• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:09 AM
Malala na Oparanya wazozania kura ya Matungu

Malala na Oparanya wazozania kura ya Matungu

Na SHABAN MAKOKHA

MGOGORO mkali wa kisiasa unatokota katika Kaunti ya Kakamega kati ya Gavana Wycliffe Oparanya na Seneta wa kaunti hiyo Cleophas Malala.

Bw Malala anamshutumu gavana huyo dhidi ya kutumia rasilimali za umma kumfanyia kampeni mgombea wa ODM, David Were, katika uchaguzi mdogo wa kuwania kiti cha ubunge cha Matungu.

Seneta huyo amedai kwamba Bw Oparanya amekuwa akikiuka sheria za uchaguzi na kutoa wito kwa Tume ya Kukabiliana na Ufisadi (EACC) na Mkurugenzi mkuu wa Uchunguzi wa Uhalifu (DPP) kuwa waangalifu kuhusu matumizi mabaya ya rasilimali za umma wakati wa shughuli za uchaguzi.

Isitoshe, Bw Malala amelaumu uongozi wa Kaunti kwa kuwatia woga wafanyakazi katika serikali ya kaunti hiyo wanaoishi eneo hilo kwa kutishia kuwaachisha kazi endapo watakosa kumuunga mkono na kumpigia kura mgombea wa ODM.

Katika mkutano wa kisiasa katika chuo cha kiufundi cha Kholera, eneo la Matungu wiki iliyopita, diwani wa Wadi ya Mayoni Libinus Oduor alitangaza kwamba mfanyakazi yeyote kutoka eneo hilo ambaye hatampigia kura Bw Were atafutwa kazi.

Bw Oduor alidai kaunti hiyo, hapo Machi 4, itawatuma maajenti kisiri katika vituo vya kupigia kura kufuatilia jinsi waajiriwa wote kutoka Matungu watakavyopiga kura.

“Watakaowapigia kura wagombea wengine wataachishwa kazi ili watafute usaidizi kutoka kwa mtu watakayemchagua,” alisema Bw Oduor.

Watu kadhaa kutoka viwango vyote vya wadi wameajiriwa katika serikali ya kaunti hiyo kuanzia wasimamizi wa kaunti hadi kazi mashinani, makundi ya vijana na wanawake, utendakazi wa kaunti, walimu katika shule za chekechea na kundi jipya la baraza la wazee.

Taarifa kutoka kwa Bw Oduor imeibua maswali tele mashinani huku wakazi wakiuliza ni kwa nini waajiriwa wa kaunti wanapaswa kupatiwa vitisho vya kuadhibiwa vikali iwapo watakosa kumchagua Bw Were katika uchaguzi mdogo ujao.

“Serikali ya kaunti hutumia fedha zinazotoka kwetu. Licha ya gavana kuwa mwanachama wa ODM, raslimali anazofurahia zinatoka kwa watu wote wa Kakamega. Aache kutia doa utawala wake kwa sababu ya Bw Were,” alisema Bw Peter Amunga, mkazi eneo hilo, akihoji kwamba vitisho kutoka kwa serikali ya kaunti vinawanyima wakazi uhuru wa kuchagua.

You can share this post!

Mwanamke amlilia Raila mumewe asiwalaani

Serikali yamrukia gavana kuhusu usalama