Kituyi akemea Uhuru, amtaja kama dikteta

Na Brian Ojamaa

WAZIRI wa zamani na mwaniaji wa urais hapo mwakani, Dkt Mukhisa Kituyi amekashifu utawala wa Rais Uhuru Kenyatta kwa kuwakandamiza wapinzani ambao wanalenga kuwania nyadhifa mbalimbali za uongozi.

Dkt Kituyi wikendi alisema kuwa wanasiasa wanaoonekana kuwa na mtazamo kinzani kuhusu masuala mbalimbali ya uongozi wamekuwa wakinyanyaswa huku serikali ikiwalazimishia raia baadhi ya viongozi.

Akihutubu wakati wa mazishi ya Mzee Charles Wekesa Maruti katika wadi ya Maraka, Webuye Mashariki, Dkt Kituyi alidai kuwa serikali imekuwa ikiwatumia maafisa wa usalama kuwatishia wapinzani wake.

“Wale ambao hawaiungi mkono serikali wamekuwa wakitishiwa kuwa watashtakiwa kortini kutokana na makosa mbalimbali. “Kenya ni nchi yenye demokrasia na kila mmoja ana uhuru wa kuamua mkondo wa kisiasa anaoutaka,” akasema.

Akigusia suala la ufisadi, Katibu huyo wa zamani wa Shirika la Kimataifa la UNACTAD, alisema tofauti za kisiasa hazifai kutumika kuwasawiri baadhi ya viongozi kama wafisadi.

“Ni kinaya kuwa Rais alikuwa ameilamu mahakama kwa kujikokota kukabiliana na kesi za ufisadi ilhali baadhi ya watu wanalazimishwa wabadilishe misimamo yao ya kisiasa,” akaongeza.

Alitoa wito kwa wanasiasa wote waendeleze kampeni ya amani na wajizuie kuwagonganisha Wakenya.

Kituyi apuuzilia mbali mkutano wa Raila na OKA

Na BRIAN OJAMAA

WAZIRI wa zamani Dkt Mukhisa Kituyi amepuuzilia mbali mkutano wa hivi karibuni baina ya Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa ODM Raila Odinga na viongozi wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

Dkt Kituyi alitaja mkutano huo kama wa kupigania maslahi ya kibinafsi wala ‘hauna manufaa kwa Wakenya’.

Rais Kenyatta, Jumanne iliyopita alikutana na Bw Odinga na viongozi wa OKA; Gideon Moi (Kanu), Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford-K) katika Ikulu ya Mombasa.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na msemaji wa Ikulu, Kanze Dena, ilisema kuwa viongozi hao walijadili kuhusu janga la corona, utangamano wa kitaifa na maendeleo.Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya pia alihudhuria mkutano huo.

Dkt Kituyi aliyekuwa akizungumza Jumamosi katika kijiji cha Mbakalo, eneobunge la Tongaren, Kaunti ya Bungoma katika mazishi ya Mzee Cheningi Lubao, viongozi hao hawakujadili changamoto zinazohangaisha Wakenya badala yake walizungumzia masilahi yao ya kibinafsi.

‘Kwa viongozi hao kujaribu kuungana si vibaya kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii. Lakini sidhani kwamba muungano wao una lolote jipya litakalosaidia kukwamua taifa hili kimaendeleo,” akasema.

Waziri huyo wa zamani wa Viwanda na Biashara, alisema kuwa muungano wa viongozi hao utawazidishia wananchi maumivu badala ya kutafuta suluhisho la changamoto tele zinazowaandama.

Dkt Kituyi, aliyejiuzulu mnamo Februari kama katibu mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD), analenga kumenyana katika kinyang’anyiro cha urais mwakani.

Kituyi arejea nyumbani kusaka baraka za urais

ONYANGO K’ONYANGO na BRIAN OJAMAA

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD) Mukhisa Kituyi amerejea nyumbani eneo la magharibi kusaka baraka za kuwania urais 2022.

Akiongea na wakazi mjini Kimilili Dkt Kituyi alisema safari yake ya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta kama rais wa tano wa Kenya imeng’oa nanga na “sitarudi nyuma”.

“Bunduki yangu ina bunduki moja ambayo inalenga Ikulu pekee na sitaangalia nyuma,” akasema huku akinadi kama kiongozi bora ambaye anaweza kuliongoza taifa hili.

Kituyi ambaye alihudumu kama Mbunge wa Kimilili kwa mihula mitatu kuanzia 1992 hadi 2007 alisema atatumia tajriba aliyopata katika ngazi ya kimataifa kuinua uchumi wa Kenya.

“Niko tayari kuongoza Kenya ili iweze kufikia upeo wa juu kimaendeleo. Nitaweza kufikia hili kutokana na tajriba yangu ya miaka mingi kama waziri serikalini na katibu mkuu wa UNCTAD ambalo ni asasi ya kimataifa,” akasema.

Dkt Kituyi ambaye amewahi kuwa Waziri wa Biashara katika utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, alisema aliamua kurejesha nyumbani “kupata baraka kwa watu wetu kabla ya kuanza kampeni rasmi ya urais.”

“Ukitafuta kiti kama cha urais utahitaji kuzunguka kote nchini. Lakini unapofanya hivyo wananchi watakuuliza ikiwa una uungwaji mkono kutoka nyumbani kwenu,” akasema.

Kwa hivyo Dkt Kituyi aliwasihi wakazi wa eneo la magharibi wamuunge mkono ili aweze kupata uungwaji mkono kutoka maeneo mengine ya nchi.

Msafara mkubwa wa magari ulimsindikiza Dkt Kituyi kutoka uwanja mdogo wa ndege wa Matulo, eneo bunge la Webuye Magharibi. Alihutubia mikutano katika maeneo ya Ligulu, Misikhu, Kimilili, Kamukunywa na hatimaye nyumbani kwake Mbakalo katika eneo bunge la Tongaren.

Dkt Kituyi pia alifichua kuwa anafanya mazungumzo na vigogo kadhaa wa kisiasa, akitoa mfano wa mkutano kati yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga na Seneta wa Siaya James Orengo.

“Juzi nilikutana na Raila, Orengo, na Profesa Kivutha Kibwana na kuwasihi waniunge mkono katika safari hii ya kukomboa nchi kwa sababu ni marafiki zangu wa enzi wa ukombozi wa pili,” akasema.

Hata hivyo, ni Profesa Kibwana, ambaye ni Gavana wa Makueni, aliyepata nafasi ya kuhudhuria hafla ya Jumamosi Bungoma. Bw Odinga, Orengo, Kituyi na Kibwana ni miongoni mwa wanaharakati waliopigania ukombozi wa pili mapema miaka ya 1990s wakishinikiza kurejeshwa kwa mfumo wa utawala wa vyama vingi.

Hata hivyo, hatua ya Dkt Kituyi kuwania urais imesawiriwa kama itakayovuruga ndoto za kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya ambao pia wametangaza azma ya kuwania urais 2022.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

Mudavadi sasa akimbilia baraka za wazee kabla ya Muhkisa Kituyi

Na DERICK LUVEGA

KIONGOZI wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, amekimbilia kukutana na wazee wa jamii ya Waluhya siku chache baada ya aliyekuwa waziri Mukhisa Kituyi kutangaza rasmi atakutana na wazee na wadau wengine wa jamii kabla aamue rasmi kama atawania urais nchini.

Bw Mudavadi aliomba radhi kwamba hajawahi kufanya kikao na wazee baada ya kupewa hadhi ya kuwa msemaji wa jamii ya Waluhya mnamo 2016.

Kiongozi huyo wa ANC alitawazwa kuwa msemaji wa jamii hiyo katika hafla iliyoongozwa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli katika uwanja wa michezo wa Bukhungu, mjini Kakamega.

Hata hivyo, baraza la wazee wa jamii hiyo walimshauri Bw Mudavadi kupuuzilia mbali ujio wa Dkt Kituyi na aendelee na mipango yake kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Mwenyekiti wa baraza hilo Philip Masinde, aliyeongoza mkutano huo nyumbani kwa kiongozi huyo wa ANC, Malulu, kaunti ya Vihifa, alisema hata ikiwa hatapata bahati ya kuunda serikali, eneo la magharibi linafaa kuwa mshirika mkuu katika serikali ijayo.

“Sharti tuunde serikali ijayo. Lakini ikiwa kwa bahati mbaya hatutafanikiwa kufanya hivyo, sharti tuwe ndani ya serikali ijayo,” Mzee Masinde akasisitiza

.“Zamani tulikuwa na zaidi ya mawaziri watano. Leo, tunaambiwa sisi ni jamii nambari mbili kwa ukubwa nchini lakini hatuna waziri kutoka magharibi,” akaongeza mwenyekiti huyo ambaye ni mwanasiasa mkongwe kutoka kaunti ya Busia.

Alimtaka Bw Mudavadi kwenda kutafuta wandani wengine kutoka kwa wanasiasa wenye maono sawa na yake katika maeneo mengine ya nchi.

“Tuko nyuma yake kwa dhati, kwa maneno na vitendo. Sasa wajibu wako kwenda huko nje kusaka marafiki zaidi watakaokuwezesha kutimiza azma yako. Sisi tutakuwakilisha hapa vijijini,” Mzee Masinde akaeleza.

Kauli ya Masinde ilijiri baada ya wanachama wa baraza hilo kuapa kuunga mkono azma ya Mudavadi kuwania urais licha ya kwamba eneo la magharibi linaendelea kutoa wagombeaji wapya wa urais.Wazee hao walisema enzi ambazo “watu kutoka nje” walizuru eneo la Magharibi kiholela na kupata kura za wakazi zimepita.

Walisema wanataka uongozi ambao utafufua uchumi wa eneo hilo walilosema umeathirika pakubwa.Kwa upande wake, mwenyekiti wa baraza la Wazee wa Jamii ya Teso Ptala Naibei alisema kabila lake linazongwa na changamoto nyingi lakini hawataelekeza lawama kwa mtu yeyote.Alisema kabila hilo ambalo linaishi katika kaunti ya Busia limechanganyikiwa kwani halijapata mwelekeo wa kisiasa.

“Kwa hivyo, namwomba Bw Mudavadi kuzuru eneo letu ili auze sera zake,” akasema Mzee Naibei.Kauli yake iliungwa mkono na mwakilishi wa jamii ya Sabaot Bw Peter Chepkurui ambaye pia alimtaka Bw Mudavadi kuzuru eneo la Mlima Elgon.

Kwa upande wake, aliyekuwa Meya wa Webuye Patrick Kilaka alishangaa ni kwa nini kiongozi huyo wa ANC ameshindwa kufuata nyayo za babake, marehemu Moses Mudamba Mudavadi.

“Mzee Mudavadi aliacha jina ambalo hatujui lilitokomea wapi. Tuko wengi lakini hatuna uongozi. Mudavadi anafaa kutupa na kutuonyesha njia,” akasema, akiongeza kuwa bila kiongozi huyo wa ANC eneo zima la magharibi halina uongozi wa kisiasa.

Siasa za matusi ni hatari – Mukhisa Kituyi

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD) Mukhisa Kituyi amewaonya wanasiasa dhidi ya kuendesha siasa za chuki zenye madhara ya ufufuzi wa uchumi.

Kwenye kikao chake cha kwanza na wanahabari Jumapili katika hoteli moja jijini Nairobi Dkt Kituyi amesema inawezekana kwa wanasiasa kutofautiana kwa njia ya heshima bila yao wao kurushiana cheche za matusi kama ambavyo wamekuwa wakifanya katika siku za hivi karibuni.

“Ni makosa kwa baadhi ya wanasiasa nchini kuchukua tofauti za kisiasa kama sababu ya wao kurushiana matusi hadharani kwani hii itawaogofya wawekezaji. Tuendeshe siasa za ustaarabu na heshima,” akasema Dkt Kituyi.

Wanasiasa katika kambi za Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakitoa matamshi ya chuki, uchochezi na matusi katika majukwaa mbalimbali.

Hii ni kwenye harakati za wao kutetea misimamo yao ya kisiasa, wandani wa Dkt Ruto wakipinga BBI na wale wa Odinga wakiunga mkono mchakato huo wa marekebisho ya katiba.

Dkt Kituyi, ambaye zamani alikuwa Mbunge wa Kimilili na Waziri wa Biashara, alisema akipatiwa nafasi ya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta kama Rais wa tano wa Kenya, atatumia ujuzi wake katika Umoja wa Mataifa (UN) kubadilisha maisha ya Wakenya.

Hata hivyo, aliungama kuwa anafahamu changamoto zinazomsubiri katika azma yake ya kutimiza ndoto hiyo.

“Naingia kwenye kinyang’anyiro cha urais nikifahamu kuwa kuna wengine ambao walianza safari hii mapema kuniliko. Lakini ningependa kuwahakikisha Wakenya kuwa wakinipa nafasi hii, nitaleta mawazo mapya uongozini kutokana na tajriba kubwa ambayo nimepata katika mida ya kimataifa,” akasema Dkt Kituyi mwenye umri wa miaka 65.

Katibu huyo mkuu UNCTAD aliyejiuzulu juzi, alisema kuwa ataelekea nyumbani kwao Bungoma kusaka “baraka kutoka kwa wazee na kufanya mashauriano zaidi” kabla ya kurejea Nairobi kuzindua rasmi kampeni zake za urais.

Mukhisa Kituyi asema atagombea urais

Na BRIAN OJAMAA

KATIBU Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na ustawi (UNACTAD) Dkt Mukhisa Kituyi ametangaza kwamba atagombea urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2022.

Dkt Kituyi anajiunga na viongozi wengine kama Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, Musalia Mudavadi wa chama cha Amani National Congress na Kalonzo Musyoka wa Wiper ambao wametangaza azima ya kugombea urais kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Akizungumza na wanahabari mjini Bungoma Jumamosi, Dkt Kituyi alisema kwamba, kwa muda ambao amehudumu katika Umoja wa Mataifa, amepata tajiriba ya kumwezesha kuongoza Kenya.

“Sio siri tena, nitagombea urais kwenye uchaguzi wa 2022, hakuna anayefaa kutuagiza tuunge fulani mkono. Tunahitaji Rais atakayeokoa nchi hii kutoka kwa mateso yanayoletwa na uchumi mbaya,” alisema.

Alisema lengo lake la kugombea urais ni kutatua matatizo ya Wakenya na kuimarisha uchumi.