• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
Wito kituo cha kuokoa wasichana waliodhulumiwa kijengwe

Wito kituo cha kuokoa wasichana waliodhulumiwa kijengwe

NA KALUME KAZUNGU

MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali na wanaharakati wa kupigania haki za watoto kaunti ya Lamu wanaitaka serikali na wadau kuanzisha kituo maalum cha kuwaokoa watoto hasa wasichana wanaopitia dhuluma mbalimbali maishani, ikiwemo kulazimishwa ndoa za mapema, mimba zisizohitajika na ubakaji.

Katika kikao na wanahabari mjini Hindi Ijumaa, maafisa wa Shirika la World Vision Kenya na wale wa Miungano ya kijamii walisema kuna haja ya wasichana wote wanaotungwa mimba au kubakwa wakiwa shuleni kujengewa kituo maalum kitakachowawezesha kuendeleza masomo yao bila hofu.

Afisa Msimamizi wa World Vision kwenye kaunti za Lamu, Tana River na Garissa, Emmanuel Mkoba na Afisa Mtetezi wa Haki za Watoto, Kaunti ya Lamu, Bi Malika Mwangi, walisema inasikitisha kwamba licha ya Lamu kushuhudia visa vya mara kwa mara vya wasichana kubakwa, kutungwa mimba na hata kuozwa kwa lazima, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa ili kujenga kituo cha kuokoa waathiriwa kama hao.

Kituo cha kuokoa watoto waliodhuklumiwa ambacho kiko karibu ni kile cha Malindi, Kaunti ya Kilifi.

Bw Mkoba aliiomba kaunti, serikali kuu na wadau mbalimbali kujitokeza ili kuanzisha kituo hicho.

Mwakilishi Mwanamke, Kaunti ya Lamu, Bi Ruweida Obbo akiandamana na afisa wa watoto Kaunti ya Lamu, Maxwell Titima muda mfupi baada ya kuokoa wasichana waliodhulumiwa eneo la Kiunga, Kaunti ya Lamu. Wito umetolewa kwa kituo maalum kujengwa ili kuwaokoa wasichana waliodhulumiwa. Picha/ Kalume Kazungu

“Wasichana wengi wa umri wa kwenda shule wamekuwa wakiacha masomo punde wanapotungwa mimba au kubakwa kutokana na hofu ya kukejeliwa na wenzao wanaporudi shuleni mwao. Suluhu ya pekee itakayohakikisha wasichana kama hao wanaendelea na masomo ni kituo maalum cha kuokoa waathiriwa hao kianzishwe Lamu,” akasema Bw Mkoba.

Bi Malika aliwalaumu baadhi ya wazazi kwa kuchangia visa vya dhuluma hasa za kingono na ndoa za mapema miongoni mwa wasichana wao.

Bi Malika alisema kituo hicho kikibuniwa Lamu kitakuwa msaada mkubwa kwa jamii ambayo imekubwa na changamoto za muda mrefu hasa kuhusiana na elimu ya mtoto wa kike.

“Kituo kikibuniwa kitachangia pakubwa kuboreshwa hata kwa elimu ya mtoto wa kike eneo hili. Isitoshe, ni jukumu la mzazi kusimama kidete kuona kwamba wasichana wao wanasoma. Inasikitisha kuona kwamba baadhi ya wazazi wanachangia kudhulumiwa kwa watoto wao. Tuko macho na tutawashtaki wazazi kama hao,” akasema Bi Malika.

Kulingana na ripoti ya World Vision, tawi la Lamu, jumla ya wasichana 25 walidhulumiwa kwa kubakwa na wazazi wao kaunti ya Lamu kati ya Januari na Mei mwaka huu.

Baadhi ya maeneo ambayo yameathirika sana na dhuluma dhidi ya watoto ni pamoja na Hindi, Bobno, Sabasaba, Bar’goni, Kiunga na sehemu zingine.

You can share this post!

Mpango wa upangaji uzazi wazinduliwa Lamu

Kanisa la pasta anayewachochea watoto kuacha shule kuvamiwa

adminleo