• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Serikali yalemewa na gharama ya kutunza wafungwa, wale wa makosa madogo kuachiliwa

Serikali yalemewa na gharama ya kutunza wafungwa, wale wa makosa madogo kuachiliwa

Na JOSEPH WANGUI

WAFUNGWA wa makosa madogo wanatarajiwa kuanza kuachiliwa huru huku serikali ikijizatiti kupunguza gharama ya kuwatunza gerezani ambayo kwa sasa ni Sh388 milioni kila mwezi.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), tayari imeanza zoezi la kutathmini upya kesi za wafungwa walioshtakiwa kwa makosa madogo.

Hatua hivyo, inanuia kupunguza idadi kubwa ya wafungwa waliojaa katika magereza ya nchini, Afisa Mkuu Msaidizi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Bw Alloys Kemo alisema.

Aliongeza kuwa zoezi hilo pia litawezesha serikali kuokoa pesa ambazo zitaelekezwa katika matumizi mengine.

Bw Kemo alikuwa akizungumza jana alipozuru gereza la King’ong’o jini Nyeri. Alisema kwa sasa kuna takriban mahabusu 54,000 katika magereza ya humu nchini na serikali hutumia Sh240 kila siku kutunza kila mmoja wao.

 

Sh12.9 milioni kila siku

Kwa jumla, serikali hutumia zaidi ya Sh12.9 milioni kila siku na Sh388 milioni kila mwezi kugharamia mavazi, maji, chakula na mahitaji yao mengine.

Kikundi cha waendesha mashtaka tayari kimezuru gereza la Nairobi, gereza la wanawake la Lang’ata, magereza ya watoto ya Kamiti na Kabete, gereza la Embu na gereza la Nyeri kutathmini upya kesi za wafungwa hao wanaoweza kuachiliwa.

“Tunazuru magereza kubaini changamoto ambazo mahabusu hupitia katika harakati za kutafuta haki. Tunataka wafungwa wa makosa madogo waachiliwe kwani hiyo itapunguza gharama ambayo serikali inatumia,” alieleza Bw Kemo.

Aliongeza kuwa zoezi hilo pia litawezesha kuharakisha kesi za wafungwa hao.

 

Kucheleweshwa kwa kesi

Afisa Mkuu huyo Msaidizi alidokeza kuwa matokeo ya awali ya zoezi hilo yameonyesha kuwa, kucheleweshwa kwa kesi kumechangiwa pakubwa na visa vya mashahidi kukosa kufika kortini kutoa ushahidi na uchanganuzi wa ushahidi katika maabara ya serikali.

Bw Kemo alisema: “Kuna sababu zingine ikiwemo uhaba wa mahakimu na majaji, kujikokota kwa maafisa wa upelelezi, mazoea ya mawakili kuomba kesi ziahirishwe, mwendo wa pole pole wa kusikizwa kwa kesi na taratibu chungu nzima.”

Aliongeza kuwa baada ya zoezi hilo kukamilika kote nchini ofisi ya DPP itawasilisha ripoti na mapendekezo jinsi ya kupunguza idadi ya mahabusu katika magereza.

 

You can share this post!

Wakuu wa shule wataka ruhusa watoze wazazi ada ya kujenga...

KINAYA: Jenerali Miguna Miguna atarudi Kenya akiwa shujaa...

adminleo