• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Jijenge Fund ni mpango mpya wa mkopo unaolenga kunufaisha wakazi wa Kiambu

Jijenge Fund ni mpango mpya wa mkopo unaolenga kunufaisha wakazi wa Kiambu

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Kaunti ya Kiambu, watanufaika kutokana na mpango wa mkopo wa Jijenge Fund ambao umezinduliwa Jumanne.

Gavana Ferdinand Waititu, amezindua mpango huo huku akiwahakikishia wakazi wa Kiambu kuwa kila mmoja ana haki ya kupokea mkopo huo.

“Wakati wa kupeana mkopo huo hakuna ubaguzi utakaoendeshwa bali kila mmoja atapata haki yake. Tunataka kuona kila mwananchi akinufaika kwa kupata mkopo,” alisema Bw Waititu.

Alisema serikali yake imetenga takribani Sh200 milioni zitakazotumika kuinua maisha ya wananchi kwa kuwapa mikopo.

“Kitu cha muhimu ni kwamba iwapo unapokea mkopo ni sharti ulipwe unavyostahili ili nao wengine pia wapewe. Hakuna riba itatozwa kwa yeyote atakayepokea mkopo huo,” amesema Gavana.

Amesema kati ya ajenda nne kuu za serikali watazingatia kilimo, na ajira kwa vijana.

Amesema wakati huu hakuna haja ya kupiga Siasa, bali kutekeleza miradi ya maendeleo ili ifikapo mwaka wa 2022 atawaeleza wananchi ni kazi ipi aliyowatendea wananchi.

Amesema kwa wakati huu wakazi wa Kiambu wanahitaji soko la kuuzia vyakula na bidhaa nyinginezo.

Baadhi ya maeneo ambayo yanaendelea kujengwa ni Kikuyu, Limuru, Juja, Ruiru, na Kimende.

Amesema mradi huo wa kujenga masoko katika kila eneo utasaidia wakazi kuuza bidhaa zao bila matatizo.

Ameeleza ya kwamba wanapanga kupanda miche ya miti 1 milioni na shughuli hiyo itaendeshwa na vijana walioasi uraibu wa kunywa pombe katika mpango unaojulikana kama ‘Kaa Sober’.

Waziri wa mchezo na vijana, Bw Karungo wa Thang’wa, amesema mikopo itatolewa kwa mtu binafsi na hata kwa vikundi.

“Tunataka kuona wananchi wanajiendeleza kibiashara na hiyo ndiyo itafanya kuwe na maendeleo,” amesema Bw Thang’ua.

Alisema wanawakaribisha watu wenye maoni ambao wataweza kuipa mawaidha Kaunti ya Kiambu.

“Iwapo kuna mtu yeyote aliye na ujuzi huo tunamkaribisha aje ili tujadiliane ili tuendeshe Kiambu Mbele,” alisema Bw Thang’wa.

Mwongozo

Ameeleza kwamba kibali  cha kuendesha biashara kitatolewa kwa uwazi bila kubagua yeyote kwa kusisitiza vijana wanastahili kupewa mwongozo jinsi ya kupata stakabadhi aina ya permit ili kuendesha biashara yao.

Alisema tayari Kaunti ya Kiambu imezindua kombe linalotambulika kama Kiambu Super Cup litakalowaniwa na klabu za soka mbalimbali kutoka wadi zote za Kaunti hiyo.

“Tunataka kuona vijana wakiwa na jambo la kufanya na mchezo ni mojawapo ya mpango huo,” alisema Bw Thang’ wa.

You can share this post!

ULIMBWENDE: Jinsi ya kufanya ili ngozi yako iwe laini na ya...

President F1: Aina ya nyanya inayostawi maeneo yote nchini...

adminleo