• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Uhuru asisitiza mipango ya BBI bado ipo

Uhuru asisitiza mipango ya BBI bado ipo

Na WAANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta amesisitiza kuwa mpango wa kurekebisha katiba bado upo, huku akiwasuta wanasiasa wanaopinga mipango hiyo.

Urekebishaji katiba kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI) ulipigwa breki wakati mahakama kuu ilipoamua ulikuwa haramu, na kuna kesi ya rufaa inayojaribu kufufua shughuli hiyo.

“Mimi sitishwi na mtu. Waseme wanavyotaka. Sisi tunataka kupitisha hii BBI ili tuhakikishe hakuna mtu anaweza kumhamisha mwenzake popote, kuwe na haki na sauti ya kila Mkenya itiliwe maanani kila mahali,” Rais alisema jana akiwa eneo la Rabai, Kaunti ya Kilifi.

Alikuwa katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kukabidhi wananchi hatimiliki za ardhi 2,100.

Msimamo huo wa rais ni sawa na ule ambao umekuwa ukitolewa na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga ambaye husema kuwa mchakato wa BBI uko katika kipindi cha mapumziko.

Wakosoaji wa marekebisho ya katiba wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto wameendelea kudai kuwa mpango huo unalenga kunufaisha wanasiasa wachache wanaomezea mate viti vitakavyoundwa kama vile vya waziri mkuu na manaibu wake endapo katiba itarekebishwa.

Wakati huo huo, Rais Kenyatta ambaye aliandamana na viongozi mbalimbali akiwemo Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, aliingilia mjadala ulioibuka nchini kuhusu uundaji wa muungano mkubwa wa kisiasa kabla mwaka wa 2022.

Duru zimekuwa zikisema rais ananuia kuleta pamoja vigogo wa kisiasa waliokuwa katika mrengo wa NASA mwaka wa 2017, ili waungane na wengine katika uchaguzi ujao.

Vigogo hao wanajumuisha Bw Odinga, Kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, Mwenyekiti wa KANU Gideon Moi ambaye pia ni Seneta wa Baringo, na Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula.

Kumekuwa na sintofahamu kuhusu muungano wa One Kenya Alliance (OKA) ulioanzishwa na Mabw Mudavadi, Moi, Musyoka na Wetang’ula kwa vile inasemekana hawajaelewana kuhusu mwelekeo watakaochukua.

Kuna uwezekano wa muungano huo kumtenga Bw Odinga kwani wenzake waliokuwa pamoja katika NASA wanasisitiza kuwa walikubaliana ataunga mkono mmoja wao katika uchaguzi ujao, msimamo ambao unapingwa na ODM.

“Wale ambao hawataki watu waje pamoja, hao si watu walio na suluhu kwa shida zinazotukumba. Lazima tuhakikishe tumepata njia ambayo viongozi watakaa pamoja, washirikiane kuleta Wakenya pamoja wala si kuwatenganisha. Kutenganisha viongozi kutaleta vita kwa wananchi na tunataka amani. Hiyo ndiyo barabara ninaomba wenzangu wafuate muone hatua tutakayopiga,” akasema.

Ziara ya rais eneo la Kilifi na Pwani kwa jumla imefanyika siku chache baada ya Dkt Ruto kuzuru eneo hilo kupigia debe azimio lake la kutaka kuwania urais 2022.

Ripoti za Anthony Kitimo, Maureen Ongala na Valentine Obara

You can share this post!

Majaji wanaswa

Wazazi wa watoto waliouawa wakiri walijua Masten Wanjala