• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Vinara wa OKA wasema wataamua mgombea urais wao mwezi ujao

Vinara wa OKA wasema wataamua mgombea urais wao mwezi ujao

Na WANDERI KAMAU

MUUNGANO wa Okoa Kenya Alliance (OKA) utaanza rasmi harakati ya kumtafuta mgombea urais kuanzia Februari 18, walisema jana vinara wa muungano huo.

Vinara hao – Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (Kanu) – walisema watafanya kikao cha faragha kutathmini ripoti kutoka kwa Jopo Maalum linaloendesha mchakato wa kutathmini kiongozi anayefaa zaidi kutwaa nafasi hiyo.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, vinara hao walisema watamuunga mkono yule atakayechaguliwa kuchukua nafasi hiyo.

“Baada ya mchakato huo kukamilika, tutamuunga mkono kikamilifu yule ambaye atachaguliwa kupeperusha bendera ya muungano huu, kwani atawakilisha matakwa ya mamilioni ya Wakenya wanaotuamini,” akasema Bw Mudavadi.

Kauli yao inajiri huku vumi zikiendelea kusambaa kwamba muungano huo umevurugika.Vinara hao wamekuwa wakilaumiwa kwa kufanya misururu ya mikutano bila kutangaza mikakati yao halisi ya kisiasa kukabiliana na ushindani kutoka kwa Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Ni hali ambayo imewafanya baadhi ya washirika wao kuhama au kutoa makataa ya kuuhama muungano huo.Baadhi ya wanasiasa ambao wamehama ni mbunge Ayub Savula (Lugari), ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Mudavadi.

Bw Savula ametangaza kuingia katika kambi ya Azimio la Umoja, inayomuunga mkono Bw Odinga.Seneta Cleophas Malala (Kakamega) naye ametishia kuhama ikiwa vinara hao hawatatangaza rasmi mwaniaji.

“Tumengoja sana vinara wetu kutwambia yule atakayepeperusha bendera ya OKA kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti. Ikiwa wataendelea kuchelewa, basi nitahamia katika mrengo mwingine,” akasema Bw Malala.

Seneta huyo alisema kuna hatari muungano huo kupoteza ushawishi wake, ikizingatiwa Dkt Ruto na Bw Odinga wamekuwa wakifanya kampeni katika sehemu mbalimbali nchini kuvumisha azma zao.

Kando na hayo, Mabwana Kalonzo na Gideon wamekuwa wakilaumiwa kwa “kuelekeza malengo yao ya kisiasa kwingineko.”

Kwa mara kadhaa, Bw Musyoka amekosekana kwenye mikutano kadhaa ya muungano huo, huku Gideon akionekana kumpendelea Bw Odinga.

Ijapokuwa wawili hao walikuwa kwenye kikao cha jana na kusisitiza kuwa muungano huo ungali thabiti, wadadisi wanasema vinara hao wana kibarua kikubwa kuthibitisha kuwa bado wako pamoja kisiasa.

Wanasema lengo kuu la kila kinara ni kuhakikisha hatakuwa kwenye baridi ya kisiasa baada ya uchaguzi wa Agosti.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yaweka kafyu ya siku 30 kukabili uvamizi Lamu

Gavana Muriithi kusimamia kampeni za Raila

T L