• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 4:32 PM
CECIL ODONGO: Kalonzo akatae mashauriano ya kusaka mwaniaji mwenza

CECIL ODONGO: Kalonzo akatae mashauriano ya kusaka mwaniaji mwenza

KINARA wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka anafaa akatae kushiriki mahojiano ya kusaka mwaniaji mwenza wa Bw Raila Odinga ndani ya Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya kwa kuwa mchakato huo unamdhalilisha na kumdunisha kisiasa.

Kamati iliyoteuliwa baada ya mkutano wa vyama tanzu ndani ya muungano huo ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta majuma mawili yaliyopita, inatarajiwa kuanza leo kuwahoji wale wanaoonekana kuwa na uzani wa kisiasa na wanatosha kuwa wagombeaji wenza wa Bw Odinga.

Mahojiano hayo yanatarajiwa kukamilika Mei 10 ambapo kamati hiyo itaibuka na mwaniaji mmoja wa kupokezwa nafasi hiyo.

Mbali na Bw Musyoka, wale ambao waliorodheshwa na kamati hiyo inayoongowa na Elizabeth Meyo ni kinara wa Narc Kenya, Martha Karua, mbunge wa zamani wa Gatanga Peter Kenneth, Waziri wa Kilimo Peter Munya, Magavana Hassan Joho (Mombasa) na Lee Kinyanjui (Nakuru), Mwakilishi wa Kike wa Murang’a Sabina Chege na mbunge wa Kieni Kanini Kega.

Mwanzo, kati ya wanasiasa hawa wote, ni wazi kuwa hakuna yule ambaye yuko kwenye ‘ligi’ ya Bw Musyoka kisiasa.

Mbali na kuhudumu kama makamu wa rais ndani ya serikali ya muungano kati ya 2008-2013 , Bw Musyoka alitumikia taifa kama waziri enzi za hayati Mzee Daniel Moi na Mwai Kibaki.

Vilevile alihudumu kama Mbunge wa Mwingi Kaskazini kati ya 1983-2013.

Je, uzoefu huu wote wa miaka mingi bado Azimio wanamhitaji Bw Musyoka kufika mbele ya jopo linalowahoji watu ambao hawamfikii kivyovyote katika uongozi na kisiasa?

Je, utamweka vipi Bw Musyoka katika kikoa kimoja na wanasiasa kama Bi Chege na Kanini Kega kisha kuwahoji kwa wadhifa wa mwaniaji mwenza?

Aidha, kihesabu Bw Musyoka anamletea mezani Bw Odinga zaidi ya kura milioni 1.8, idadi ya juu zaidi ikilinganishwa na wengine ambao wameorodheshwa kwa nafasi ya mgombeaji mwenza.

Ingawa kuna mjadala kuwa mgombeaji mwenza wa Bw Odinga anafaa atoke Mlima Kenya ili kulemaza umaarufu wa Dkt Ruto Mlimani, kuna uwezekano waziri huyo mkuu wa zamani bado atabwagwa eneo hilo hata kama Bi Karua au Mabw Kenneth na Kinyanjui watapokezwa wadhifa huo.

Kulingana na itifaki, Bw Musyoka ndiye wa tatu baada ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kwenye ngazi ya uongozi ndani ya Azimio la Umoja.

Aidha, Bw Musyoka amekuwa nambari mbili au mwaniaji mwenza kwa Bw Odinga chini ya CORD 2013 na NASA 2017.

Je, mbona wakati huo hakufanyiwa mahojiano hayo ilhali alimsaidia kuzoa kura nyingi licha ya kushindwa pembamba na Rais Kenyatta katika chaguzi hizo?

Huenda hujuma dhidi ya Bw Musyoka ndani ya muungano huo ndiyo imesababisha awe akitoa kauli tatanishi na masharti makali kwa waziri huyo mkuu wa zamani.

Tangu mwanzo ilikuwa bayana kuwa Bw Musyoka alikuwa akilenga kuwania Urais kwa tikiti ya OKA na hata kauli ambazo alikuwa akitoa baada ya kujiunga na Azimio ziliashiria kuwa huenda alilazimishwa kumuunga Bw Odinga.

Hata hivyo, hilo halimaanishi kuwa hawezi kuunga mkono mrengo wa Kenya Kwanza.

Sheria inaweza kumfunga ndani ya Azimio la Umoja lakini akiamua kuelekea mrengo wa Dkt Ruto basi ni Bw Odinga ambaye atapoteza pakubwa kisiasa.

Isitoshe magavana watatu kutoka Ukambani Charity Ngilu (Kitui), Profesa Kivutha Kibwana (Makueni) na Dkt Alfred Mutua wa Machakos wameonekana kutochangamkia uwepo wa Bw Musyoka ndani ya Azimio la Umoja.

Kutokana na mchango mkubwa anaouleta ndani ya muungano huo, Bw Musyoka anastahili kupokezwa wadhifa wa mgombeaji mwenza wa Bw Odinga bila masharti yoyote.

Hoja kuwa atatengewa wadhifa wa waziri mwenye mamlaka makubwa katika serikali ijayo haina mashiko kwa sababu mikataba mingi ya kisiasa huwa haizingatiwi na haiheshimiwi baada ya uchaguzi kuandaliwa.

Viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya wanafaa wawe wameungana na kuvumisha Bw Odinga badala ya vita hivi vya ndani kwa ndani ambavyo vitaponza nafasi yao ya kushinda urais.

  • Tags

You can share this post!

Wito watolewa Joho awe mgombea-mwenza wa Raila

TAARIFA ZA WIKI: Serikali yasisitiza kunayo chanjo ya...

T L