• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wabunge wa ODM waogopa ‘cheo’ cha Raila

Wabunge wa ODM waogopa ‘cheo’ cha Raila

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE wamepinga mpango wa kubuni Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani Bungeni wakihofia kwamba, itaua afisi ya Kiongozi wa Wachache na kumeza majukumu ya kamati za bunge.

Kinaya ni kwamba, wabunge wa mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya unaoongozwa na Raila Odinga ndio wamepinga pendekezo hilo.

Hii ni licha ya kwamba, Bw Odinga ndiye anatarajiwa kushikilia wadhifa huo endapo pendekezo hilo la Rais William Ruto litatekelezwa anavyodhamiria.

Kulingana na pendekezo hilo, Kiongozi Rasmi wa Upinzani atatengewa fedha za matumizi kutoka hazina ya kitaifa huku akiwa na mamlaka ya kuajiri maafisa wa kumsaidia kutekeleza majukumu ya afisi hiyo.

Wakati wa mjadala, wa siku mbili, bungeni kuhusu pendekezo ambalo ni miongoni mwa mapendekezo manne kwenye memoranda ya Dkt Ruto, Wabunge hao wakiongozwa na kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi pia walipinga wazo la kuwaruhusu mawaziri kufika bungeni kujibu maswali bungeni.

“Afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani haiwezi kuundwa katika wakati huu Kenya bado inaendesha mfumo wa utawala wa urais ambapo wabunge wa mirengo yote wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja kuhakiki utendakazi wa serikali. Tukiruhusu kubuniwa kwa afisi hii, basi hakutakuwepo na afisi ya kiongozi wa wachache inayopendekezwa kwenye kipengele cha 108 cha Katiba ya sasa,” akasema mbunge wa Ugunja.

Bw Wandayi, ambaye ni mwandani wa karibu Bw Odinga, alisema Rais Ruto anaongozwa na nia mbaya kupendekeza kubuniwa kwa afisa wakati amefaulu “kuwanunua wabunge wa mrengo wa Azimio.”

“Hata kama muujiza utokea kwamba, Rais Ruto amefaulu kuunda afisi hiyo, kiongozi huyo wa upinzani hataweza kufaulu kutekeleza wajibu wake kwa sababu hatakuwa na wabunge tosha wa kumsadia kazi. Lakini ukweli ni kwamba, marekebisho ya katiba ya kuunda afisi hiyo sharti yaidhinishwe katika kura ya maamuzi,” akasisitiza.

Washirika wengine wa karibu wa Bw Odinga waliopinga wazo hilo, wakati mjadala wa hoja hiyo Jumatano na Alhamisi, walikuwa ni mbunge maalum John Mbadi, Otiende Amollo (Rarieda), Peter Kaluma (Homa Bay Mjini), Wilberforce Oundo (Funyula), James Nyikal (Seme) miongoni mwa wengine.

“Kubuniwa kwa afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani, bila kubadilishwa kwa mfumo wa utawala, kutabadili kabisa muundo wa Bunge. Afisi hiyo itameza majukumu ya Kamati za Bunge za Kuhakiki Utendakazi wa Wizara, Idara na Masharika ya Serikali Kuu kama vile Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) na Kamati ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC),” akasema Bw Mbadi ambaye ni mwenyekiti wa ODM.

Bw upande wake, Bw Otiende, alionya kuwa, mchakato huo wa marekebisho ya katiba anavyopendekeza Rais Ruto, utabatilishwa na mahakama sawa na ule wa BBI.

“Kwa kuwasilisha memoranda bungeni yenye mapendekezo kuhusu marekebisho ya Katiba, Rais Ruto anaanzisha mchakato wa marekebisho ya katiba yanayolenga kubadili muundo wa serikali. Hapa Rais amerudia kosa ambalo lilitendwa na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta, na kupelekea mchakato wa BBI kuzimwa na mahakama,” akasema mbunge huyo ambaye ni wakili mwenye tajriba ya juu.

Bw Otiende, ambaye ni mmoja wa wataalamu wa kisheria walioandika Katiba ya sasa, alipendekeza kuwa Kenya irejelee mfumo wa utawala wa ubunge “ikiwa kuna mwafaka kwamba mfumo wa urais hauafiki matakwa ya nchi hii”.

“Rais Ruto asijidanganye kwamba, anaweza kuanzisha afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani bunge, kuwaleta mawaziri bunge na kufanikisha usawa wa kijinsia bungeni bila kubadili mfumo wa uongozi wa taifa hili. Afisi ya kiongozi wa upinzani haitakuwa na maana yoyote wakati huu ambapo kuna kamati za bunge za kuhakiki wizara za serikali,” akaeleza.

Hata hivyo, wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza waliunga mkono pendekezo hilo wakisema utaimarisha utendakazi wa upinzani.

“Kama kungekuwa na afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani, Raila angefanya kazi yake ya kukosoa serikali kwa njia rasmi badala ya kuchochea fujo nchi kupitia mikutano na maandamano barabarani,” akasema kiongozi wa wengine Kimani Ichung’wa.

Wabunge wengine waliounga mkono mapendekezo ya Rais Ruto, wakati wa mjadala huo ni; Ferdiand Wanyonyi (Kwanza), Didmus Barasa (Kimilili), David Gikaria (Nakuru Mjini Mashariki), Dido Rasso (Saku) miongoni mwa wengine.

Inatarajiwa kuwa endapo afisi hiyo itabuniwa, itatoa afueni kwa Bw Odinga na Bi Martha Karua ambao waligombea urais kwa tiketi moja na kushindwa na Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Wanasiasa wa Mlima Kenya watumie akili au...

Wanawake washtuka kugundua waume wao ni mashoga

T L