• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Wagombeaji ugavana wakaidi wito wa Raila

Wagombeaji ugavana wakaidi wito wa Raila

NA ALEX NJERU

WAGOMBEAJI watatu wa ugavana chini ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Kaunti ya Tharaka Nithi wamekaidi wito wa mgombea urais wa muungano huo Raila Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua, kuunga mmoja wao kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Profesa Erastus Njoka (Jubilee), Dkt Mzalendo Kibunjia (Narc Kenya) na Naibu Gavana wa Tharaka Nithi Nyamu Kagwima (Wiper), wanamenyania kiti hicho kinachoshikiliwa kwa wakati huu na Gavana Muthomi Njuki, ambaye anakitetea kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Watatu hao ambao wamekuwa wakizozana, wamesisitiza kuwa ni wapigakura watakaoamua atakayekuwa gavana wa kaunti hiyo.

Wakizungumza wakiwa Marimanti, kaunti ndogo ya Tharaka wiki mbili zilizopita, Bw Odinga na Bi Karua waliwapa wagombeaji hao wiki moja kukubaliana atakayesalia kuperusha bendera ya kiti cha ugavana katika kaunti hiyo.

Bw Odinga alisema alikuwa amezungumza na watatu hao faraghani na kuwahimiza wakubaliane kuunga mmoja wao ili muungano huo uweze kushinda kiti hicho.

“Nimezungumza na wagombeaji hao watatu chini ya muungano wa Azimio na tukakubaliana kuwa katika muda wa wiki moja, watakuwa wamekubaliana mtu mmoja wa kupeperusha bendera ya muungano wetu,” Bw Odinga alisema.

Hata hivyo, hakuna anayeonekana kuwa tayari kuachia mwenzake.Akizungumza akiwa Tunyai, eneobunge la Tharaka wiki jana, Dkt Kibunjia alisema kwamba, hayuko tayari kwa mazungumzo isipokuwa Prof Njoka na Bw Kagwima wawe tayari kumuunga mkono.

Alisema kwamba mbali na kauli ya kisiasa ambayo Bw Odinga alitoa akiwa mjini Marimanti, chama chake hakijatoa mawasiliano rasmi kuhusiana na suala hilo.“Chama changu hakijaniambia nishiriki katika mazungumzo ya aina hiyo na ni pale wapinzani wangu watakuwa tayari kuniunga mkono ambapo nitaweza kushiriki,” akasema Dkt Kibunjia.

Aliongeza kuwa wafuasi wake wanasema anafaa kuwa debeni na ni wakati wa eneobunge la Tharaka kutoa gavana.Alisema kwmba gavana wa kwanza wa kaunti hiyo, Bw Samuel Ragwa, alitoka eneobunge la Maara naye Bw Njuki anatoka eneobunge la Chuka/Igambang’ombe na kwa moyo wa usawa, gavana anayekuja anafaa kutoka eneobunge la Tharaka.

Bw Kagwima aliambia Taifa Leo kwamba mbali na kauli ya Bw Odinga na Karua wakiwa Marimanti, hakuna chochote kilichofanyika kuhusiana na suala hilo.

Alisema kwamba muungano wa Azimio haujajitolea kufanikisha mazungumzo hayo kwa sababu unaunga Prof Njoka.

“Hilo lilikuwa tamko la kupita kwa kuwa katika maeneo mengine ambako Azimio inataka mazungumzo, uongozi wa vyama umekuwa ukihusika,” alisema Bw Kagwima anayetoka eneobunge la Tharaka.

Watatu hao wakiwa kwenye debe, kuna uwezekano wa kushindwa na Bw Njuki.

Wengine wanaogombea kiti hicho ni Bw Gitari Mbiuki wa Chama cha Kazi kutoka Chuka/Igambang’ombe na Kaugi Mboya, mgombeaji huru kutoka eneobunge la Maara.

  • Tags

You can share this post!

Ziara za Uhuru kubomoa Ruto

Raila kuzuru Nyanza kura zikinukia

T L