• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Wito watolewa Joho awe mgombea-mwenza wa Raila

Wito watolewa Joho awe mgombea-mwenza wa Raila

NA BRIAN OCHARO

VIONGOZI wa ODM katika Kaunti ya Mombasa, wamejitosa katika mjadala kuhusu utafutaji wa mgombea mwenza wa kinara wa chama hicho, Bw Raila Odinga, na kutaka wadhifa huo umwendee Gavana Hassan Joho.

Jopo lililoteuliwa na baraza la Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kuwapiga msasa waliopendekezwa kuwa wagombea wenza, linatarajiwa kuanza vikao vyake leo Jumatano jijini Nairobi.

Meya wa zamani wa Mombasa, Bw Ahmed Mudhar, ndiye alipasua mbarika jana kuhusu suala hilo alipokuwa akifungua Baraza la Idd ambalo lilihudhuriwa na vigogo wa kisiasa wa kaunti hiyo.

Viongozi hao walisema kuwa eneo la Pwani lina idadi kubwa ya wapigakura na hivyo basi linastahili kuzingatiwa kwa nafasi ya Naibu Rais katika uchaguzi wa Agosti.

“Bw Joho ni maarufu na ana mvuto wa kitaifa. Anapendwa na watu wengi kote nchini. Anafaa kuwa mgombeamwenza wa Bw Odinga,” akasema Bw Mudhar.

Alisema itakuwa rahisi kwa Bw Joho kuchukua nafasi ya Bw Odinga kuwania urais katika uchaguzi wa 2027 ikiwa atakuwa mgombeamwenza wake katika uchaguzi wa Agosti.

Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, alisema ana imani kuwa Bw Joho atakuwa katika serikali ijayo.

Mbunge huyo alisema kuwa uongozi wa ODM una nia ya kufufua uchumi wa eneo hilo kwa kurejesha huduma muhimu za bandari, ambazo alisema zimeathiriwa na ubinafsishaji wa kituo hicho.

Alisema yeye alikuwa mtu wa kwanza kupendekeza Bw Joho kuwania kiti cha juu zaidi nchini akibaini kuwa bado anaamini kuwa gavana huyo wa Mombasa ana uwezo huo.

“Usiwaangushe watu wa Mombasa kwa kukataa wadhifa wa naibu rais,” alisema mbunge huyo wa Mvita.

Seneta Mohamed Faki alimwambia Bw Joho kwamba wapigakura wa Mombasa wako nyuma yake anapoelekeza siasa zake katika serikali ya kitaifa.

Kwa upande mwingine, mfanyabiashara Suleiman Shahbal, alisema uamuzi wake kumwachia Bw Nassir nafasi ya kuwania ugavana haukutokana na ahadi yoyote ya kazi serikalini.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi imani za majini migodini zinavyoleta ufukara Taita

CECIL ODONGO: Kalonzo akatae mashauriano ya kusaka mwaniaji...

T L