• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
MAUAJI YA SHARON: Gavana Obado atoweka machoni pa umma

MAUAJI YA SHARON: Gavana Obado atoweka machoni pa umma

Na PETER MBURU

KUTOONEKANA hadharani kwa Gavana wa Migori Okoth Obado wakati amekuwa akihusishwa na mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo Sharon Otieno kumeibua maswali tele kuhusu alipo kiongozi huyo.

Tangu mkasa wa utekaji nyara wa mwanahabari wa ‘Nation’ Barrack Oduor na Bi Otieno Jumatatu na baadaye kuuawa kinyama kwa Bi Otieno baada ya Bw Oduor kujinasua kutoka mikononi mwa wauaji hao, washirika wa karibu wa Bw Obado wamehusishwa na mauaji hayo.

Hata hivyo, licha ya msaidizi wake wa kibinafsi Michael Oyamo kukamatwa Jumanne baada ya kuwaingiza Bw Oduor na Bi Otieno katika mtego uliopelekea mauaji ya mwanafunzi huyo aliyekuwa na mimba ya miezi saba, Gavana huyo hajaonekana, jambo ambalo sasa limeibua maswali kuhusu alipo.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa gavana huyo alifaa kuwakilisha Baraza la Magavana (CoG) katika hafla ya kuhamasisha kuhusu kilimo na mazingira kama mwenyekiti wa kamati ya baraza hilo mjini Kigali, Rwanda kuanzia Jumanne Septemba 4.

Hata hivyo, Gavana Obado hakuhudhuria hafla hiyo ambayo inakamilika leo, ikiaminika kuwa kukosekana kwake kulichochewa na mauaji hayo na uchunguzi unaoendelea hadi sasa, licha ya watu walio karibu naye kudhihirisha hilo.

“Ni kweli kuwa gavana alifaa kuwakilisha CoG katika hafla hiyo ya Rwanda. Lakini kwa sasa siwezi kuwafahamisha alipo kwa hakika,” akasema mtu anayefahamu ratiba ya gavana huyo.

Vilevile, Bw Obado jana alistahili kumpokea Naibu wa Rais William Ruto katika ziara yake ya kaunti ya Migori japo hakujitokeza.

Ingawa mkuu wa mawasiliano katika afisi yake Nicholas Anyuor amekuwa akijibu maswali yanayoelekezwa kwa mwajiri wake, alikataa kueleza alipo gavana huyo.

“Gavana akihitajika kutoa ushahidi kwa polisi atajiwasilisha,” akasema Bw Anyuor.

Mdokezi mwingine alifahamisha Taifa Leo kuwa, gavana huyo alionekana katika afisi yake kwa mara ya mwisho Ijumaa wiki iliyopita, na kuwa alisafiri kuelekea Nairobi Jumatatu ili kusubiri safari yake ya Rwanda siku iliyofuata. Siku hiyo anayodaiwa kusafiri kuelekea Nairobi ndiyo waliyotekwa nyara Bw Oduor na Bi Otieno, kabla ya maiti ya Bi Otieno kupatikana Jumatano asubuhi msituni.

Kumekuwa na madai kuwa marehemu alikuwa na uja uzito wa gavana huyo na kuwa, waliwasiliana mara kadha siku ya tukio, lakini wapelelezi wanajaribu kutegua kila kilichotendeka.

You can share this post!

Ajabu ya ng’ombe kuua simba zizini

Elachi alilia Jubilee imwokoe

adminleo