• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
Wanaobadilisha mikondo ya mito eneo la Mlima Kenya waonywa vikali

Wanaobadilisha mikondo ya mito eneo la Mlima Kenya waonywa vikali

 

Na LAWRENCE ONGARO

WAKULIMA wanaogeuza mkondo wa mito kuingia mashambani mwao wamepewa onyo kukomesha mtindo huo.

Kamishna wa eneo la Kati, Wilfred Nyagwanga, alisema Jumatano kwamba kuna ripoti wamepokea inayoeleza kuwa watu fulani wamebuni mtindo wa kugeuza mkondo wa mito kuingia kwenye mashamba yao huku mito hiyo ikionekana kupungua maji.

Alitaja mito kama Chania na Thika iliyoko katika Kaunti ya Kiambu na ile ya Sagana iliyoko eneo la Murang’a.

“Kutokana na ukame tunaoshuhudia kwa sasa, tunaona mito kadha ikionyesha dalili ya kukauka hivi karibuni. Kwa hivyo, kutoka leo
nimetoa amri hakuna  mtu yeyote ataruhusiwa kunyunyizia maji shamba lake ama kuvuta maji  kwa njia isiyokubalika,” alisema Bw Nyagwanga.

Aliyasema hayo mnamo Jumatano mjini Thika alipozuru eneo hilo kushuhudia jinsi wakazi wake wanavyojiandikisha kupata Huduma Namba.

“Nimeridhika na  jinsi usajili huo unavyoendeshwa na kwa hivyo nawahimiza wananchi wajitokeze kwa wingi ili kujisajili,” alisema Bw
Nyagwanga.

Alisema kwa siku za hivi karibuni wananchi wengi wametoa malalamiko kuhusu ukosefu wa maji katika mito kadha ya eneo hilo. Lakini
ilibainika watu fulani wamekuwa wakitumia  mbinu  mbaya ya kutumia maji hayo kutoka  kwenye mito hiyo.

Alisema  iwapo hali hiyo itaendelea hivyo bila hatua ya dharura kuchukuliwa bila shaka mifugo hasa ng’ombe huenda watafariki kutokana na ukosefu wa maji ya kunywa.

Alisema atahakikisha mito hiyo inalindwa dhidi ya watu wanaotaka kuletea wakazi shida ya kupata maji  ambayo ni muhimu kwa binadamu.

Ilidaiwa kuwa eneo la Thika Mashariki ambayo inapakana na Murang’a na Machakos limepata pigo kubwa kwa sababu mito iliyoko katika maeneo
hayo imeanza kukauka jambo ambalo limekuwa hasara kwa wafugaji wengi.

“Sisi kama wakazi wa eneo la Kilimambogo, Thika Mashariki tunalazimika kutembea mwendo mrefu kutafuta lishe ya mifugo na maji,”
alisema Dominic Waita na kuongeza tunaiomba serikali itafute njia ambayo itaweza kutunusuru kutokana na janga hilo la ukame.

Wakazi hao walisema tayari wametayarisha mashamba yao wakingojea mvua inyeshe lakini wataalamu wa hali ya hewa “wametushtua tena
kusema ya kwamba tusitarajie mvua yoyote  msimu huu unaokuja”.

“Msimu uliopita tulijiandaa vyema kwa upanzi wa  chakula na tulifanikiwa, lakini wakati huu mambo yametuendea mrama hata hatujui
tufanye nini,” alisema Bi Mary Kinuthia wa Gatuanyaga, Thika Mashariki.

You can share this post!

Wabunge wa kike wa Jubilee wamtaka Rais kuitisha mkutano wa...

Transfoc mbioni kulipiza kisasi

adminleo