• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kabogo sasa aabiri treni la ‘Tangatanga’

Kabogo sasa aabiri treni la ‘Tangatanga’

PHYLIS MUSASIA NA CECIL ODONGO

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu William Kabogo, Jumapili alitangaza kwamba eneo la Mlima Kenya litamuunga mkono Naibu Rais, Dkt William Ruto kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2022, matamshi ambayo yameshangaza wengi ikizingatiwa kuwa Bw Kabogo amekuwa mkosoaji mkubwa wa Dkt Ruto.

Bw Kabogo alitoa tangazo hilo la kushangaza wakati alipoandamana na Naibu Rais kwenye hafla ya mchango wa fedha kugharimia ujenzi wa kanisa la waumini wa Akorino katika eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru.

“Hatuhitaji mwelekeo wowote kutoka kwa mtu yeyote kwa sababu tushaamua kumuunga mkono Naibu Rais,” akasema Bw Kabogo.

Katika uchaguzi wa mwaka 2017, Bw Kabogo alishutumiwa vikali na viongozi kutoka ukanda wa Mlima Kenya alipojitokeza hadharani na kumwambia Dkt Ruto asitarajie kuungwa mkono kutoka eneo hilo kwa kuwa kuna viongozi bora kumshinda watakaowania kiti cha urais.

Bw Kabogo vilevile alimlaumu Dkt Ruto kwa kuvuruga uteuzi wa chama cha Jubilee mnamo 2017 na kusababisha kushindwa kwa wagombeaji aliowaona kama tishio kwenye nia yake ya kuwania urais 2022.

Wengi, hata hivyo, wanasubiri kuona jinsi Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu atakavyochukulia matamshi ya Bw Kabogo baada ya uhasama wa wawili hao kuendelea kutokota tangu 2017.

Bw Waititu amekuwa gavana wa pekee kutoka Mlima Kenya kuonekana kumvumisha Dkt Ruto na huandamana naye mara kwa mara kwenye mikutano yake kila wakati maeneo mbalimbali ya nchi.

Katika kile ambacho kilidhihirisha zaidi kuwa yuko kwenye kambi ya Naibu Rais, mbunge huyo wa zamani wa Juja pia alisema kura ya maoni haifai kuandaliwa kwa sasa na ikilazimu basi iandaliwe baada ya miaka mitatu.

Wakati wa mkutano huo, Dkt Ruto alikariri kwamba yuko tayari kupambana na wawaniaji wengine kung’ang’ania tiketi ya chama cha Jubilee ili kuwania urais 2022.

“Hiki chama si lazima kiongozwe na Ruto, kama kutakuwa na mtu bora kuliko Ruto, tutamuunga mkono. Hata hivyo, sote tutaungana,” akasema Dkt Ruto huku akishangiliwa na waumini.

“Chama cha Jubilee ndicho huendesha serikali na shughuli zote za maendeleo zikiwemo Ajenda Nne za serikali ambazo zinathaminiwa sana na Rais Uhuru Kenyatta. Ni chama cha kila Mkenya na ndicho kinachotekeleza miradi ya maendeleo. Wale wanaozungumzia rekodi yetu ya maendeleo wanafaa kukoma kwa sababu tunajua wana nia ya kutugawanya kisiasa,” akaongeza Dkt Ruto.

Naibu Rais alidhihaki chama cha KANU na ODM kwa kushindana naye akisema yuko kifua mbele kisiasa, idadi ya wabunge wa chama tawala ikiwa ithibati ya hilo.

“Kama wewe ni mtu wa KANU ama ODM, una nia gani na chama chetu, fanyeni mambo yenu tupatane kwenye debe,” akasema Dkt Ruto na kuwasisimua waumini. Wengine walioandamana na Dkt Ruto ni Seneta wa Nakuru Susan Kihika, Naibu Gavana Dkt Erick Korir na zaidi ya wabunge 10.

You can share this post!

Jericho Allstars na South B United kuwasha moto Chapa Dimba

Walioasi Al Shabaab sasa wajiunga na magenge Pwani

adminleo