• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Mawaziri wapya wahimizwa kuzingatia usawa kwenye utendakazi

Mawaziri wapya wahimizwa kuzingatia usawa kwenye utendakazi

Mwanahabari wa zamani wa runinga ya Citizen Bi Farida Karoney ambaye ndiye Waziri mpya wa Ardhi na Mipango ya Miji. Picha/ Hisani

 

Na CHARLES WASONGA
MAWAZIRI wapya wametakiwa kuwahudumia Wakenya kutoka pembe zote za Kenya bila kuzingatia ukabila, maeneo au mirengo ya kisiasa wanayounga mkono.
Mbunge wa Yatta Bw Charles Kilonzo pia aliwashauri kuepukana na mwenendo wa zamani ambapo mawaziri walikuwa wakiwateua watu kutoka makabila yao katika Mashirika ya Serikali yaliyoko katika wizara zao bila kuzingatia taratibu zilizowekwa katika utumishi wa umma.
“Nawaunga mkono mawaziri hawa wote kwani wanafaa kwa wizara ambazo Rais aliwateua kuhudumu. Lakini wanafaa kutambua kwamba wao ni watumisha wa Wakenya wote na ni wajibu wao kuwahudumia bila mapendeleo kwa misingi yoyote ile ikiwemo siasa,” akasema.
Bw Kilonzo ambaye ni mbunge alichaguliwa bila udhamini wa chama cha kisiasa, vile vile aliwaonya mawaziri hao kwamba bunge litapendekeza wafutwe kazi endapo hawatatekeleza majukumu yao ipasavyo au kujihusisha na ufisadi.
Kuwang’oa ofisini
“Endapo utendakazi wenu hautaridhisha bila shaka bunge hilo ambalo linawaidhinisha halitasita kuwaondoa afisini. Kwani hivyo, nawaomba mawaziri hawa tisa kufanya kazi nzuri ya utumishi kwa wote,” akasema Bw Kilonzo.
Mbunge huyo alisema hayo alipokuwa akichangia mjadala kuhusu ripoti ya kamati ya kuhusu uteuzi ambayo iliidhinisha majina ya mawaziri hao wateule.
Wale walioidhinishwa ni; Profesa Margaret Kamar kama Waziri wa Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia, John Munyes (Mafuta na Madini), Balozi Monica Juma (Mashauri ya Kigeni), Farida Karoney (Ardhi na Mipango ya Miji) na Peter Munya (Afrika Mashariki).
Wengine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Keriako Tobiko (Mazingira na Misitu), Simon Chelugui (Maji na Usafi), Ukur Yatani (Leba) na Rashid Echesa Muhamed (Michezo na Utamaduni).
Wakichangia mjadala huo, wabunge wa Jubilee waliwaunga mkono tisa hao wakiwataja kama wanaume na wanawake ambao wana uwezo wa kuisaidia Jubilee kutekeleza nguzo nne za maendeleo zilizoko kwenye manifesto yao.

You can share this post!

Kenya yashuka hadi nafasi ya 106 viwango vya FIFA

Waziri Echesa ashauriwa arudi shuleni kunoa maarifa

adminleo