• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:50 AM
Wawaniaji huru kuteua mmoja wao kuwawakilisha katika Uchaguzi Mkuu

Wawaniaji huru kuteua mmoja wao kuwawakilisha katika Uchaguzi Mkuu

NA JURGEN NAMBEKA

WAGOMBEAJI huru 12 wa Urais Alhamisi walieleza kuwa watamteua mmoja wao, kupeperusha bendera ya wagombeaji huru katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Wagombeaji hao, Rueben Kigame, Waweru Mbugua,Warunga Esther, Njenga Kinyanjui, Paul Muriungi, James Irungu, Dkt Joseph Karani, George Munyotta, Stephen Owoko, Duncan Otieno, James Kamau na Kariuki King’ori walieleza kuwa hatua hii itaboresha nafasi zao za kuteuliwa.

Walieleza kuwa kuteuliwa kwa mwaniaji mmoja kuwawakilisha kwenye uchaguzi wa Agosti 9, 2022, kutarahisisha mchakato mzima wa uchaguzi.

Akizungumza katika kongamano la wawaniaji huru lililofanyika jijini Nairobi, Mwenyekiti wa wawaniaji huru Bw Stephen Owoko ambaye pia anawania urais, alieleza kuwa ni wakati wa kuonyesha uwezo wao wakiungana.

“Kila mmoja akiamua ataenda kwenye uchaguzi pekee yake hatutafaulu. Ni vyema tumuunge mkono mmoja wetu na tumpe kila anachohitaji ili awe rais,” alieleza Bw Owoko.

Mwanamuziki wa nyimbo za Injili na mwaniaji huru wa urais Bw Reuben Kigame, aliwaomba wawaniaji kujadiliana na kutafita njia itakayowawezesha kutwaa ushindi.

“Hakuna lisilowezekana. Mungu akiwa upande wetu mwishoni tutakuwa na rais ambaye ni mwaniaji huru,” alisema Bw Kigame.

Viongozi hao walieleza kuwa kuungana kwao kutarahisihsa shughuli za uchaguzi ikiwemo ukusanyaji wa saini zinazodaiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

IEBC inahitaji angalau saini 2000 kwa kila kaunti kama moja wapo ya mahitaji ya kuwania urais.

Kuungana kwao pia kutawasaidia kukusanya saini zinazohitajika na IEBC na pia kufadhili kampeni zao.

Mwaniaji wa urais Balozi Esther Waringa aliwaomba wawaniaji huru kutoa pesa walizopanga kutumia kwenye kampeni, kuwafadhili wawaniaji walio na nafasi nzuri zaidi ya kuteuliwa.

“Niko tayari kuacha azma yangu, iwapo tutamteua mmoja wetu atuwakilishe,” alisema Bi Waringa.

Waliwaomba wawaniaji wa viti vya Useneta, Ugavana, MCA, Ubunge kufuata mfumo huo.

Kulingana nao hakuna haja ya wagombeaji huru wengi, kwani wangewachanganya wapiga kura ambao huenda, wasiwapigie kura wanaopeperusha bendera za vyama tajika.

“Itakuwa vyema iwapo wanaotafuta viti vya MCA katika wodi moja ni watatu, wazungumze na kumchagua mmoja,” alieleza Bw James Kamau Irungu mwaniaji wa urais.

Bw Owoko alieleza kuwa wanapanga kupatana Jumatatu kujadili watakayempendekeza, kabla ya tarehe ya IEBC kuchapisha majina kwenye gazeti haijawadia.

Hatua hii huenda ikapunguza idadi ya wagombeaji wa urais ambayo kwa sasa ni 46. Idadi hii ni ya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini.

  • Tags

You can share this post!

Sonko, Nassir kukutana ana kwa ana hafla ya Azimio Tononoka

WANDERI KAMAU: Mrithi wa Uhuru aendeleze uhuru wa kujieleza...

T L