• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Kibarua cha Matiang’i: Mkwaruzano na wanasiasa akikabili maovu

Kibarua cha Matiang’i: Mkwaruzano na wanasiasa akikabili maovu

BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa usalama wa Ndani Fred Matiang’i, amejitokeza kuwa mchapa kazi katika wizara nne alizohudumu tangu alipoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta miaka sita iliyopita.

Msimamo wake mkali na hatua anazochukua zimewafurahisha Wakenya hasa wa kawaida na kuwakasirisha wengine wanaohisi kwamba anawaharibia biashara na hata kuvuka mipaka ya mamlaka yake.

Lakini msimu huu anakabiliwa na kibarua kigumu akisimamia moja ya wizara muhimu zaidi nchini, hali inayomfanya kukwaruzana na watu walio na ushawishi katika nyanja mbali mbali wakiwemo wabunge, mawaziri wenzake, mitandao ya wafanyabiashara, maafisa wa serikali wakiwemo jamaa zao wa karibu na hata wahalifu.

Wakenya wanatazama kuona iwapo atafua dafu katika wizara hii muhimu ambayo ametwikwa jukumu pana la kuhakikisha Wakenya wako salama. Tayari Bw Matiang’ia amekiri ana kibarua kigumu na hata kusema anajua maisha yake na wanaoshirikiana naye yanaweza kuwa hatarini, lakini hatakoma.

Alipotangaza msako wa bidhaa haramu, baadhi ya wabunge walionekana kukereka na wakaanza kudai kwamba Bw Matiang’i ni limbukeni na anasimamia shughuli za serikali kama mwanaharakati.

Kulingana na mbunge wa Kipipiri, Amos Kimunya, mikakati ya Bw Matiang’i ya kupambana na bidhaa za magendo ni hatari kwa uchumi. Alisema Bw Kimunya “amekosa uzoefu wa kazi” na anafanya kazi “kama mwanaharakati” ili kuonekana anafanya kazi kwa bidii. Aliongeza kuwa hakufaa kutangaza hadharani kuwa sukari ina sumu.

Kulingana na ujasusi, biashara ya bidhaa ghushi imesambaa sana katika sekta nyingi za kiuchumi, na ina uwezo hata wa kuangusha serikali.

Jana, kwa mara ya pili, Bw Matiang’i alikosa kufika mbele ya kamati ya pamoja ya bunge kufafanua kuhusu madai ya kuwepo kwa sukari yenye sumu ya Zebaki, hatua ambayo iliwakera wabunge hao.

Ingawa alituma barua kuarifu kwamba alikuwa amebanwa na shughuli katika mkutano wa marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaoendelea katika mkahawa wa Safari Park, Nairobi, wabunge walichukulia kukosa kwake kama kitendo cha madharau na ukaidi.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kukasirika kwa wabunge hakuwezi kumtisha Bw Matiang’i kwa sababu anatekeleza maagizo ya mkubwa wake ambaye ni Rais Uhuru Kenyatta.

Wanaounga mkono utendakazi wa Bw Matiang’i wanasema kuwa vita dhidi ya bidhaa za magendo sio za kubahatisha kwa vile vinashirikishwa kutoka Ikulu na Naibu Mkuu wa Utumishi wa Umma, Wanyama Musiambo kwa maagizo ya rais mwenyewe.

 

Mkwaruzano

“Kwa kutekeleza maagizo kutoka kwa mkubwa wake, ni lazima Bw Matiang’i akwaruzane na watu wengi ambao wanahisi hatua anazochukua ni hatari kwa biashara zao.

Ukweli wa mambo ni kuwa biashara hizi haramu huendeshwa na watu walio na ushawishi wakiwemo wanasiasa, maafisa wa serikali, maafisa wa usalama na washirika wao. Hizi ndizo changamoto ambazo Bw Matiang’i anakabiliana nazo,” anasema afisa mmoja wa usalama ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Alipotangaza msako dhidi ya sukari ya magendo nchini iliyokuwa na sumu, Bw Matiang’i alitofautiana na waziri mwenzake Adan Mohamed ambaye mwanzoni alipuuzilia mbali kauli hiyo.

Hii sio mara ya kwanza Bw Matiang’i kuzima mitandao haramu ambayo imedumu nchini kwa miaka mingi. Akiwa waziri wa elimu, alikabiliana na udanganyifu katika mitihani kwa kubadilisha usimamizi wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) na kuleta mabadiliko makubwa katika usimamizi wa mitihani na sekta ya elimu kwa jumla.

Ukakamavu wake kama waziri mchapa kazi ulianza akiwa Waziri wa Habari na Tekinolojia alipokabiliana na mashirika ya habari yalipotofautiana naye kuhusu mfumo wa kuhama kutoka mawimbi ya analogi hadi dijitali.

Baada ya aliyekuwa Waziri wa Ardhi Charity Ngilu kushurutishwa kujiuzulu kufuatia madai ya ufisadi katika wizara, Bw Matiang’i aliteuliwa kaimu waziri wa wizara hiyo na katika muda mfupi akazima mzozo wa kampuni ya mashamba ya Kiiru Mwiri, Kaunti ya Murang’a ambayo maafisa kadhaa walikuwa wameuawa.

 

Jubilee haina raha

Ishara kwamba utendakazi wa Bw Matiang’i hauwafurahishi hata wabunge wa Jubilee ni hatua ya kiongozi wa wengi Aden Duale ya kumlaumu kwa kutowaandama wanaoingiza bidhaa hiyo nchini huku “akiwahangaisha wauzaji wadogo”.

Kulingana na Bw Duale, mabwenyenye wanaoagiza sukari hiyo kutoka nje ni watu wenye ushawishi na wanalindwa. Naye Kiranja wa Wengi bungeni Benjamin Washiali alisema shughuli za Bw Matiang’i sio muhimu kuliko maisha ya Wakenya yanayohatarishwa na biashara ya sukari yenye madini ya sumu.

Lakini Mbunge wa Aldai Cornelly Serem alidai Dkt Matiang’i alisusia kikao hicho kwa “hofu ya kuulizwa maswali kuhusu madai kuwa jamaa wa Rais Uhuru Kenyatta ni miongoni wa wanaoagiza sukari kutoka nje bila kulipia ushuru”.

“Dkt Matiang’i anaogopa kufika mbele yetu kwa sababu hataki kuulizwa maswali kuhusu kampuni ya Protech Investment Limited inayomilikiwa na mmoja wa jamaa wa Rais.

Lakini ajue kuwa nina stakadhi hapa yenye jina la jamaa huyo ambaye tutataka afike mbele yetu baadaye,” akasema Mbunge huyo wa chama cha Jubilee.

You can share this post!

Ajabu mwanamume kumea uke kwa nyeti zake baada ya kuchepuka

Bidhaa feki huipotezea serikali Sh200 bilioni – Ripoti

adminleo