• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Peru wakung’uta Colombia huku Ecuador na Venezuela wakitoshana nguvu Copa America

Peru wakung’uta Colombia huku Ecuador na Venezuela wakitoshana nguvu Copa America

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

TIMU ya taifa ya Peru iliweka hai matumaini ya kuingia robo-fainali za Copa America baada ya kuvuna ushindi wa 2-1 dhidi ya Colombia katika mechi ya Kundi B mnamo Jumatatu.

Peru sasa wanajivunia alama tatu na wanashikilia nafasi ya tatu katika kundi hilo linaloongozwa na wenyeji Brazil kwa pointi sita.Kwa upande wao, Colombia wanakamata nafasi ya pili kwa pointi nne, mbili zaidi kuliko Ecuador walioambulia sare ya 2-2 dhidi ya Venezuela katika gozi jingine la Kundi B.

Jumla ya vikosi vinne miongoni mwa vitano vinavyounga Kundi B na vinne vingine kutoka Kundi A linaloongozwa na Argentina kwa alama nne kufikia sasa, vitafuzu kwa hatua ya nane-bora.

“Ushindi dhidi ya Colombia unatupa tumaini kubwa. Naamini kuanzia sasa kusonga mbele, motisha itakuwa ya juu zaidi kadri tunavyojiandaa kupepetana na Ecuador na Venezuela katika michuano miwili ijayo kundini,” akasema beki Renato Tapia.

Chini ya kocha Ricardo Gareca, Peru walifungua makala ya 47 ya Copa America kwa kupokezwa kichapo kinono cha 4-0 kutoka kwa mabingwa watetezi Brazil mnamo Juni 18. Mabao yao dhidi ya Colombia yalipachikwa wavuni kupitia Sergio Pena na beki wa Everton, Yerry Mina aliyejifunga.

Colombia waliojutia masihara makubwa ya kipa David Ospina, walifutiwa machozi na Miguel Borja. Kikosi hicho cha mkufunzi Reinaldo Rueda kilisajili ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Ecuador mnamo Juni 14 kabla ya Venezuela kuwalazimishia sare tasa siku tatu baadaye.

“Hatukujituma ipasavyo. Tulisuasua katika vipindi vyote viwili vya mchezo na makosa yaliyofanywa na kila idara uwanjani yalikuwa mengi. Itatulazimu kujinyanyua haraka kabla ya mechi ijayo,” akasema kiungo mkabaji wa Colombia Wilmar Barrios.

Colombia ambao wanakosa maarifa ya kiungo tegemeo James Rodriguez aliyetemwa kikosini na kocha Rueda, watafunga kampeni zao za Kundi B dhidi ya Brazil usiku wa Jumatano jijini Rio de Janeiro.Sare dhidi ya Ecuador iliwasaza Ecuador na alama mbili kutokana na mechi tatu za hatua ya makundi.

Kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne mbele ya Ecuador ambao wana alama moja kutokana na mechi mbili.Venezuela walipigwa na Brazil 3-0 katika mechi ya kwanza kabla ya kuokota alama moja katika sare tasa dhidi ya Colombia mnamo Juni 18.

Watacheza na Peru katika mechi ya mwisho kundini mnamo Jumatatu ijayo.Ecuador kwa upande wao watapimana ubabe na Peru mnamo usiku wa Jumatano kabla ya kushuka dimbani kuonana na Brazil mnamo Juni 28.

 

  • Tags

You can share this post!

Ndoa ya Jubilee na ODM yapigwa mawe

ManCity wamtia Harry Kane wa Tottenham mtegoni