• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
Hyvin Kiyeng kuhamia mbio za mita 10,000 na marathon

Hyvin Kiyeng kuhamia mbio za mita 10,000 na marathon

Na CHRIS ADUNGO

MSHINDI wa nishani ya fedha katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Olimpiki, Hyvin Jepkemoi Kiyeng, amefichua mpango wa kujitosa katika mbio za mita 10,000 na marathon baada ya kukamilika kwa Michezo ya Olimpiki jijini Tokyo, Japan mnamo 2021.

Kiyeng amejivunia mataji mengi ya haiba katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji tangu ajitose kwenye fani hiyo mnamo 2011.

Nyota ya Kiyeng ambaye ni afisa wa Idara ya Huduma kwa Polisi (NPS), ilianza kung’aa katika mbio hizo kwenye ulingo wa kimataifa mnamo 2011 alipoibuka mshindi wa Michezo ya Afrika jijini Maputo, Msumbuji kabla ya kutia kapuni medali ya shaba katika mbio za Mataifa Bingwa Afrika mwaka mmoja baadaye.

Kiyeng alitwaa nishani ya dhahabu katika Riadha za Dunia mnamo 2015 jijini Beijing, China kabla ya kujizolea medali ya shaba mnamo 2017 jijini London, Uingereza mwaka mmoja baada ya kushinda nishani ya fedha kwenye Olimpiki za Rio, Brazil mnamo 2016.

Kiyeng pia alishiriki Riadha za Dunia mnamo 2013 nchini Moscow ila akaambulia nafasi ya sita kabla ya kutupwa hadi nafasi ya nane kwenye Riadha za Dunia za 2019 jijini Doha, Qatar.

Alikamilisha Mbio za Nyika za Dunia jijini Kampala, Uganda mnamo 2017 katika nafasi ya nne baada ya kushikilia tena nafasi hiyo kwenye Michezo ya Afrika katika mbio za mita 5,000 mnamo 2011.

Baada ya Olimpiki za Tokyo mwaka huu 2021, Kiyeng amesema atapania kuzungumzia kocha na usimamizi wake, Global Sports Communication, kuhusu jinsi ya kumsaidia kuhamia hadi kwenye fani ya mbio za masafa marefu kuanzia kilomita 10.

Hata hivyo, amesisitiza kwamba kwa sasa maazimio yake ni kujiandaa vilivyo kwa michezo ijayo ya Olimpiki ambapo analenga kutwaa nishani ya dhahabu baada ya kuambulia nafasi ya pili miaka minne iliyopita nchini Brazil.

You can share this post!

Natembeya awataka machifu Nakuru wawatafute na kuwarejesha...

Gor Mahia waaga CAF Champions League baada ya kupokezwa...