TAHARIRI: Walimu ndio kinga yetu dhidi ya corona shuleni

KITENGO CHA UHARIRI

BAADA ya likizo ya zaidi ya miezi tisa, hatimaye shule zimefunguliwa na wanafunzi kurejelea masomo.

Kufunguliwa kwa shule kumekuwa chanzo cha afueni kuu kwa wengi wa wadau katika sekta ya elimu japo kwa wakati huo huo kumezua hofu kubwa miongoni mwa wengine.

Mwanzo kabisa lazima tuungame kwamba sawa na sekta nyinginezo, janga la corona limekuwa pigo kubwa kwa taifa na dunia. Madhara ya gonjwa hili kwa afya na uchumi hayana kifani.

Kwa upande wake, sekta ya elimu haikusazwa. Ililemazwa kabisa tangu mlipuko wa corona ulipotokea nchini. Hata hivyo, kadri ya mpito wa wakati sekta nyinginezo zilianza kurejelea shughuli zake japo taratibu. Ya mwisho ikawa ni elimu. Afya ya watoto wetu ilikuwa muhimu zaidi na ndiyo sababu ya kuwa ya mwisho.

Maadamu imebainika kwamba kufikia sasa ni watu wazima tena wenye maradhi kama vile shinikizo la damu pamoja na kisukari ndio walio katika hatari kubwa ya kuangamizwa na maradhi ya Covid-19, na kwamba watoto hawako katika hatari kubwa sana, basi tunafaa kuchukua tahadhari mpya wakati huu ambapo shule zimefunguliwa.

Tangu Jumatatu shule zilipofunguliwa tumesikia habari kadha ambazo zinafaa kututia hofu. Kumekuwepo na visa ambapo wanafunzi wanashindwa kustahimili kuvaa barakoa kwa muda mrefu, hatua inayowalazimu kuzivua. Wanapozivua wanatangamana bila kujali. Wengine wamekuwa wakibadilishana barakoa zao bila kujali. Aidha, tumesikia habari za baadhi ya wanafunzi hasa wa madarasa ya chini wakiramba pipi au peremende moja kwa zamu bila kutilia maanani hatari inayotokana na mwenendo huu.

Ukizingatia athari za matukio yaliyoripotiwa shuleni katika hizi siku chache za ufunguzi, basi sisi sote tuna kila sababu ya kuingiwa na hofu. Kuna hatari ya kutokea mlipuko hatari wa corona ambao kiini chake kitakuwa wanafunzi shuleni.

Ni kwa mantiki hii ambapo kunafaa kuchukuliwe hatua za dharura kuepuka kutosa taifa katika janga jipya ambalo huenda likaleta maafa na madhara mengine makubwa ya kiuchumi.

Walimu ambao ndio waangalizi wa wanafunzi wawapo shuleni wanafaa kuchukua hatua mara moja kuwaelekeza na kuwafuatilia wanafunzi ili kuhakikisha kwamba wanazingatia maelekezo ya wizara ya Afya katika juhudi ya kudhibiti ugonjwa wa corona. Hatua zisipochukuliwa basi huenda watoto wakawasambazia wazazi wao ugonjwa huu na kuchangia vifo vya baadhi yao.

Habari zinazohusiana na hii