• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Vyama huru kutoa tiketi bila mchujo

Vyama huru kutoa tiketi bila mchujo

NA CHARLES WASONGA

VYAMA vya kisiasa viko huru kutoa tiketi ya moja kwa moja kwa wawaniaji wa viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao, Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu amesema.

Hata hivyo, alieleza kuwa vyama hivyo sharti vihakikishe kuwa wawaniaji, afisi yake na umma kwa ujum – la unajulishwa kuhusu sababu ya vyama husika kuamua kutumia mbinu hiyo ya uteuzi.

“Sheria inaviruhusu vyama kuteua wagombeaji wao kwa njia ya kura za mchujo au mfumo wa mwafaka, kura ya maoni au uteuzi wa moja kwa moja. Lakini sharti vyama hivyo vijulishe afisi yangu na umma kwa ujumla kuhusu mfumo utakaotumika,” Bi Nderitu akasema jana kwenye kikao na wanahabari afisini mwake, Nairobi.

Msajili huyo wa vyama alisema kuwa wawaniaji ambao watahisi kuwa hawakutendewa haki katika shughuli hiyo ya uteuzi inayoanza Ijumaa wiki hii wako huru kuwasalisha malalamishi yao kwa kamati ya kushughulikia masuala hayo ndani ya vyama hivyo.

“Wawaniaji husika pia wanaweza kuwasilisha malalamishi yao kwa Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDRT) au mahakamani,” Bi Nderitu akaeleza, huku akishikilia kuwa siku ya mwisho kwa vyama kukamilisha mchujo wa wawaniaji ni Aprili 22.

Mwishoni mwa wiki jana chama cha ODM kilitoa tiketi za moja kwa moja kwa baadhi ya wawaniaji wa viti mbalimbali katika ngome zake za Pwani, Magharibi na Nyanza.

Hatua hiyo iliibua malalamishi miongoni mwa wawaniaji wengine waliokuwa wakisubiri kushiriki kura za mchujo kuanzia Ijumaa wiki hii.

Kwa mfano, katika Kaunti ya Kwale, chama hicho kimempa tiketi ya moja kwa moja aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Kilimo, Hamadi Boga kuwania ugavana wa kaunti hiyo.

Aidha, ODM ilifutilia mbali kura ya mchujo ya ugavana katika Kaunti ya Kakamega na kuamua kumteua aliyekuwa mkurugenzi wa kampuni ya Ketraco, Fernandes Barasa kuwania ugavana katika kaunti hiyo.

Wengine waliopokezwa tiketi ya moja kwa moja kutetea viti kwa tiketi ya ODM ni wabunge Tindi Mwale (Butere), Titus Khalama (Lurambi), Christopher Aseka (Khwisero), Emmanuel Wangwe (Navakholo) na Benard Shinali (Ikolomani).

Hatua hiyo imezuia malalamishi miongoni mwa wawaniaji wengine ambao tayari walikuwa wamelipa ada za uteuzi huku baadhi yao wakitisha kugura ODM na kuwania viti kama wagombeaji wa kujitegemea.

Hata hivyo, mwenyeketi wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) wa chama hicho Catherine Mumma ametetea hatua hiyo akisema inalandana na sheria za uteuzi katika ODM.

  • Tags

You can share this post!

#KCPE2021: Mabingwa wafichua siri ya ufanisi wao

Usajili wa boda kusaidia vita dhidi ya ugaidi –...

T L