya mazoezi mara kwa mara na kula vyakula kudhibiti nguvu yao ya kuona na pia kuepuka maradhi kama vile kisukari na shinikizo la damu yanayosababisha nguvu ya macho kupotea.

Kulingana na Dkt Gathoni, wakazi wengi eneo hilo wamepuuzilia mazoezi ya viungo, hivyo kuwaweka kwenye hatari zaidi ya kuugua kisukari, shinikizo la damu na maradhi mengine yanayoambatana nayo.

“Ningewasihi wananchi kuwa makini wanapokula. Waache kutumia sukari na chumvi nyingi kwenye mlo wao ambao mara nyingi huwasababishia maradhi ya sukari na shinikizo la damu. Pia wafanye mazoezi. Wakizingatia haya wataepuka haya maradhi ya kisukari na mengineyo,” akasema.

Kulingana na ripoti iliyochapishwa kwenye jarida la masuala ya kisukari la World Journal of Diabetes 2019, kisukari kina uwezo wa kuathiri sehemu yoyote ya macho ingawa cataract ndiyo huathiriwa sana.

Ripoti hiyo inasema ingawa kuna teknolojia za kisasa za upasuaji wa macho kwa njia salama, bado wagonjwa wengi wa kisukari huwa hatarini kupatwa na upofu.

“Tafiti kadha za kimatibabu zimeonyesha kuwa cataract hutokea sana kwa wagonjwa wa kisukari kuliko wale wasiougua kisukari. Kutokana na kuwa idadi ya wagonjwa wa kisukari imetabiriwa kuongezeka katika siku za usoni, upasuaji utaendelea kuwa jambo muhimu la kuzingatiwa ,” ikaeleza ripoti hiyo.

Wataalamu hao wanasema maradhi ya macho kwa wagonjwa wa kisukari ni rahisi kutibiwa kwa vijana ikilinganishwa na wazee.

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), idadi ya watu waliougua kisukari iliongezeka kutoka milioni 108 mwaka wa 1980 hadi milioni 422 mwaka wa 2014 huku idadi hiyo ikiendelea kuongezeka kwa kasi ya ajabu katika nchi za mapato ya chini na ya kati.

Wakfu wa Kimataifa wa Kisukari unakadiria kuwa, takriban watu milioni 537 wenye umri kati ya miaka 20 na 79 ulimwenguni wanaugua kisukari.

Idadi hiyo imetabiriwa kuongezeka hadi milioni 643 kufikia mwaka wa 2030 na hadi milioni 783 kufikia mwaka wa 2045.

Hata hivyo, mtaalamu wa upasuaji wa macho kutoka Hospitali ya Macho ya Lions, Dkt Evans Cherono, anasema kando na magonjwa ya kisukari, hali ya kimazingira na uzee pia zimeibuka kuwa chanzo cha maradhi ya macho Lamu.

Dkt Cherono anawashauri wakazi kuzingatia uchunguzi wa mapema wa macho ili tatizo ligunduliwe na kutibiwa.

Mtaalamu huyo pia alitaja lishe duni kama chanzo kingine.

Chumba cha upasuaji kwenye hospitali kuu ya King Fahd mjini Lamu.
PICHA | KALUME KAZUNGU

Baadhi ya waathiriwa wanasema kuwa, bei ghali ya uchunguzi ni kizingiti.

Geni Hassan, 63, anawasihi wataalamu kuandaa kambi za matibabu kila mara ili kuwasaidia wanaoshindwa kusaka matibabu kutokana na umaskini.

“Nimesumbuka na ugonjwa wa macho kwa zaidi ya miaka mitatu. Matibabu ya macho huwa ni ghali mno. Ningeomba wahisani zaidi kujitokeza ili kusaidia hawa wagonjwa wa macho, wengi wakiwa ni sisi wazee,” akasema.

Mkazi huyo wa Lamu ni miongoni mwa wale ambao walifanyiwa upasuaji kupitia kambi ya bure ya matibabu ya macho iliyoandaliwa na kampuni ya Nation Media kwa ushirikiano na wakfu wa TeamPankaj, mwaka 2021 na sasa amepata nafuu na anaona vyema.

Ahmed Mzee, mkazi mwingine pia alipona baada ya kupokea tiba kupitia kambi ya bure ya macho iliyoandaliwa wakati wa hafla ya Maulid ya Lamu mwaka 2021.

Anaeleza haja ya wataalamu kufanya warsha za mara kwa maraka kuhamasisha wakazi kuhusu na jinsi ya kuepuka matatizo ya macho.

Pia ameomba serikali ya kaunti kuboresha miundomsingi ya afya eneo hilo, hasa kliniki za macho ili kuwasaidia wenye matatizo hayo.

  • Tags

You can share this post!

Ruto atarajiwa Pwani wandani wakizozana

Sonko aanza kusuasua

T L