• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:58 PM
Maandalizi duni shule zikifunguliwa kesho

Maandalizi duni shule zikifunguliwa kesho

WINNIE ATIENO na FAITH NYAMAI

HATIMAYE wanafunzi wanarejea shuleni Jumatatu baada ya miezi tisa huku shule nyingi za umma zikianza maandalizi ya dakika za mwisho kuzingatia kanuni za Wizara ya Afya za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Katika shule nyingi, hali ya madarasa ni mbovu, hakuna madawati ya kutosha, maji, vyoo na mabweni licha ya Waziri wa Elimu Profesa George Magoha kusisitiza kwamba shule zitafunguliwa serikali ilivyotangaza.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya elimu nchini, wanafunzi, walimu na wazazi wanajiandaa kwa hali ngumu shule zikitekeleza masharti hayo makali.

Jumamosi, Prof Magoha alionya walimu wakuu dhidi ya kulazimisha wanafunzi kubeba sanitaiza zao binafsi, kuongeza karo au kununua maski zinazotumiwa na matabibu akisema watakaokiuka maagizo hayo watachukuliwa hatua.

Prof Magoha alisema serikali inatarajia shule kununua sabuni na sanitaiza na kuziweka maeneo maalumu iliwanafunzi kunawa mikono licha ya taasisi hizo kukumbwa na changamoto za pesa.

“Shule zinazowataka wanafunzi kubeba sanitaiza zao zinafaa kukoma,” alisema katika shule ya upili ya Kibera alipopokea madawati na viti.

Alisema hayo huku wazazi wengi wakikosa nafasi za shule kwa watoto wao. Wazazi walisema shule za kibinafsi ambamo watoto wao walikuwa wakisomea zilifungwa na wamekosa nafasi katika shule za umma.

Hata hivyo, wazazi wengine walidai wanashurutishwa kutoa hongo ili wapewe nafasi.

Shule zote zilifungwa Machi kutokana na janga la corona. Hata hivyo, shule nyingi za kibinafsi zimeshindwa kufungua wakurugenzi wakidai ni kutokana na ukosefu wa fedha za kuendesha biashara hizo.

Wazazi hao sasa wanamtaka Prof Magoha kuingilia kati suala hilo wakidai wanatozwa kati ya Sh5,000 shule za msingi hadi Sh10,000 kwa shule za upili.

“Profesa Magoha alituhakikishia kuwa wanafunzi wote watapata nafasi lakini mambo ni tofauti. Nina watoto wanne na mmoja tu ndio amepata nafasi katika shule moja ya msingi Mombasa. Sijui nitakakopeleka watoto wengine,” alisema Bw Richard Odera.

Bw Odera alielezea namna mwalimu mkuu alimwambia atoe pesa ili watoto wake wapate nafasi.

  • Tags

You can share this post!

Vijana wamzuia Gideon kupokea baraka

Cotu yapinga kuongezwa kwa ushuru wa mapato