• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
Wabunge wapya wafika bungeni kuelewa mazingira ya kazi

Wabunge wapya wafika bungeni kuelewa mazingira ya kazi

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE wateule 286 Agosti 25 walianza kufika bungeni kwa mara ya kwanza tangu kuchaguliwa ili kujiandisha rasmi na kupewa uhamasisho kuhusu utendakazi wa bunge.

Wabunge wa zamani waliofaulu kudumisha viti vyao baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, pia waliandikishwa upya katika shughuli hiyo inayokamilishwa Ijumaa.

Kaimu Karani wa Bunge la Kitaifa Sera Kioko hata hivyo alisema kuwa wabunge hao wateule wanahitajika kuwasilisha vitambulisho vyao vya kitaifa au paspoti, nambari ya utambulisho kutoka Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) na cheti cha ushindi walichopewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Aidha, wabunge wateule wanahitaji kujaza maelezo yao katika fomu maalum kutoka kwa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) na kuwasilisha wasifu wao kwa ajili ya kuwekwa katika kumbukumbu za bunge.

“Hata hivyo, leo (Alhamisi)  wabunge hawa hawatapewa afisi kwa sababu hawajaapishwa rasmi kama wabunge. Kwa hivyo, kimsingi, shughuli ya leo ni ya kuchukua maelezo ya wabunge hawa wateule na kuwatembeza katika majengo ya bunge ili wawe na ufahamu kuhusu masuala kadha ya kimsingi,” Bi Kioko akawaambia wanahabari.

Kulingana na sheria, Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kutoa notisi ya kuitisha kikao cha kwanza cha bunge ndani ya siku 30 baada ya uchaguzi mkuu.

Hii ina maana kuwa wabunge hawa wapya watafanya kikao cha kwanza kabla ya tarehe tisa mwezi ujao wa Septemba, Rais Kenyatta atakapotoa notisi hiyo kupitia gazeti rasmi la serikali.

Mbunge mpya wa Suba Kusini Caroli Omondi ni miongoni waliofika bungeni Agosti 25, 2022 kwa uhamasisho. PICHA | CHARLES WASONGA

Miongoni mwa wapya waliofika katika majengo ya bunge jana ni pamoja na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Bomet Linet Chepkorir maarufu kama ‘Toto’, Amos Mwago (Starehe), Omondi Caroli (Suba Kusini), Nabii Nabwera (Lugari), Njeri Maina (Mbunge Mwakilishi wa Kike Kirinyaga), Kenga Mupe (Rabai), Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o (Langata) miongoni mwa wengine.

Mbunge mpya wa Lugari Nabii Nabwera. PICHA |  CHARLES WASONGA

Kwa ujumla wabunge 161 walichaguliwa kwa tiketi ya vyama tanzu katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya huku wabunge 159 wakichaguliwa kwa tiketi ya muungano wa Kenya Kwanza.

Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kirinyaga Njeri Maina. Ni Mbunge mpya aliyechukua mahala pa Wangui Ngirici aliyewania ugavana na akashindwa na Anne Waiguru. PICHA | CHARLES WASONGA

Wabunge wengine 12 walichaguliwa kwa tiketi huru bila kudhaminiwa na chama chochote cha kisiasa.

Wabunge hao ni pamoja na; Rahim Dawood (Imenti Kaskazini), Ronald Karauri (Kasarani), Elijah Njoroge (Gatundu Kaskazini), Shakeel Shabbir (Kisumu Mashariki), Timothy Toroitich (Marakwet Magharibi), Joshua Mwalyo (Masinga), Nebert Muriuki (Mbeere Kusini), Geoffrey Mulanya (Nambale) na Kitilai Ntutu (Narok Kusini).

Mbunge mpya wa Kasarani Ronald Karauri akiongea na wahabari katika Majengo ya Bunge, Agosti 25, 2022. PICHA | CHARLES WASONGA 

Wabunge Wawakilishi waliochaguliwa kwa tiketi huru ni; Fatuma Mohamed (Migori), Caroline Ngelechei (Elgeyo-Marakwet) na Monica Muthoni (Lamu).

Maeneo bunge manne hayana wabunge baada ya uchaguzi katika maeneo hayo kuahirishwa na IEBC kufuatia hitilafu katika karatasi za kupigia kura. Maeneo hayo ni; Kacheiba, Pokot Kusini, Rongai na Kitui Mashambani.

  • Tags

You can share this post!

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Kuvumiliana na kupendana ndiko...

Barcelona, Bayern Munich na Inter Milan watiwa katika kundi...

T L