• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Wandani wa Kalonzo wampa presha Raila kuhusu 2027

Wandani wa Kalonzo wampa presha Raila kuhusu 2027

Hili linajiri huku Bw Odinga akisisitiza kuwa hang’atuki katika siasa, hilo likiwa ishara kuwa huenda akawa na msimamo tofauti na msukumo wao.

“Sitashawishika na rai za yeyote anayeniambia kustaafu. Kuna watu wanaonitaka kurejea Bondo. Kile hawafahamu ni kuwa ninaifahamu vizuri barabara ya kuelekea Bondo kuwaliko,” akasema Bw Odinga, alipohutubu katika eneo la Oyugis, Kaunti ya Homa Bay wiki iliyopita.

Shinikizo hizo za kumtaka kumwidhinisha Bw Musyoka, hata hivyo, zimetajwa kama zisizofaa na vyama vikubwa katika muungano huo, huku baadhi ya wanachama wa Wiper wakieleza kutoridhishwa kwao na shinikizo hizo.

Mwenyekiti wa chama hicho, Bw Chirau Ali Mwakwere ametishia kujiuzulu ikiwa viongozi wakuu wa chama hicho watashinikiza msukumo huo.

Washirika wa Bw Musyoka wanasisitiza ni muhimu kuwa na mgombea urais wa 2027 mapema iwezekanavyo kama vile Rais William Ruto alivyofanya ili kumwezesha kubuni ushindani wa kutosha dhidi ya wawaniaji wake.Wanasisitiza kuwa lazima mgombea huyo awe ni Bw Musyoka.

“Hatushinikizi matakwa yetu na rai zetu hazilengi kuzua mafarakano katika muungano huo. Lengo lake ni kubuni utathmini mtulivu kuhusu kule tumetoka na kule tunakoelekea. Hatulengi kuleta majibizano yasiyofaa katika muungano huu,” akasema Seneta Enoch Wambua wa Kitui kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Kauli yake iliungwa mkono na Seneta Dan Maanzo wa Makueni, aliyesema ni vizuri muungano huo kumteua mwaniaji urais mpya, ikiwezekana awe Bw Musyoka, kukabiliana na Rais Ruto kwenye uchaguzi wa 2027.

“Ninaunga mkono pendekezo kuwa Raila anafaa kutangaza msimamo wake kuhusu yule atakayekuwa mgombea urais wa Azimio katika uchaguzi wa 2027. Sababu ni kuwa huwezi kufanya jambo kwa njia ile ile na kutarajia matokeo tofauti,” akasema Bw Maanzo.

Hata hivyo, Seneta Edwin Sifuna wa Nairobi alitaja shinikizo hizo kama zisizofaa.

“Tumemaliza uchaguzi juzi. Miezi sita hata haijaisha. Sidhani tunafaa kuzungumzia siasa za 2027,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya waukaribisha Mwaka Mpya kwa shangwe

Ukusanyaji kodi sasa waongezeka maradufu kaunti

T L