• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
WANDERI KAMAU: Waliopigania ukombozi wasipuuzwe

WANDERI KAMAU: Waliopigania ukombozi wasipuuzwe

Na WANDERI KAMAU

MAJUZI, nimemaliza kusoma vitabu viwili—Detained: A Writer’s Prison Diary chake Ngugi wa Thiong’o na I Refuse to Die chake mwanasiasa Koigi wa Wamwere.

Ni vitabu vilivyonipa kumbukumbu chungu kuhusu machungu ambayo wapiganiaji wa ukombozi wa kisiasa walipitia nchini katika tawala wa marais Jomo Kenyatta na marehemu Daniel Moi.

Katika tawasifu yake, Ngugi anarejelea kwa kina masaibu yake akiwa mhadhiri wa Fasihi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Anaeleza jinsi alivyokamatwa na polisi kwa tuhuma za kuwachochea wananchi na wanafunzi kupitia kitabu chake ‘Ngaahika Ndeenda’ (Nitaoa Nikipenda), kilichoangazia jinsi tawala dhalimu zilivyopanga njama kuwahangaisha wananchi kwa kuwanyang’anya mali zao kwa njia za kilaghai.

Baada ya tuhuma hizo, alikamatwa na kufungwa katika Gereza Kuu la Kamiti mnamo 1978 bila kufunguliwa mashtaka yoyote.

Kwa upande wake, Koigi anaeleza kwa kina mahangaiko aliyopitia pamoja na wafungwa wengine wa kisiasa kama Wasonga Sijeyo, Martin Shikuku, Ngugi, Wanyiri Kihoro kati ya wengi katika Jumba la Mateso la Nyayo, Nairobi.Kwa wakati mmoja, anaeleza jinsi wafungwa ‘waasi’ walivyotishwa kwa kurushiwa siafu wakali ama nyoka mkubwa aliyekuwa amefugwa katika jumba hilo.

Bila shaka, simulizi za wanaharakati hao wawili zinaashiria safari ndefu na pevu ambayo Kenya imepitia katika harakati za kutafuta Katiba inayowafaa wananchi wote, bila kuwabagua hata kidogo.

Katika nchi iliyopitia safari chungu kama hiyo, inasikitisha kuwaona wanasiasa wakiichezea Katiba kwa lengo la kujifaidi wao wenyewe.

Ni kosa kubwa kwa wanasiasa kuiteka Katiba na kutishia kuifanyia mageuzi machoni mwa watu ambao walipoteza jamaa zao na nafasi muhimu maishani wakipigania ukombozi wa kisiasa wa taifa hili.

Bw Wamwere ni miongoni mwa wanaharakati waliofungwa gerezani kwa muda mrefu zaidi wakipigania Ukombozi wa Pili.

Kitakwimu, anadaiwa kufungwa jumla ya miaka 13 na tawala za marais Kenyatta na Moi kwa kuwa mwanasiasa “msumbufu.”

Watu wengine ambao wamejitoa kafara kupigania ukombozi wa kisiasa nchini ni kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Seneta James Orengo (Siaya), Gavana Anyang’ Nyong’o (Kisumu), Gavana Kiraitu Murungi (Meru), mawakili Paul Muite, Gibson Kamau Kuria, Dkt John Khaminwa, Gitobu Imanyara kati ya wengine wengi.

Bw Odinga amefungwa gerezani jumla ya miaka tisa kutokana na harakati zake za kisiasa. Kwenye tawasifu zake ‘Raila Odinga: An Enigma in Kenyan Politics’ na ‘The Flame of Freedom’, Raila anaeleza kuwa mamake alifariki na kuzikwa akiwa bado gerezani.

Hakufahamishwa alipofariki wala hakuhudhuria mazishi yake.Bila shaka hayo ni baadhi ya mahangaiko ambayo wanaharakati hao walipitia chini ya tawala dhalimu za Mzee Kenyatta na marehemu Moi.

Hata hivyo, inasitikisha kuwa wanasiasa kama Raila wanaonekana kuunga mkono juhudi hizo!Je, wamesahau masaibu waliyopitia kwenye harakati za kupigania ukombozi?K

wa Rais Uhuru Kenyatta na wale wanaoendesha mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI), wakati umefika wasikilize kauli na sauti za watu waliojitolea kuhatarisha maisha yao kupigania uhuru wa kisiasa.

Kuwatenga ni sawa na kutafuta laana zao kwa machungu waliyopitia.

[email protected]

You can share this post!

Makala ya spoti- Pema Ladies FC

Desturi ya aina yake kisiwani Lamu inayozipatia mashua...