• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MWISHO WA GIZA!

MWISHO WA GIZA!

NA WAANDISHI WETU

RAIS anayeondoka wa Amerika Donald Trump ameingia katika historia ya Amerika kama rais pekee aliyepigiwa kura ya kutimuliwa na bunge mara mbili, mbali na kuwa wa pekee katika siku za majuzi kukataa kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa mrithi wake.

Kiongozi huyo aliyechaguliwa 2016, ameacha Amerika ikiwa inayumbayumba na kudhoofika kiuchumi, kidiplomasia na migawanyiko ya kikabila.

Katika utawala wake wa miaka minne, mfanyibiashara huyo, ambaye wakati mmoja alikuwa ‘celeb’ wa televisheni, alitumia vitisho, kugawanya watu, kudharau taasisi na kusisitiza kupewa uaminifu na wote.

Yeyote aliyejaribu kutofautiana naye alifutwa kazi ama kutukanwa hadharani na rais huyo aliyekuwa mzushi ajabu. Alivuruga pia uhusiano kati ya Amerika na mataifa ya kigeni wakiwemo washirika wake wa karibu, akataja mataifa ya Afrika kama yanayofanana na mashimo ya choo, akadunisha Waislamu na watu weusi, wanawake miongoni mwa wengine.

Alizozana na China kipindi chake chote madarakani, akaondoa Amerika katika shirika la afya la WHO na mikataba kadhaa ya kimataifa, akadunisha muungano wa NATO, uhusiano wake na marafiki wa Uropa ukaingia baridi, akavuruga mkataba wa nyuklia na Iran miongoni mwa masihala mengine ya kidiplomasia.

Hata hivyo alipendelea Israeli na kulazimisha mataifa kadhaa kuanza uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo ya Mashariki ya kati.

MCHOCHEZI SUGU

Trump pia alifanikiwa kuchochea hisia kali za ubaguzi wa rangi hasa miongoni mwa wazungu wenye misimamo mikali.Kiongozi huyo alivunja mtindo wa marais wa Amerika kuzungumza na raia wao na ulimwengu kwa jumla kwa kugeukia mtandao wa Twitter kama njia yake kuu ya mawasiliano.

Hakusita kuwatisha wakosoaji wake mitandaoni kwa matusi na kuwadhalalisha wakiwemo raia wa kawaida hadi marais wa mataifa mengine. Mtindo huo ulimwezesha kupata ufuasi wa watu zaidi ya milioni 88 wengi wao wakiwa wenye misimamo mikali.

Alitumia Twitter pia kuwafuta kazi maafisa wake akiwemo aliyekuwa waziri wa mashauri ya kigeni Rex Tillerson na mwenzake wa ulinzi, Mark Esper.Lakini katika siku zake za mwisho madarakani, akaunti zake za Twitter, Facebook na Instagram zilifungwa kwa kuzitumia kuchochea ghasia na uasi.

Pia hakuona aibu kueneza uongo kupitia mitandao ya kijamii, kwa mfano madai ya wizi wa kura kwenye uchaguzi wa mwaka jana alioshindwa na Biden.Aliwachukia sana wanahabari ambao aliwadunisha kama “waenezaji wa habari za uwongo” na kuwataja kama “maadui wa watu”.

Alipuuza misimamo ya kisayansi na kueneza propaganda zake zisizokuwa na msingi, kama vile kuhusu ongezeko la joto duniani, uchafuzi wa mazingira na ugonjwa wa corona.

Trump pia hakuwapa amani wahamiaji nchini Amerika wakiwemo Wakenya. Wakati mmoja alihimiza kupigwa marufuku kwa Waislamu kuingia nchini humo akidai ilikuwa mbinu ya kukabiliana na ugaidi, akaongoza sera za kutenganisha familia za wahamiaji na pia akaanza kujenga ukuta kati ya nchi yake na Mexico kuzuia wageni kuingia.

KUVUNJA SHERIA

Aidha ni kati ya marais wa Amerika walioondoka madarakani wakiwa na uungwaji mkono wa chini zaidi tangu 1939.Katika utawala wake, Trump alipendelea marafiki na familia yake kwa kuwateua katika nyadhifa kuu licha ya kutofuzu kuzishikilia pamoja na kutumia madaraka yake kisiasa, pamoja na kuwasamehe marafiki wake waliofungwa.

Kiongozi huyo alilazimisha uaminifu kutoka kwa maafisa wake kwa kuwataka kufanya kila alichowataka kufanya hata kama ingemaanisha kuvunja sheria, na walipokataa aliwasuta ama kuwatimua.Jaribio la mwisho kulazimisha uaminifu kwake lilikuwa ni majuzi alipomtaka makamu wake Mike Pence kuvuruga kikao cha bunge cha kuidhinisha ushindi wa Biden, ambalo Pence alikataa.

Alimdhalalisha kiongozi wa wengi katika Seneti, Mitch McConnel alipokubali ushindi wa Biden kwenye uchaguzi wa mwaka jana, mbali na kukosana na kiongozi wa wachache katika bunge la waakilishi alipomlaumu kwa kuchochea uvamizi wa bunge.

Chini ya utawala wake aliwafuta maafisa waliokataa kuvunja sheria kwa niaba yake kama vile Jeff Sessions (mwanasheria mkuu) na James Comey (Mkuu wa FBI).

Vituko vya Trump vilichochea hisia kuwa alikuwa na matatizo ya kiakili na mwisho mwisho wa utawala wake kulikuwa na wasiwasi kuwa angechukua hatua hatari kwa Amerika na dunia.

You can share this post!

Kibarua cha kurejesha hadhi ya Amerika duniani chaanza

Changamoto tele zinazomsubiri Biden kukabili