• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Viongozi wa ODM wakana kulegea

Viongozi wa ODM wakana kulegea

Na WINNIE ATIENO

WANASIASA wandani wa Gavana wa Mombasa, Hassan Joho, wamejipiga kifua kwamba wana uwezo wa kutosha kudhibiti kampeni za ODM katika kaunti hiyo bila yeye kuwepo.

Bw Joho amekuwa akijishughulisha na siasa za kitaifa baada ya kinara wa ODM, Raila Odinga kumjumuisha kwenye kikosi chake kikuu, hali iliyofanya kampeni za chama hicho Mombasa na Pwani kwa jumla kukosa uchangamfu uliokuwa ukionekana wakati alipoziongoza.

Huku wakionekana kusuta jinsi Taifa Leo ilivyofichua ulegevu wa ODM kuandaa kampeni kubwa tangu Bw Joho kukosekana mashinani, wanasiasa hao walisema watahakikisha ufuasi wa Bw Odinga utakuwa thabiti zaidi kuelekea kwa Uchaguzi Mkuu wa Agosti.

Waliongozwa na Mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir, mwenzake wa Jomvu, Badi Twalib na wa Likoni, Mishi Mboko.

“Bw Joho amepanda juu na tunamtakia kila la kheri. Tuliobakia tuko na uwezo kupeleka chama cha ODM mbele. Pwani itafaidi sana na uongozi wa Bw Odinga kwa hivyo tuchukue kadi za kura, tumuunge mkono, tupige kura kwa wingi. Mombasa ni ngome ya ODM,” akasema Bw Nassir.

Alikuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa katika uwanja wa Mvita. Mkutano huo uliitishwa kwenda sambamba na ule wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA) ulioongozwa na Naibu Rais William Ruto, katika uwanja mkubwa wa Tononoka.

Imekuwa muda mrefu tangu mkutano wa kisiasa kuandaliwa katika uwanja huo ambao vigogo wa kisiasa wakati mwingi huutumia kudhihirisha ubabe wao wa kuvutia umati Mombasa.

Kwa upande wake, Bw Twalib aliwasihi wanachama wa Azimio La Umoja kusimama kidete na kuacha kuzozana ili Bw Odinga ashinde.

Naye Bi Mboko alisema Bw Odinga ndiye kiongozi atakayeleta amani, umoja na ajira kwa vijana.

“Tusikubali kuganywa kwa misingi ya kikabila na kidini,” alisema Bi Mboko.

Wabunge hao pia walichukua fursa hiyo kumpigia debe Bw Nassir kuchaguliwa gavana wa Mombasa wakisema ataendeleza kazi za Bw Joho.

Wakati huo huo, walitoa wito kwa Bw Odinga kumpa Bw Joho cheo cha juu serikalini iwapo atashinda urais ifikapo Agosti.

Bw Joho ambaye anamaliza hatamu yake ya ugavana wa miaka miwili amekuwa akionekana akiandamana na Bw Odinga kwenye kampeni zake za kuwania Urais. Kwa muda sasa gavana huyo amepotea katika siasa za Mombasa.

Wiki iliyopita, Taifa Leo ilifichua kupitia kwa uchanganuzi jinsi ukosefu wa Bw Joho kwa siasa za Pwani umempa Dkt Ruto mwanya wa kupiga kampeni nyingi kaunti zote za ukanda huo ikilinganishwa na ODM ambayo huchukulia Pwani kama ngome yake ya kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo akana madai ya kutoa masharti kwa Raila

Msitu wa Arsenal kunyanyua hadhi ya kijiji cha Shingwaya

T L