• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 11:46 AM
Tim Wanyonyi sasa ndiye mwaniaji ubunge Westlands kwa tiketi ya ODM, Gumo asalimu amri na kumpisha

Tim Wanyonyi sasa ndiye mwaniaji ubunge Westlands kwa tiketi ya ODM, Gumo asalimu amri na kumpisha

NA CHARLES WASONGA

ODM imetangaza kuwa mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi ndiye atatetea kiti chake kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Hii ni baada ya mshindani wake mkuu Michael Gumo kujiondoa Jumapili, Mei 8, 2022 na kutangaza kuwa atamuunga mkono.

Akiongea na wanahabari katika mkahawa wa Serena Nairobi, mkurugenzi wa uchaguzi wa ODM Junet Mohamed alisema kuwa hatua hiyo ilifikiwa kufuatia makubaliano kati ya Wanyonyi na Gumo.

“Wawili hawa wamekubaliana kuhusu suala hili. Sasa Mheshimiwa Tim Wanyonyi ndiye atapeperusha bendera ya ODM katika eneo bunge la Westlands. Maafikiano hayo ni kwa manufaa ya chama chetu kwani kitatuwezesha kuhifadhi kiti hicho,” Bw Mohamed akaongeza.

Kwa upande wake, Bw Gumo alisema kuwa ameamua kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho kwa hiari yake bila kushurutishwa na mtu yeyote.

“Naamini kuwa hatua hii ni ya busara na itawezesha muungano wetu wa Azimio na chama chetu cha ODM. Kwa hivyo, wapinzani wetu wafahamu kwamba Westlands ingali ngome ya ODM,” akasema.

Michael Gumo akihutubu jijini Nairobi, Jumapili, Mei 8, 2022. PICHA | CHARLES WASONGA

Tangazo hilo lilijiri baada ya Jopo la Kutatua Mizozo katika Vyama vya Kisiasa (PPDT) kufutilia mbali uteuzi wa Bw Wanyonyi na kuamuru ODM ifanye kura nyingine ya mchujo katika eneobunge la Westlands ndani ya saa 72.

Hii ni baada ya Bw Gumo kulalamikia hatua ya ODM kumkabidhi Bw Wanyonyi tiketi ya uteuzi kuwania kiti hicho ilhali yeye (Gumo) ndiye aliibuka mshindi katika kura hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Ukarimu wa Ruto wampa makanisa

Beki Mkenya Okumu amaliza ukame mkali wa magoli Ubelgiji

T L