• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mwamerika Kerley amchongoa Omanyala kiujanja kuwa hana medali

Mwamerika Kerley amchongoa Omanyala kiujanja kuwa hana medali

Na GEOFFREY ANENE

FRED Kerley anaonekana kumchongoa Mkenya Ferdinand Omanyala kiujanja kwa kusema kuwa medali ni muhimu katika mashindano wala si rekodi.

Bingwa huyo wa riadha za Kip Keino Classic mbio za mita 200 kutoka Amerika amewasili jijini Nairobi mnamo Jumatano kwa makala ya tatu yatakayofanyika Mei 7 ugani Kasarani. Atakabiliana na mshikilizi wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100 Omanyala pamoja na bingwa wa Olimpiki, Marcell Jacobs kutoka Italia, miongoni mwa wengine.

Kerley alipoulizwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta iwapo kuna uwezekano wa rekodi ya Mjamaica Usain Bolt ya mbio za mita 100 ya sekunde 9.58 kuvunjwa uwanjani Kasarani, alisema rekodi hazina maana kwake.

“Kitu muhimu katika riadha za uwanjani ni ushindi na medali. Unaweza kuvunja kila rekodi unataka, lakini hiyo si hoja ikiwa utasalia bila medali,” alisema Kerley anayejivunia nishani nne kutoka mashindano makubwa.

Alishinda medali ya fedha katika mbio za mita 4×100 akishirikiana na Wilbert London III, Gil Roberts na Michael Cherry katika Riadha za Dunia jijini London, Uingereza mwaka 2017 na dhahabu katika kitengo hicho kwenye Riadha za Dunia 2019 nchini Qatar akishirikiana na Cherry, London III na Rai Benjamin.

Kerley pia alizoa medali ya shaba mbio za mita 400 kwenye Riadha za Dunia 2019 na alinyakua fedha katika mbio za mita 100 kwenye Olimpiki 2020 mwaka jana nchini Japan.

Omanyala, ambaye alibanduliwa katika nusu-fainali kwenye Olimpiki jijini Tokyo, hana medali kutoka kwa mashindano makubwa.

Medali yake kubwa ni fedha ya Kip Keino Classic aliyopata akiandikisha rekodi ya Kenya na Afrika mbio za mita 100 ya sekunde 9.77 uwanjani Kasarani mnamo Septemba 2021.

Inspekta huyo wa polisi yuko katika orodha ya wanariadha 78 ambao Kenya imeingiza kwenye Riadha za Afrika zitkazofanyika Mauritius mnamo Juni 8-12. Alipojikatia tiketi ya kuelekea Mauritius wakati wa mashindano ya kitaifa mnamo Aprili 26-28, Omanyala alisema kuwa amevunja rekodi za kitaifa na Afrika, lakini sasa analenga kushinda medali yake ya kwanza katika mashindano makubwa. Mbali na mashindano ya Mauritius, Omanyala analenga kushiriki Riadha za Dunia nchini Amerika mnamo Julai 15-24 na michezo ya Jumuiya ya Madola nchini Uingereza mnamo Julai 28 hadi Agosti 8.

  • Tags

You can share this post!

DCI wachunguza kifo cha mwanawe mbunge maalum

Wawaniaji huru watia Ruto, Raila tumbojoto

T L