• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kipchoge sasa halali akiwazia mamilioni ya Berlin Marathon

Kipchoge sasa halali akiwazia mamilioni ya Berlin Marathon

Na Geoffrey Anene

BINGWA wa Olimpiki Eliud Kipchoge anasubiri kwa hamu kubwa mbio za kifahari za Berlin Marathon zitakazofanyika wiki mbili mapema kuliko miaka mingine hapo Septemba 16 nchini Ujerumani.

Kupitia kwa mtandao wake wa Twitter, bingwa huyu mara mbili wa Berlin Marathon alisema jana, “Berlin ni mji spesheli kwangu. Nasubiri kwa hamu kubwa kurejea uwanjani kushindania taji la Berlin Marathon tena hapo Jumapili.”

Kipchoge atakuwa akiwinda taji lake la tatu jijini Berlin baada ya kuibuka mshindi mwaka 2015 na 2017.

Anatarajiwa kuwa na motisha hata zaidi baada ya kampuni ya magari ya Isuzu East Africa kumuahidi Septemba 5 kumpa gari (Isuzu Dmax double-cab) lenye thamani ya Sh20 milioni akifuta rekodi ya Kimetto.

Vilevile, mbali na tuzo ya mshindi ya Sh4.6 milioni, waandalizi wa Berlin Marathon wametengea mkimbiaji atakayevunja rekodi ya Mkenya Dennis Kimetto bonasi ya Sh5.8 milioni. Pia kuna zawadi ya kifedha kwa wakimbiaji watajika kujitokeza kushiriki mashindano.

Kipchoge alishinda makala yaliyopita kwa saa 2:03:32, ambayo ni sekunde 35 nje ya rekodi ya Kimetto. Muda wake bora katika marathon ni saa 2:03:05, ambao ni sekunde nane nje ya rekodi ya dunia. Alitimka muda huu akishinda taji la London Marathon nchini Uingereza mwaka 2016.

Kipchoge ameshinda marathon zake nane zilizopita na tisa kwa jumla katika marathon 10 ameshiriki tangu ajitose katika mbio hizi za kilomita 42 mwaka 2013.

Hata hivyo, atakabiliwa na tishio kubwa kutoka kwa mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia na Mkenya mwenzake Wilson Kipsang pamoja na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 Zersenay Tadesse kutoka Eritrea.

Kipsang’ alishinda makala ya mwaka 2013 kwa saa 2:03:23, ambayo ilikuwa rekodi ya dunia wakati huo.

Wakenya hawa wameapa kushinda Berlin Marathon mwaka huu, huku Kipchoge akilenga kuvunja rekodi ya dunia ya saa 2:02:57, ambayo Kimetto aliweka jijini Berlin mwaka 2014.

Baadhi ya washiriki watajika katika kitengo cha wanawake katika makala haya ya 45 ni Muethiopia Tirunesh Dibaba na Wakenya Edna Kiplagat na Gladys Cherono, ambaye atakuwa akitafuta taji lake la tatu la Berlin Marathon baada ya kunyakua yale ya mwaka 2015 na 2017. Kiplagat ni bingwa wa New York Marathon mwaka 2010, London Marathon mwaka 2014 na Boston Marathon mwaka 2017.

Vile vile, alishinda mataji ya Riadha za Dunia mwaka 2011 na 2013. Dibaba alishinda London Marathon mwaka 2017. Makala ya 45 ya Berlin Marathon mwaka 2018 yamevutia washiriki 40, 000.

Sababu ya makala haya kufanyika mapema ni maandalizi yanayoendelea ya siku ya kuadhimisha siku ya Umoja wa Ujerumani (Day of Germany Unity) hapo Oktoba 3. Berlin ni moja ya mashindano makubwa yam bio za kilomita 42 yanayounda Marathon Kuu Duniani (WMM).

Mengine ni Tokyo (Japan), Boston (Marekani), London (Uingereza) na Chicago na New York (Marekani). Mshindi wa Marathon Kuu Dunia hutunukiwa Sh25.2 milioni. Kipchoge alishinda makala mawili yaliyopita ya marathon kuu duniani.

You can share this post!

Mswada bungeni kupunguza miaka ya kitambulisho hadi 16

Vipaji vyachochea KPL kuanzisha ligi kuu ya wafungwa

adminleo