Mwanamke amlilia Raila mumewe asiwalaani

Na MWANGI MUIRURI

MWANAMKE mmoja Kaunti ya Murang’a, anaomba kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga kumtembelea katika boma lake ili kuepushia familia yake laana baada ya mumewe kujitengenezea kaburi atakalozikwa akifariki.

Bi Jane Wanjira, 69, anataka Bw Odinga amshawishi mumewe, Samuel Karanja abadilishe nia na kuachana na mipango yake.Bw Karanja amejenga kaburi atakalozikwa akisema familia yake yote itapata laana ikikosa kutimiza mapenzi yake.

Lakini familia inasema itakuwa vigumu kutimiza takwa lake atakapofariki kwa sababu kaburi ni chumba alichojenga hatua chache kutoka kwa nyumba yake katika kijiji cha Mbombo, eneobunge la Kiharu.  Karanja amesisitiza kuwa akifariki, mwili wake unafaa kulazwa kwenye kitanda na kufungiwa ndani ya kaburi hilo.

Hata hivyo, alisema ni mwanamume mmoja pekee, Raila Odinga, anayeweza kumfanya afute laana kwa familia asipolazwa kwenye kaburi alilojenga.Anasema kwamba amekuwa akimpigia kura Bw Odinga mara nne ambayo waziri huyo mkuu wa zamani amegombea urais.

Bi Wanjira anasema tabia za mumewe zinashtua na kutisha hasa kwa kuwa laana ya kiongozi wa familia sio mzaha katika tamaduni za jamii yao na inaweza kumaliza familia yote.Bw Karanja, 75, alithibitishia Taifa Jumapili kwamba ni Bw Odinga anayeweza kumshawishi abadilishe matakwa aliyoagiza familia itimize akifariki.

Alisema akifariki anafaa kuzikwa alivyoagiza na kwamba ana akili timamu tofauti na watu wanavyofikiria.Mwalimu huyo aliyestaafu 2001, anasema anaamini kwamba nambari yake ya bahati ni saba na tarehe yake ya kufa na siku yake ya kuzikwa inafaa kuwa na herufi hiyo iwe katika mwezi au mwaka.

Bw Karanja alizaliwa Agosti 27 1947, alipata mafunzo ya ualimu katika chuo cha Thogoto Teachers Training College kati ya 1967 na 68 na aliajiriwa 1969. Anasema anampenda Bw Odinga kwa sababu “baba ni shujaa wa siasa zetu.”

Bw Karanja anasisitiza kwamba anadai serikali malimbikizi ya pensheni kutoka kwa mkataba wa maelewano (CBA) kati ya chama cha walimu cha (Knut) na Tume ya Huduma ya Walimu wa mwaka wa (TSC) wa mwaka wa 2003.

Anasema kwamba anataka Bw Odinga kuwa rais ili aweze kurekebisha dhuluma aliyotendewa kwa kutolipwa pensheni hiyo yote. “Nilikuwa na matumaini kwamba Bw Odinga angekuwa rais ili anilipe pesa zangu, walimuibia kura 2007, 2013 na 2017 na nikakosa imani angeniokoa. Nilitamani kufariki Julai 2018 lakini akasalimiana na Uhuru Kenyatta na nikaambia Mungu aahirishe kifo changu,” alisema.

Ingawa maafisa wa afya wanasema kaburi lake halijatimiza viwango vya afya ya umma, anasisitiza kwa mkewe, watoto wake watatu na wajukuu wanne watapata laana iwapo hawatamzika humo na Bw Odinga anayeweza kumshawishi abadilishe nia.

Habari zinazohusiana na hii

ODM: Raila anachezwa

Kingi amzima Raila

Kichwa kinauma

Raila akausha marafiki

Watamjaribu Baba?