• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
Bara la Afrika lalala huku dunia ikianzisha chanjo ya corona

Bara la Afrika lalala huku dunia ikianzisha chanjo ya corona

LEONARD ONYANGO na MASHIRIKA

NCHI za Afrika zimo hatarini kubaki nyuma katika vita dhidi ya virusi vya corona wakati mataifa mengine yakipiga hatua kubwa kuwapa raia wao chanjo ya kuzima maambukizi.

Kufikia jana, mamilioni ya watu katika mataifa ya nje ya bara la Afrika walikuwa wamepewa chanjo, huku nchi za barani zikiendelea kujikokota.Waziri wa Afya Mutahi Kagwe wiki iliyopita alitangaza kuwa chanjo ya corona itatolewa bure itakapowasili humu nchini.

Lakini Bw Kagwe hajasema ni lini chanjo hiyo itakapofika humu nchini.Kenya imeagiza chanjo hiyo kupitia muungano wa kimataifa kuhusu chanjo (Gavi).

Muungano wa Gavi unalenga kusaidia nchi maskini kupata chanjo ya corona kwa bei nafuu. Hata hivyo, chanjo inayoletwa na Gavi itatumika kuchanja asilimia 20 tu ya Wakenya.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kudhibiti Maradhi (CDC) ulionyesha kuwa asilimia 75 ya Waafrika watakubali kupewa chanjo iwapo itathibitishwa kuwa salama.

Huku mataifa ya Afrika yakiendelea kungojea chanjo, mataifa tajiri duniani yanaendelea kutoa kinga kwa mamilioni ya raia wayo.

Nchi tajiri tayari zimeagiza dozi bilioni 9 za chanjo ambazo zimetengenezewa katika mataifa ya Magharibi na kuacha Afrika katika hali ya sintofahamu. Hiyo inamaanisha kwamba kiasi kikubwa cha chanjo itakayotengenezwa mwaka ujao kitachukuliwa na nchi tajiri.

Nchini Amerika, zaidi ya watu milioni mbili kati ya watu milioni 331 tayari wamepata chanjo hiyo. Serikali ililenga kuhakikisha kuwa watu milioni 20 wanapewa chanjo hiyo kufikia Ijumaa, wiki hii.

Visa zaidi ya 19.2 milioni vya watu walioambukizwa na virusi vya corona vimethibitishwa nchini Amerika tangu Januari mwaka huu.Umoja wa Mataifa ya Ulaya (EU) umeanza harakati za kuhakikisha kuwa watu milioni 446 wanapewa chanjo hiyo katika nchi zote 27 wanachama.Mamlaka ya Matibabu ya Ulaya (EMA) imeidhinisha matumizi ya chanjo iliyotengenezwa na Pfizer-BioNTech ya Amerika.

Rais wa Tume ya EU Ursula von der Leyen jana alisema kuwa chanjo hiyo imesambazwa katika mataifa yote ya Ulaya. Watu 800,000 tayari wamepewa chanjo ya corona nchini Uingereza.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw Boris Johnson alisema kuwa watu milioni 15 ambao wanastahili kupata chanjo hiyo kwa dharura wametambuliwa.

Uingereza imekuwa ikitumia chanjo ya Pfizer lakini serikali imesema kuwa itazindua matumizi ya chanjo ya pili iliyotengenezwa na AstraZeneca kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza.Uingereza inalenga kutoa chanjo kwa raia wake milioni 2 ndani ya wiki mbili zijazo.

Wataalamu wanasema kuwa huenda mataifa ya Afrika ambayo yameshindwa kupata chanjo iliyotengenezwa katika nchi za Magharibi, yatalazimika kutumia chanjo ya China.

China ina chanjo sita ambazo zinafanyiwa majaribio ya mwisho. Rais Xi Jinping ametangaza kuwa China itatengeneza jumla ya dozi bilioni 1 mwaka ujao. Taifa la Bahrain na Milki za Uarabuni (UAE) tayari zimeagiza chanjo ya corona kutoka China.

Morocco pia inalenga kutumia chanjo ya China kuanzia mwezi ujao. Mataifa ya Uturuki, Indonesia na Brazil tayari yameanza mchakato wa kuidhinisha chanjo ya China.Majaribio ya kuthibitisha usalama wa chanjo ya China pia yanaendelea nchini Urusi, Misri na Mexico.

You can share this post!

Daktari akana kunyemelea na kubaka mwanafunzi

Makanisa yaililia serikali kuyaruhusu kuandaa kesha za...