• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Mwenye matatu iliyohusika kwa ajali ajitokeza kusaidia manusura

Mwenye matatu iliyohusika kwa ajali ajitokeza kusaidia manusura

NA RICHARD MAOSI

MMILIKI wa basi lililowaua watu 9 na kuwaachia wengine majeraha mkesha wa kuamkia Jumapili katika barabara ya Nakuru-Eldoret, amejitokeza kuwasaidia manusura.

Kwa mujibu wa muuguzi mkuu Bi Anyise Serem kutoka hospitali ya rufaa ya Eldama Ravine, mmiliki huyo aliahidi kutoa njia za usafiri kwa walioathiriwa hadi makwao.

“Jumatano pia tulitembelewa na OCPD na afisa mwingine ambao waliahidi kufanya uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali hiyo,” alisema.

Naibu msimamizi wa huduma za hospitali hiyo Bw Masai Shipaya, aliongezea kuwa japo hospitali haina vifaa vya kutosha kushughulikia wagonjwa mahututi walifanikiwa kutoa huduma ipasavyo.

Vilevile alielezea haja ya kuongeza idadi ya matabibu wenye ujuzi maalum katika nyanja ya upasuaji.

Mmoja wa majeruhi Wycliffe Kibor kutoka Cheptais mlima Elgon alisema anaendelea kupata nafuu baada ya kuhudumiwa na madaktari.

Alieleza furaha yake kwa kunusurika kifo na hali yake inaendelea kuboreka kila siku.

Taifa Leo Dijitali ilipozuru Eldama Ravine kutathmini hali halisi, kati ya waathiriwa 75 waliofikishwa hospitalini ni 4 tu waliokuwa wamelazwa wakiendelea kupokea matibabu.

Ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Kamara ilihusisha lori na basi linalomilikiwa na kampuni ya Greenline Sacco.

Aidha watu 56 waliruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kutibiwa na kuhakikishiwa walikuwa katika hali nzuri.

Wengine saba walisafirishwa hadi kwenye hospitali ya rufaa ya Moi,huku wengine 4 wakiendelea kutibiwa katika hospitali ya Eldama Ravine.

“Madaktari wetu waliweza kudhibiti hali,pia serikali ya kaunti imeonyesha juhudi kufanikisha huduma tangu jana,” Masai aliongezea.

You can share this post!

Wachezaji watatu warejea katika kikosi cha Shujaa

Huenda Zidane atue Juve, Chelsea kula hu

adminleo