• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
Ziara za Uhuru kubomoa Ruto

Ziara za Uhuru kubomoa Ruto

WANDERI KAMAU Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta anatarajiwa kutumia ziara zake za kuzindua miradi ya maendeleo sehemu mbalimbali nchini wiki hii kumwanika na kufifisha umaarufu wa naibu wake Dkt William Ruto ambaye amekuwa akimshambulia vikali kwa kumuunga mkono mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga.

Ziara hizo za wiki yake ya mwisho uongozini, zinatajwa kuwa sehemu ya mikakati yake ya kumpigia debe Bw Odinga na kumbomoa kisiasa Dkt Ruto.

Kulingana na wadadisi wa siasa, hatua hiyo pia ni mkakati wa kumkabili Dkt Ruto na washirika wake, ambao wamekuwa wakimlaumu Rais Kenyatta kwa matatizo ya kiuchumi yanayoikabili nchi hii.

Dkt Ruto amekuwa akiongoza washirika wake kudai kwamba ukuruba wa kisiasa wa Rais Kenyatta na Bw Odinga ulilemaza ajenda ya maendeleo ya serikali ya Jubilee.

“Lakini sasa, shughuli za afisi ya Rais zikiendelea kupungua na uchaguzi unapokaribia, Rais Kenyatta anaendelea kuzindua miradi ya maendeleo katika maeneo tofauti kuthibitisha kuwa Dkt Ruto na washirika wake wamekuwa wakidanganya Wakenya,” asema mchambuzi wa siasa, Dkt Isaac Gichuki.

Anasema Rais Uhuru Kenyatta anaonekana kutumia siku saba zilizosalia kabla ya uchaguzi mkuu ujao, ‘kujitakasa’ dhidi ya madai hasi ya Dkt Ruto.Hapo jana, Rais Kenyatta alizindua rasmi barabara ya Nairobi Expressway, jijini Nairobi, ambapo alitumia nafasi hiyo kupuuza madai ya Dkt Ruto kwamba Rais anapanga kumdhuru.

Dkt Ruto alitoa madai hayo Ijumaa, alipowahutubia wafuasi wake mjini Kapsabet, katika Kaunti ya Nandi.

“Ninataka kumwambia Rais, acha kunisumbua. Mfanyie kampeni Bw Odinga, acha kunitaja kwenye hotuba zako. Acha kuzungumza kunihusu. Achana nami. Nilikuunga mkono wakati ulihitaji mtu wa kukuunga mkono. Ikiwa hutaki kuniunga mkono, niache. Kuwa na shukrani. Sisi ndio tuliokusaidia. Sasa umeanza kunitishia. Bora tu usiwadhuru watoto wangu. Tuheshimiane kati yetu,” akasema Dkt Ruto huku akishangiliwa na wafuasi wake.

Lakini jana Jumapili, Rais Kenyatta alisema kuwa hana mpango wowote wa kumdhuru mtu yeyote, kama inavyodaiwa na Dkt Ruto na washirika wake.

Alisema amevumilia matusi kutoka kwa Dkt Ruto na washirika wake, kwa miaka minne na hajamhangaisha yeyote licha ya kuwa na mamlaka ya kufanya hivyo.

“Umenitukana kwa zaidi ya miaka mitatu, kuna yeyote amekudhuru? Je, kwa muda huo niliokuwa uongozini, sikuwa na uwezo wa kufanya hivyo? Kwa sasa ambapo najitayarisha kukabidhi serikali kwa utawala mpya, unadhani nina muda wa kukutafuta, ikizingatiwa pia nina mamlaka?” akasema Rais Kenyatta.

Akaongeza: “Kila mtu, nikiwa mmoja wao, ana uhuru wa kumfanyia kampeni yeyote anayemtaka. Hakuna haja sisi kutusiana. Ninakujibu haya kwa sababu umekuwa ukiwadanganya raia. Hakuna haja kuwaambia watu eti ninataka kukuua.”

Kando na Dkt Ruto, washirika wa karibu kama mgombea-mwenza wake, Rigathi Gachagua, wabunge Moses Kuria (Gatundu Kusini), Ndindi Nyoro (Kiharu) na Kimani Ichung’wa (Kikuyu) wamekuwa wakidai uwepo wa njama za serikali kuwadhuru.

Wiki hii, Rais Kenyatta anatarajiwa kuzuru Kaunti ya Vihiga (eneo Magharibi), maeneo ya Nyanza, Pwani na ngome yake ya Mlima Kenya, ambako anatarajiwa kuzindua miradi ya maendeleo.

“Itakuwa wiki ya kuanika uongo ambao Dkt Ruto amekuwa akiambia Wakenya. Ndipo kitaeleweka kwa kuwa amekuwa akieneza propaganda akidai miradi ya maendeleo na ajenda za Jubilee zilisambaratishwa na Bw Odinga,” akasema Bw Joseph Chomba mtaalamu na mwanamikakati wa siasa za uchaguzi.

Miradi pia inatarajiwa kutumiwa kuwarai Wakenya kumuunga mkono Bw Odinga katika azma yake ya kuwa rais kupitia uchaguzi ujao wa Agosti 9, hasa katika maeneo ya Nyanza na Pwani.

Kwa muda wa wiki mbili zilizopita, Rais Kenyatta amezuru kaunti za Samburu, Laikipia na Nakuru, ambako amezindua miradi kadhaa ya maendeleo.Vilevile, amekuwa akiwarai wenyeji “kujiepusha na uwongo ambao umekuwa ukienezwa na Dkt Ruto na washirika wake”.

Hapo jana Jumapili, Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee, David Murathe, alisema kuwa ‘hasira’ za Dkt Ruto zinaonyesha kuwa mikakati ya Rais Kenyatta imeanza kupunguza umaarufu wake.

“Alikasirika kwa sababu kuna wawaniaji wengi huru katika Bonde la Ufa ambao hawamuungi mkono,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Otieno ana sifa zote za mwalimu bora

Wagombeaji ugavana wakaidi wito wa Raila

T L