• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Chokoraa aliyetekwa na vileo sasa ni balozi dhidi ya unywaji pombe

Chokoraa aliyetekwa na vileo sasa ni balozi dhidi ya unywaji pombe

Na SAMMY WAWERU

PETER Muhia, ni jina ambalo alipewa mwaka wa 1990 na msamaria mwema. Akivuta mawazo yake nyuma anapohijiwa na Taifa Leo Dijitali, anaona maisha asiyoyatamani tena.

Ingawa anasema hajui mwaka aliozaliwa, wazazi wake waliko na majina halisi waliyompa, alikuwa chokoraa mjini Limuru.

“Jina ninalotambulika nalo kwa sasa nilipewa mwaka wa 1990 na msamaria mwema Nyandarua, aliyenichukua ili kupashwa tohara,” anafafanua Bw Muhia.

Muhia ni jina la jamii ya Agikuyu, lenye maana ya kuungua. Maisha ya barobaro huyu akiwa mchanga yalikuwa ya mitaa, ambapo anasema alitegemea chakula kilichotupwa kwenye majaa.

Licha ya kupata vibarua Limuru na Thika kuosha vyombo katika mikahawa, Muhia alitekwa na unywaji wa pombe minghairi ya kubagua aliyobugia.

“Kwa siku nilikuwa nikitia mfukoni mapato ya Sh500. Pia nilikuwa nikitekea watu maji na kupokea Sh20 kwa awamu, lakini hela zote ziliishia kwa pombe,” asimulia.

Bw Peter Muhia, akiwa katika hafla ya kufuzu uasi wa pombe, chini ya mradi wa Kaa Sober ulioendeshwa na gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, mnamo Februari 26, 2019 katika uwanja wa Ndumberi, Kiambu. Picha/ Sammy Waweru

Ni uamuzi ambao ulimgeuza kuwa mateka wa pombe. Maisha yakawa kufanya kazi, kunywa na kurejea mtaani. “Nilikuwa mtu asiyejijua, nilikunywa na hata kulala katika baa wakati mwingine,” anaongeza.

Alipata jiko, japo hakumbuki ulikuwa mwaka upi. Anaokumbuka ni 2007, mke wake alipoaga.

Hakufa moyo, alioa tena 2016 na wa pili alikuwa na watoto wawili. Anaeleza kwamba walijaaliwa kupata mtoto mmoja 2017, na akiwa na miezi miwili kibarafu wake wa roho alimuacha kwa sababu ya kunywa kupindukia kiasi cha kuzua vita.

“Wakati aliponiacha na mtoto wa miezi miwili, nilikuwa nikiishi Kiambu. Mambo yalizidi unga kwa sababu ya mzongo wa mawazo, pombe ikawa ndiyo suluhu,” anasema. Mwanawe ambaye kwa sasa ametimiza umri wa miaka miwili, alilelewa na majirani wake.

Afueni kuacha pombe

Kiambu ni miongoni mwa kaunti zinazotajwa kuathirika kwa unywaji wa pombe. Gavana wa sasa Ferdinand Waititu na mbunge mwakilishi wa wanawake, Gathoni Wa Muchomba, wamekuwa katika mstari wa mbele dhidi ya pombe na utumizi wa dawa za kulevya.

Mradi wa Kaa Sober ulioanzishwa na Bw Waititu 2018 kurekebisha watekwa wa pombe kwa kuwahusisha katika vibarua, ingawa ulikamilika Februari mwaka huu baada ya waasi kufuzu, ndio ulimnusuru Peter Muhia. “Nilijiunga na Kaa Sober Machi 2018 kupitia chifu wa eneo nililoishi,” anadokeza.

Uamuzi wa busara kuacha pombe, ulifungua mianya ya ufanisi kwa Bw Apollo Maina ambaye kwa sasa ni mwalimu Murang’a na mkulima hodari. Picha/ Sammy Waweru

Walionuwia kuacha unywaji wa pombe walikuwa wakilipwa Sh400 kwa siku. Isitoshe, walisajiliwa kufanya mafunzo ya kozi mbalimbali kama vile usemeremala, uashi, sanaa, ususi na ushonaji wa mavazi katika taasisi tofauti za elimu ya juu Kiambu.

Mradi huo pia ulitumika kuwapeleka mafunzo ya mapishi na hata kuwapa kitita cha Sh20, 000 kuanzisha biashara.

“Mtaweza kujianzishia biashara ili mjiimarishe kimaisha. Nikifanya kampeni 2017 niliahidi wakazi wa Kiambu, vijana nitawasaidia kuangazia suala la ukosefu wa ajira. Hatua hii ni mojawapo kutatua ukosefu wa kazi,” alisema gavana Ferdinand Waititu, akihutubu katika hafla ya kufuzu kwa waasi hao Februari 26, 2019 katika uwanja wa Ndumberi.

Wakati wa mahojiano, Bw Muhia aliambia Taifa Leo Digitali kuwa mpango wa Kaa Sober ulimuwezesha kusomea cheti cha mafunzo ya upishi katika Taasisi ya Masomo ya Kiufundi ya Kamirithu, Kiambu.

“Ninaelewa barabara kupitia mafunzo niliyopata kuoka keki hasa za harusi na vyakula mbalimbali,” akasema.

Akiwa katika shamba lake la maparachichi. Picha/ Sammy Waweru

Anasema lengo lake ni kupata tanuri, jiko la kuoka keki, ili apalilie kozi aliyopata akieleza kwamba aliichagua kwa ajili ya mapenzi yake kufanya upishi.

Mwalimu wa kuigwa baada ya kuacha pombe

Mwalimu Apollo Maina kutoka eneo la Kigumo kaunti ya Murang’a, ambaye miaka ya tisini alikuwa mtumwa wa pombe hasa ile haramu anapongeza Bw Muhia kwa uamuzi wake akiutaja kuwa ni wa busara.

Kulingana naye, anasema yaliyopita yasiwe kikwazo kwa Muhia kutimiza ndoto zake maishani akimhimiza kukaza kamba kujiimarisha kimaadili na kimaisha. Akitoa mfano wake, anasema alipohitimu kidato cha nne 1994, alifanya vibarua vya hapa na pale ili kusukuma gurudumu la maisha.

Anaeleza kwamba mapato aliyopokea, aliyaelekeza kwa mgema. Anasema uraibu wake katika mvinyo ulisababisha kumwaga unga mnamo 1998, ambapo mwajiri wake alichoshwa na sarakasi za kunywa kupindukia kiasi cha kusahau majukumu yake.

“Nilikuwa nimeajiriwa kama shambaboi. Bosi alighadhabishwa na tabia zangu za ulevi, akanifuta kazi,” anasimulia Bw Maina. Ni kufuatia hilo, ambapo alikata kauli ya kuacha pombe maishani.

Mwaka uliofuata, 1999, aliiga nyayo za baba yake kufanya kilimo, ambapo alikuza mboga kama vile spinachi, sukuma wiki, kabichi. Ilimgharimu mtaji wa Sh2, 000 pekee kuanza shughuli hiyo katika kipande chake cha shamba cha urithi. Pia aliwekeza katika ufugaji wa ng’ombe.

Kwa kuwa alikuwa na cheti cha kuhitimu kidato cha nne, KCSE, na alikuwa na matamanio kusomea taaluma ya ualimu, baada ya kutuma maombi kwa taasisi mbalimbali zinazotoa mafunzo hayo nchini, 2010, alipata mwaliko kujiunga na Chuo cha Ualimu cha Moi Teachers, Baringo. Anafichua kwamba alitumia mapato ya kilimo kujilipia karo.

Ni mkulima wa mboga pia. Picha/ Sammy Waweru

Miaka miwili baadaye, alihitimu, na kufanya viabarua vya kufunza katika shule za msingi tofauti Murang’a. Bw Maina aliendelea kufanya kilimo.

Mwaka wa 2015, alifanikiwa kuarijiwa na serikali kuu ambapo kufikia sasa anafunza katika shule ya msingi ya Mathareini, iliyoko kaunti ndogo ya Kigumo. Maina 44, anasema laiti angalijua athari za pombe, angaliiacha pindi alipotahadharishwa na baba yake, ambaye wakati mmoja amewahi kuhudumu kama mwalimu.

“Kuvunjika kwa mwiko si mwisho wa mapishi, kuacha pombe ni uamuzi wa kibinafsi na wanaopania kuiasi hawajachelewa kuafikia malengo yao maishani. Ninajivunia uamuzi niliofanya kwa kuwa uliniwezesha kutimiza ndoto zangu kuwa mwalimu,” anaelezea Bw Maina, ambaye ni baba wa watoto wanne.

Kando na kuwa mwalimu, anaendeleza ari yake katika zaraa. Katika kijiji cha Marumi, Kigumo, taswira inayokaribisha katika shamba lake ni rangi ya kijani kibichi cha mimea ainati.

Amelipamba kwa maparachichi yenye soko zaidi nchini aina ya ‘Hass’, matunda ya kuongeza damu mwilini ‘Tree tomato’, kahawa na majani chai. Pia analima kabichi, viazi asili aina ya nduma, sukuma wiki na pilipili mboga.

Kwa upande wake Bw Peter Muhia anasisitiza kwamba ameasi unywaji wa pombe, ikizingatiwa kuwa yeye ni singo fatha, shabaha aliyo nayo ikiwa kujiendeleza kimaisha na kulea mtoto wake kwa msingi wa kumcha Mungu. Anaongeza kuwa, yeye sasa ni ‘balozi’ wa kueneza injili dhidi ya unywaji wa pombe, haswa akilenga vijana.

Aliasi unywaji pombe na sasa anamiliki shamba la viazi vikuu. Picha/ Sammy Waweru

Bw Dayan Masinde, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kifamilia anasema malezi bora kwa watoto ni chanzo cha kuwadhibiti dhidi ya kushiriki maovu, kunywa pombe na hata utumizi wa dawa za kulevya.

“Vijana tunaoshuhudia wakishiriki matendo yasiyofaa, wengi wao hupotoka wakiwa wadogo. Hivyo basi ni jukumu la kila mzazi kuwa makini wawapo wadogo,” anashauri. Anahimiza umuhimu wa kuwatahadharisha kuhusu pombe na dawa za kulevya, kauli inayoungwa mkono na mwalimu Apollo Maina ambaye ni mwasi.

Endapo Peter Muhia angepata wa kumnusuru alipojiingiza katika unywaji wa pombe licha ya kuwa mtoto wa mtaa, huenda pandashuka alizopitia zingeepukika. Hata hivyo, wasemavyo wahenga ‘kuteleza sio kuanguka’ na kwa mujibu wa maelezo ya maisha ya Bw Maina, Muhia ana fursa nyingine kulainisha maisha yake.

You can share this post!

MATATU: Wamiliki waapa kukaidi sheria ya NTSA wakidai...

South B United, Acakoro Ladies ndani ya fainali Chapa Dimba

adminleo