• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Washukiwa wafurika katika siasa

Washukiwa wafurika katika siasa

Na CHARLES WASONGA

WAKENYA watawachagua tena viongozi wanaokabiliwa na kesi za ufisadi kutokana na ukosefu wa sheria inayowazima washukiwa kuwania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi mkuu.

Kufikia sasa zaidi ya wanasiasa 20 ambao wanawania viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, wanakabiliwa na kesi mbalimbali mahakamani ambapo wanatuhumiwa kuiba mabiliani za pesa za umma.

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, anayekabiliwa na kesi ya wizi jumla ya Sh7.5 bilioni kutoka serikali ya kaunti ya Nyeri na asasi nyingine za serikali kuu, kati ya 2015 na 2016 anang’ang’ania ateuliwe kuwa mgombea mwenza wa Naibu Rais William Ruto.

Akipata nafasi hiyo huenda akawa Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya endapo Dkt Ruto atashinda urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero na wabunge Ayub Savula (Lugari) na Aisha Jumwa (Malindi) wanawania ugavana katika kaunti za Homa Bay, Kakamega na Kilifi, mtawalia, ilhali hawajaondolewa lawama kesi za uporaji mamilioni ya fedha za umma zinazowakabili.

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero akiwa Shauri Yako, Homa Bay, Februari 20, 2022. PICHA | GEORGE ODIWUOR

Dkt Kidero anakabiliwa na kesi ya wizi wa Sh213 milioni alipokuwa akihudumu kama gavana wa Nairobi, Bw Savula anazongwa na kesi ya uporaji wa Sh122 milioni katika Shirika la Kusimamia Matangazo ya Biashara Serikalini (GAA) huku Bi Jumwa akikabiliwa na tuhuma za wizi wa Sh19 milioni za Hazina ya Ustawi wa Eneo Bunge lake (NG-CDF).

Wanasiasa wengine ambao ni washukiwa wa ufisadi lakini wanatetea nyadhifa zao, au wanawania viti vingine, ni pamoja na Mithika Linturi (Meru), James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Alfred Keter (Nandi Hills), Stanley Muthama (Lamu Magharibi) na mwaniaji wa useneta Nakuru Bi Tabitha Karanja miongoni mwa wengine.

Wabunge William Kamket (Tiaty) na Johanna Ng’eno (Emurua Dikirr) ni miongoni mwa wale wanaokabiliwa na kesi za uchochezi wa chuki kinyume cha hitaji la Sura ya Sita ya Katiba.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inasema kuwa haiwezi kuwazuia wanasiasa wanaokabiliwa na kesi za ufisadi kuwania viti baada ya wao kuidhinishwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kwa misingi ya ukosefu wa sheria maalum ya kuiwezesha kuchukua hatua hiyo.

Akiongea katika mkutano wa wadau katika sekta ya uanahabari katika mkahawa mmoja kaunti ya Kwale mwishoni mwa mwaka jana, mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alisema vipengele cha 99 (3) na 193 (3) vya Katiba vinazuia tume hiyo kuwazuia wawaniaji wenye kesi za ufisadi au uhalifu kuwania viti uchaguzini.

“Mtu hawezi kuzuiwa kushiriki uchaguzini kabla ya rufaa zote kuhusu kesi zinazomkabili kusikizwa na kuamualiwa,” kulingana na ibara ya tatu ya kipengele cha 99 cha Katiba.

Naye Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Twalib Mbarak aliambia mkutano huo kwamba ukosefu wa sheria mahsusi wa kuzuia wanasiasa washukiwa wa uhalifu kuwania viti ndio sababu kuu ambayo imechangia tume hiyo kutoidhinisha wanasiasa wenye kesi.

“Ni kutokana na ukosefu wa sheria inayozima kabisa washukiwa wa uhalifu kuwania viti ndio umetufanya tusikose kuwaidhinisha wanasiasa wengi kesi mbalimbali kushiriki uchaguzi. Katiba nayo inatoa nafasi kwa watu kama hao kuwania hata kabla ya kukamilika kwa kesi za ufisadi au uhalifu zinazowakabili,” akasema Bw Mbarak.

Afisa huyo alitoa mfano wa Mbunge wa Bonchari Pavel Oimeke ambaye mwaka 2021 aliruhusiwa kuwania na akashinda licha ya kukabiliwa na kesi ambapo ameshtakiwa kuitisha hongo ya Sh200 milioni kutoka kwa mfanyabiashara mmoja alipokuwa akihudumu kama Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA).

Jumla ya wawaniaji 106 ambao walikuwa na kesi mbalimbali mahakamani waliidhinishwa kuwania viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa 2017, kulingana na EACC.

Jaribio la Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi kuwasilisha bungeni mswada wa kuwazuia wanasiasa na maafisa wa serikali wenye kesi za ufisadi kuwania nyadhifa katika uchaguzi mkuu liligonga mwamba mwaka 2021 kutokana na upinzani mkali kutoka kwa wenzake.

“Licha ya mswada wangu kupigwa vita kiasi kwamba sijaweza kupewa nafasi ya kuuwasilisha rasmi bungeni, sitachoka. Nitauwasilisha hata katika bunge la 13,” Bw Wandayi akaambia Taifa Leo alipoulizwa kuhusu hatima ya mswada wake.

Mbunge huyo ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) alilenga kuifanyia marekebisho Sheria ya Maadili na Uongozi Bora ya 2012 na Sheria ya Uchaguzi ya 2011, ili kuzuia washukiwa wa ufisadi kuwania nyadhifa uchaguzini hata kabla ya kesi zao kuamuliwa.

You can share this post!

Watu walio na kesi wajibwaga siasani

Raila ajitahidi kudhibiti kaunti telezi ya Pwani

T L