• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:04 PM
Shevchenko, Allegri pazuri zaidi kutua Chelea endapo kocha Frank Lampard atatimuliwa

Shevchenko, Allegri pazuri zaidi kutua Chelea endapo kocha Frank Lampard atatimuliwa

Na MASHIRIKA

CHELSEA wamefichua mpango wa kumwajiri mwanasoka wao mwingine wa zamani Andriy Shevchenko kuwa kocha iwapo matokeo yao yatazidi kudorora chini ya mkufunzi wa sasa Frank Lampard.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, Lampard kwa sasa yuko katika hatari ya kutimuliwa ugani Stamford Bridge baada ya kushinda mechi moja pekee kati ya saba zilizopita ikiwemo ile iliyowashuhudia wakipokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Manchester City mnamo Januari 3, 2021.

Ingawa hivyo, gazeti la SunSport limeshikilia kwamba Lampard huenda akapewa mechi chache zijazo kujinyanyua la sivyo, apigwe kalamu ikizingatiwa historia ya Roman Abramovich, bwanyenye mmiliki wa Chelsea aliye mwepesi wa kutimua makocha pindi kikosi kinapoanza kusuasua.

Baada ya kuvaana na Morecambe katika raundi ya tatu ya Kombe la FA mwishoni mwa wiki hii, Lampard aliyechezea Chelsea kwa miaka 13, atakuwa na presha ya kuongoza masogora wake kusajili ushindi dhidi ya Fulham ugenini kabla ya kuwaendea Leicester City uwanjani King Power kisha kualika Wolves ugani Stamford Bridge katika EPL.

Iwapo Chelsea hawatajinyanyua kutokana na mechi hizo, gazeti la Le10Sport limesisitiza kwamba Lampard atafutwa na nafasi yake kutwaliwa na Shevchenko ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Ukraine tangu 2016.

Japo hajawahi kudhibiti mikoba ya kikosi kingine hata katika ngazi ya klabu, Shevchenko ameongoza waajiri wake kushinda mechi 21 kati ya 40 alizosimamia. Hivi majuzi, aliongoza Ukraine kufuzu kwa fainali za Euro 2020 baada ya kudhibiti kilele cha kundi lao lililojumuisha pia mabingwa watetezi, Ureno.

Ingawa Shevchenko hakung’aa sana kambini mwa Chelsea akiwa mchezaji, aliondoka ugani Stamford Bridge miaka 11 iliyopita akiwa kipenzi cha Abramovich aliyemnunua kwa kima cha Sh4.2 bilioni kutoka AC Milan mnamo 2006. Akivalia jezi za Chelsea, fowadi huyo alifunga mabao 22 pekee kutokana na mechi 77.

Mtoto wa Shevchenko aitwaye Kristian, 14, alizaliwa Uingereza na kwa sasa anachezea akademia ya Chelsea. Kwa mujibu wa gazeti la ‘The Athletic’ nchini Uingereza, Chelsea watapania pia kuajiri kocha wa zamani wa AC Milan na Juventus, Massimiliano Allegri iwapo Bodi ya Usimamizi itahisi kwamba Shevchenko hana tajriba ya kutosha kuwashindia taji la EPL na kuwapigisha hatua kwenye soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Allegri ambaye ni raia wa Italia, alifurushwa na Juventus mnamo 2019 licha ya kuongoza kikosi hicho kutia kapuni mataji matano mfululizo ya Ligi Kuu ya Serie A.

Wakufunzi wengine wanaohusishwa na mikoba ya Chelsea ni nahodha wao wa zamani John Terry ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi kambini mwa Aston Villa, Thomas Tuchel aliyeagana na PSG mwishoni mwa 2020, Lucien Favre aliyetimuliwa majuzi na Borussia Dortmund pamoja na Julian Nagelsmann wa RB Leipzig nchini Ujerumani.

Kichapo kutoka kwa Man-City kiliwatupa Chelsea hadi nafasi ya nane kwenye jedwali la EPL kwa alama 26 sawa na Aston Villa na West Ham United wanaofunga mduara wa 10-bora.

Ni pengo la pointi tatu pekee linalowatenganisha Chelsea kwa sasa na Arsenal ambao hivi majuzi, walikuwa wakihusishwa na uwezekano wa kuteremshwa daraja katika EPL mwishoni mwa muhula huu kutokana na msururu wa matokeo duni chini ya kocha Mikel Arteta.

Kwa mujibu wa The Athletic, kiini cha kushuka kwa makali ya Chelsea ni manung’uniko miongoni mwa wanasoka wazoefu wanaohisi kupuuzwa na Lampard huku baadhi ya sajili wapya wakiwajibishwa mara kwa mara licha ya makali yao kupungua.

“Bodi ya Chelsea huenda isimstahimili Lampard kwa muda mrefu. Wapo wachezaji ambao wamekuwa wakipata nafasi katika kikosi cha kwanza mara kwa mara licha ya ubora wao kudidimia. Hatua hiyo imetishia kusambaratisha uthabiti uliojivuniwa na kikosi mwanzoni mwa msimu,” likasema gazeti hilo kwa kumrejelea mafowadi Timo Werner na Kai Havertz.

Werner na Havertz wamekuwa wakipoteza nafasi nyingi za wazi katika takriban kila mchuano huku Olivier Giroud na Tammy Abraham wanaojivunia fomu nzuri wakisazwa benchi.

Chelsea walipigiwa upatu kuwa miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la EPL na ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu wa 2020-21 baada ya kufungulia mfereji wao wa fedha na kuweka mezani kima cha Sh30 bilioni kwa minajili ya huduma za wachezaji Thiago Silva (PSG), Malang Sarr (Nice), Ben Chilwell (Leicester City), Hakim Ziyech (Ajax), Werner (RB Leipzig), Havertz (Bayer Leverkusen) na Edouard Mendy (Rennes).

“Hawa ni wachezaji nyota wanaohitaji muda zaidi ili kuoanisha mitindo ya kucheza kwao. Nafahamu presha iliyopo. Kufutwa kazi katika ulingo wa ukocha ni rahisi japo kwa sasa sitaki kuanza kufikiria jinsi waajiri wangu wanavyofikiria kunihusu na kuhusu matokeo ya kikosi,” akasema Lampard huku akitaka usimamizi wa Chelsea na mashabiki wa kikosi hicho kuvuta subira zaidi kabla ya matunda ya juhudi zake za kukisuka upya kikosi kuanza kuonekana.

Chelsea waliotawazwa mabingwa wa EPL mara ya mwisho mnamo 2016-17, wamepoteza mechi nne kati ya sita zilizopita huku wakishinda michuano miwili pekee ligini tangu mwanzoni mwa Disemba 2020.

Kichapo cha 1-0 ambacho Chelsea walipokezwa na Everton mnamo Disemba 12 ugani Goodison Park kilipiga breki rekodi ya kutoshindwa katika mechi 17 ambayo awali iliibua gumzo la Chelsea kuhusishwa na uwezekano mkubwa wa kutwaa ufalme wa EPL muhula huu.

Baadhi ya wakufunzi ambao Chelsea imewahi kuwatimua awali kutokana na matokeo duni ni Avram Grant, Luiz Felipe Scolari, Guus Hiddink, Roberto Di Matteo na Andre Villas-Boas. Wengine ni Claudio Ranieri, Carlo Ancelotti, Rafael Benitez, Jose Mourinho, Antonio Conte na Maurizio Sarri.

You can share this post!

Mbunge ataka wakazi Buxton wahusishwe kikamilifu katika...

Mwanasoka wa zamani wa Man-United, Darren Fletcher, arejea...