• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Tulikupa kazi AU lakini sasa unaharibu sifa ya nchi, Ruto amkejeli Raila

Tulikupa kazi AU lakini sasa unaharibu sifa ya nchi, Ruto amkejeli Raila

Na PETER MBURU

MAKABILIANO ya kisiasa kuhusu sakata ya biashara ya dhahabu feki yanazidi kuvutia hisia kali, Naibu Rais William Ruto akiendelea kutumia fursa hiyo kumkejeli kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Dkt Ruto Jumapili alidai kuwa chama cha Jubilee ndicho kilimtafutia kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kazi katika Muungano wa Afrika, na kuongeza kuwa hawakuwa na maelewano atumie nafasi hiyo kufanya biashara za kuuza madini.

“Sehemu ya kazi ya rafiki yetu ambayo tulimtetea AU haikuhusisha kushiriki biashara za madini ama kuuza mali ama dhahabu za aina yoyote. Lazima alitekwa na wakora na ndio wamemwingiza kwa hayo maneno ya madini na dhahabu ambayo ni feki,” Dkt Ruto akasema alipokuwa katika kanisa la St Xavier, Naivasha.

Naibu Rais aliwalaumu washirika katika sakata hiyo kuwa wanaingiza jina la Rais ndani yake, na kuchafua Jubilee.

Aliendelea kusema kuwa sakata hiyo inaweza kuharibu uhusiano baina ya Nairobi na Dubai.

“Wasiweke hatarini nafasi za kazi na biashara ya Wakenya kule Dubai kwa sababu ya kukimbizana na dhahabu feki,” akasema.

Alisema kazi ambayo walimtafutia Bw Odinga katika idara ya miundomsingi haikuhusisha kuwa akishiriki biashara ya madini.

“Hatuna wakora Jubilee. Hiyo ni biashara ya watu wa huko nje ambao tunawajua,” akasema.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Naibu Rais kusema kuwa alikuwa mmoja wa waliomtafutia Bw Odinga kazi AU.

Pamoja na wafuasi wake ambao walikuwa wameandamana katika kanisa katoliki la St Xavier, Naivasha, walimkashifu Bw Odinga kuwa anachafulia serikali jina katika mashirika ya kimataifa na mataifa ya nje.

You can share this post!

BI TAIFA MEI 09, 2019

Unaaibisha Pwani, Kingi amwambia Jumwa

adminleo