• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Wawaniaji huru watia Ruto, Raila tumbojoto

Wawaniaji huru watia Ruto, Raila tumbojoto

NA ONYANGO K’ONYANGO

NAIBU Rais William Ruto na mgombea urais kwa tikiti ya Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga sasa wamelazimika kupanga mikakati mipya kukabiliana na idadi kubwa ya wawaniaji huru kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Jumla ya wawaniaji 7,212 huru tayari wameidhinishwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Idadi hii ni ya juu zaidi ikilinganishwa na jumla ya watu 4,950 walioidhinishwa mnamo 2017.

Hata hivyo, ni wawaniaji huru 4,002 pekee walioidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Mwaka huu, jumla ya watu 106 wamekubaliwa kuwania viti vya ugavana huku 147 wakiwania viti vya useneta kama wagombeaji wa kujitegemea.

Viti vya Wabunge Wawakilishi wa Kike vimevutia wawaniaji 110 huku watu watakaopigania nyadhifa 290 za ubunge kama wagombeaji huru ni 958.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Anne Nderitu pia amewaruhusu watu wengine 5,845 kuwania jumla ya viti 1,450 vya udiwani kote nchini.

Dkt Ruto na Bw Odinga wamekuwa wakiwahimiza wandani wao walioshinda na walioshindwa katika kura za mchujo kufanyakazi pamoja kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Wawili hao huwahimiza wafuasi wao kutowapigia kura wawaniaji huru kwa sababu hawako katika kambi zao; Kenya Kwanza au Azimio la Umoja-One Kenya.

Kulingana na Profesa Masibo Lumala wa Chuo Kikuu cha Nairobi, wawaniaji huru wenye umaarufu mkubwa na ambao wanaweza kufadhili kampeni zao ndio tishio kubwa kwa mirengo mikubwa.

“Wawaniaji huru wanahisi hawakutendewa haki katika kura za mchujo za vyama vikubwa. Kwa hivyo wao sio tishio kubwa sababu itakuwa vigumu kwao kuvutia wapiga kura bila kujihusisha na vyama vya kisiasa. Hata hivyo, wale matajiri au wanaouza sera zinazovutia wapiga kura watatoa jasho miungano mikubwa,” akaongeza.

Hii ndio maana Dkt Ruto ambaye ni mgombeaji wa urais kwa tikiti ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) ameamua kukutana na wale walioshiriki mchujo wa chama hicho kuwapatanisha walioshindwa na walioshinda.

Lengo lake ni kuhakikisha walioshinda wanawaunga mkono washindi ili kwa pamoja waweze kushinda wawaniaji huru katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Aidha, Dkt Ruto anaendesha upatanisho huo kuziba mianya ambayo huenda ikawezesha wagombeaji wa mrengo wa Azimio kushinda.

“Tunashirikiana kuhakikisha kuwa tunalinda kura za urais za UDA. Aidha, tunapatanisha wawaniaji wote, walioshinda na walioshindwa, ili tushinde viti vingi vya ugavana, useneta, ubunge na udiwani. Hatutaki wapinzani wetu wa Azimio au wale wanaojiita wagombeaji huru, kutulemea,” Dkt Ruto akasema wiki jana baada ya kukutana na viongozi kutoka kaunti ya Embu katika makazi yake rasmi katika mtaa wa Karen, Nairobi.

Kwa upande mwingine, Bw Odinga amekuwa akiwahimiza wafuasi wa Azimio kutowapigia kura wawaniaji wa vyama visivyo ndani ya muungano huo au wawaniaji huru.

  • Tags

You can share this post!

Mwamerika Kerley amchongoa Omanyala kiujanja kuwa hana...

Wazazi wanaoingiza wana wao sekondari walia kukabiliwa na...

T L