• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Gavana Muriithi kusimamia kampeni za Raila

Gavana Muriithi kusimamia kampeni za Raila

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga, amedhihirisha imani yake katika eneo la Mlima Kenya kwa kuteua Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi, mpwa wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, kusimamia bodi ya kampeni zake za urais.

Bw Odinga ambaye ametangaza azma yake ya kugombea urais kwa mara ya tano, alimteua Gavana Muriithi, mtaalamu wa masuala ya uchumi kuwa mwenyekiti wa bodi ya kampeni zake, huku Bi Elizabeth Meyo, ambaye pia ni mtaalamu wa uchumi, akiwa Afisa Mkuu Mtendaji na katibu wa bodi hiyo.

Bw Muriithi ni mmoja wa magavana wanne wa Mlima Kenya waliotwikwa jukumu la kumpigia debe Bw Odinga katika eneo la Mlima Kenya na Rais Uhuru Kenyatta, na ni mwana wa kaka wa Bw Kibaki, Phillip Muriithi Kibaki.

Hii ni mara ya kwanza kwa Bw Odinga kuteua mtaalamu kutoka eneo la Mlima Kenya kusimamia kampeni zake huku wataalamu wakisema uamuzi huo ulishawishiwa pakubwa na Rais Kenyatta na mabwanyenye wa eneo hilo ambao wanaunga azima yake.

“Kuna mkono wa Rais Kenyatta na pia wa mabwanyenye wa Mlima Kenya ambao wanaamini hekima na mchango wa Bw Muriithi katika masuala ya kisiasa na kiuchumi,” alisema mdadisi wa siasa Francis Kimenye.

Bw Muriithi alitekeleza wajibu muhimu katika kampeni za Bw Kibaki mwaka wa 2007 ‘chini ya maji’ na kuteuliwa waziri msaidizi wa viwanda.

Alikuwa mbunge wa Laikipia Magharibi wakati huo.“Kwa kumteua Bw Muriithi, Bw Odinga amehakikisha Mlima Kenya umehisi na kuamini kwamba unamiliki kampeni zake,” asema Kimenye.

Mlima Kenya

Kwa baraka za Rais Kenyatta, Bw Muriithi amekuwa akiandamana na Bw Odinga katika ziara zake zote eneo la Kati na alihudhuria kikao cha Bw Odinga na wafanyabiashara matajiri wa eneo la Mlima Kenya katika hoteli ya Safari Park, Nairobi walipotangaza ndiye chaguo lao la rais.

Alikuwa gavana wa kwanza kualika Bw Odinga eneo la Mlima Kenya na amekuwa mmoja wa viongozi wa Mlima Kenya wanaopigiwa upato kuteuliwa mgombea mwenza wa waziri mkuu huyo za zamani kwenye uchaguzi wa Agosti 9 mwaka huu.

Duru zinasema kuwa ni kutokana na utaalamu wake katika masuala ya uchumi, siasa na uhusiano wake mwema na mashirika ya kimataifa kama vile Benki ya Dunia alikohudumu kabla ya kugombea ugavana kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, pamoja na imani ya wafanyabiashara wa Mlima Kenya kwake, ndipo Rais Kenyatta akamwamini kwa wadhifa wa kumpigia debe Bw Odinga eneo la Mlima Kenya.

Bw Muriithi pia ni mmoja wa viongozi wachache wasio na doa la ufisadi, na anaaminiwa sana na Mzee Kibaki.

Kwa kuteua wataalamu wa uchumi kusimamia kampeni zake, Bw Odinga ameonyesha kujitolea kwake kuyapa masuala ya uchumi kipaumbele akishinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

“Ni mkakati unaolenga kuonyesha Mlima Kenya kuwa ameweka suala la uchumi katika mipango yake,” asema. Bw Odinga alisema bodi ya kampeni zake za urais itakuwa injini itakayohakikisha kuwa anamrithi Rais Kenyatta baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Muriithi ambaye alikubali uteuzi huo ndiye mwenyekiti wa kamati ya masuala ya fedha, mipango na uchumi ya Baraza la Magavana kuanzia Januari 2021.

Bw Odinga amemsifu kwa kubadilisha uchumi na utumishi wa umma katika kaunti yake iliyokumbatia utaalamu na viwango vya utendakazi vya kimataifa.

Bi Meyo ambaye ni kamishna wa zamani wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru ya Kenya (KRA) na mshauri wa Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF), atatekeleza maamuzi ya bodi ya kampeni za Bw Odinga na atakuwa msemaji wa pekee wa bodi hiyo.

Aidha, wana wa marais wote waliotawala Kenya, wakijumuisha Rais Uhuru, Gideon Moi na Jimmy Kibaki wameonyesha nia ya kuunga mkono azimio la Bw Raila. kutwaa urais wa nchi.

  • Tags

You can share this post!

Vinara wa OKA wasema wataamua mgombea urais wao mwezi ujao

Amazon Ladies imani ipo siku itawika katika handiboli

T L