• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Iniesta nje miezi 4 baada ya kupata jeraha Klabu Bingwa Asia

Iniesta nje miezi 4 baada ya kupata jeraha Klabu Bingwa Asia

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA wa zamani wa klabu ya Barcelona, Andres Iniesta atakuwa katika chumba cha majeruhi miezi minne baada ya kujeruhiwa mguu akipeperusha bendera ya Vissel Kobe kwenye Klabu Bingwa bara Asia.

Kobe imethibitisha Desemba 16 kuingia mkekani kwa kiungo huyo mbunifu ikisema, “Iniesta, 36, alifanyiwa upasuaji uliokamilika vyema mjini Barcelona.”

Iniesta alipata hilo katika mechi ya robo-fainali dhidi ya Suwon Samsung Bluewings kutoka Korea Kusini ambayo Kobe ilishinda kwa njia ya penalti 7-6 mnamo Desemba 10. Mhispania huyo alikosa mechi ya nusu-fainali dhidi ya Ulsan Hyundai ambayo timu hiyo kutoka Korea Kusini ilishinda 2-1 katika muda wa ziada mjini Doha nchini Qatar.

Katika taarifa kwenye mtandao wake wa Instagram iliyoandamana na picha yake akiwa amelazwa hospitalini, Iniesta alithibitisha alivunjika mfupa wa “rectus femoris” kwenye mguu wake wa kulia.

“Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa jeraha hili mara kadhaa, niliamua kufuata ushauri wa kundi langu la madaktari na tuliamua kuwa njia ya pekee ilikuwa kufanyiwa upasuaji na kuharakisha kupata nafuu tena.

“Upasuaji ulikamilika salama na ninahisi vizuri sana.”

Msimu huu, Iniesta, ambaye anapokea mshahara wa juu kuliko wote Ligi Kuu Japan (Sh35 bilioni kila mwaka), amechezea Kobe mechi 26 na kufunga mabao manne pamoja na kuchangia pasi sita zilizozalisha mabao.

  • Tags

You can share this post!

Maraga afichua jinsi alivyotishwa mara kadha

Watu wachache kualikwa kuhudhuria hafla ya Biden kuapishwa