• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
Serikali yapiga marufuku ukataji wa miti kwa siku 90

Serikali yapiga marufuku ukataji wa miti kwa siku 90

Na VALENTINE OBARA

Kwa ufupi:

  • Amri hiyo ilitolewa na Naibu Rais William Ruto, wakati ambapo athari ya kiangazi inazidi kushuhudiwa nchini
  • Wizara ya Mazingira na Misitu itahitajika kushauriana na wadau wote na kutoa mapendekezo kuhusu hatua zinazofaa kuokoa mazingira
  • Ukataji wa miti misituni umekuwa ukishuhudiwa sana kutokana na unyakuzi wa ardhi, biashara za mbao na uchomaji wa makaa

SERIKALI imepiga marufuku ukataji wa miti katika misitu yote nchini, iwe ni ya kitaifa au ya kijamii.

Amri hiyo ya kisheria itakayodumu kwa siku 90 ilitolewa Jumamosi na Naibu Rais William Ruto, wakati ambapo athari ya kiangazi inazidi kushuhudiwa katika maeneo tofauti nchini.

Kulingana na Bw Ruto, kiangazi kikali ambacho kimeshuhudiwa kwa karibu miaka mitatu sasa kimesababisha uhaba wa maji mitoni na katika chemchemi za maji.

Alisema hali hii imetokana na ukataji wa miti kiholela pamoja na jinsi watu wanavyonyakua maeneo yanayotega maji na hivyo basi kuathiri vibaya uwezo wa nchi kuzalisha chakula cha kutosheleza mahitaji ya umma.

“Kutokana na haya, serikali imepiga marufuku mara moja ukataji wa miti katika misitu yote ya kitaifa na ya kijamii kwa siku 90 ili kutoa nafasi kwa utathmini wa misitu yote ya Kenya,” akasema.

Katika kipindi hicho, Wizara ya Mazingira na Misitu itahitajika kushauriana na wadau wote ili kubuni jopo kazi la kufanyia misitu utathmini na kuchapisha ripoti baada ya siku 14 kutoa mapendekezo kuhusu hatua zinazofaa kuchukuliwa kuokoa mazingira ya Kenya.

 

Hatua mwafaka

“Wizara ya Masingira na Misitu pamoja na wizara zingine zote husika, idara na taasisi za serikali kuu na za kaunti zimeagizwa kushirikiana kuchukua hatua mwafaka mara moja kutekeleza agizo hili,” akasema.

Shirika la Kenya Red Cross lilitangaza kuna watu zaidi ya milioni tatu wanaokumbwa na janga la njaa nchini, huku idara ya utabiri wa hali ya hewa ikisema msimu wa mvua utakaoanza mwishoni mwa Machi utashuhudia kiwango kidogo cha mvua.

Ukataji wa miti misituni umekuwa ukishuhudiwa sana kutokana na unyakuzi wa ardhi zilizotengwa kuwa misitu, mbali na biashara za mbao, uchomaji wa makaa na jinsi jamii mbalimbali zinavyojenga vijiji vyao misituni.

Miongoni mwa misitu ambayo imeathirika zaidi na ukataji wa miti kiholela ni msitu wa Mau ambao unategemewa kutega maji yanayoingia mito ya Ewaso Ng’iro Kusini, Sondu, Mara na Njoro. Mito hii hutiririza maji kwa maziwa makubwa ya Victoria, Nakuru na Natron.

Mbali na msitu wa Mau, misitu mingine katika maeneo tofauti nchini pia yamekuwa yakiharibiwa kama vile msitu wa Ngong ulio Kaunti ya Nairobi.

You can share this post!

Maraga arukwa katika uteuzi wa Jaji Nyachae

Baa la njaa: Watoto sasa wazirai shuleni

adminleo