• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Kuvumiliana na kupendana ndiko huleta amani na umoja katika nchi yoyote ile

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Kuvumiliana na kupendana ndiko huleta amani na umoja katika nchi yoyote ile

NA WALLAH BIN WALLAH

UVUMILIVU ndio ufunguo wa faraja na amani! Nchi yetu imetunukiwa neema na faraja tele!

Lakini badala ya kuneemeka na kufarijika kutokana na tunu hizo adhimu, nyakati nyingine hutokea tukaishi kwa wasiwasi na wahaka nyoyoni kwa sababu ya kutovumiliana tu!

Mvumilivu hula mbivu! Kuvumilia maishani kunaleta mbivu! Kuyavumilia matatizo kunalisha mbivu! Na ukimvumilia mja mwenzako ukaishi naye kwa furaha, upendo na ushirikiano, mtakula mbivu ya kuishi kwa amani! Tuvumiliane tuvune amani, tupate umoja ili tule matunda ya upendo nchini mwetu!

Ni masikitiko makubwa kwamba katika baadhi ya nchi zetu licha ya kupata uhuru zaidi ya miaka sitini iliyopita, bado utasikia makabila fulani au jamii fulani huchukiana na kupigana kwa kisasi cha kuzozania mipaka ya wilaya wakitafuta malisho na mito ya kunyweshea mifugo yao!

Yote haya ni matukio yanayozuka kwa kukosa utu wa kuvumiliana ili watu waishi kwa umoja, upendo na amani!

Walakini kinachokera zaidi katika nchi zetu ni migogoro na mizozo inayotokea nyakati za uchaguzi ati kwa sababu za tofauti za vyama vya kisiasa! Upuuzi mtupu.

Wakati umefika ambapo tusikubali kuzozana na kupigana tena kipindi cha uchaguzi! Tujue kwamba tunapowachagua viongozi ni kwa maslahi ya taifa zima ili waje kuwatumikia watu wote nchini! Tuvumiliane tudumishe amani mpaka siku ya kiama! Tuvumiliane!

  • Tags

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Aisee, ni kosa kusema kuwa simu imezima!

Wabunge wapya wafika bungeni kuelewa mazingira ya kazi

T L