• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
EPL: Liverpool wajifufua ugenini wakipiga tena Tottenham Hotspur

EPL: Liverpool wajifufua ugenini wakipiga tena Tottenham Hotspur

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL walifufua makali yao kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) muhula huu kwa kuwapepeta Tottenham Hotspur 3-1 mnamo Alhamisi usiku.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool waliingia katika mchuano huo baada ya kukosa kushinda mechi tano mfululizo, nne ya hizo zikikamilika bila ya wao kufunga bao.

Spurs walioshuhudia nahodha na fowadi wao Harry Kane akipata jeraha la kifundo cha mguu, walisalia kumtegemea Son Heung-min. Bao la nyota huyo raia wa Korea Kusini lilifutiliwa mbali na refa kwa madai ya kuotea kabla ya Liverpool kupachika wavuni goli lao la kwanza baada ya ukame wa dakika 482 uwanjani.

Roberto Firmino ambaye ni raia wa Brazil alichuma nafuu kutokana na masihara ya beki Eric Dier na kipa Hugo Lloris na kupachika wavuni bao la kwanza la Liverpool baada ya kushirikiana vilivyo na Sadio Mane mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Lloris alitepetea tena dakika chache baada ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa kipindi cha pili kupulizwa aliposhindwa kuondoa kombora la Mane katika eneo la hatari na badala yake, kumpa beki Trent Alexander-Arnold fursa ya kumzidi ujanja kunako dakika ya 47.

Licha ya Pierre-Emile Hojbjerg kuwarejesha Spurs mchezoni kwa kufunga bao kutoka hatua ya 20 katika dakika ya 49, Liverpool walisalia imara na kumiliki asilimia kubwa ya mpira ugenini.

Mohamed Salah alishuhudia refa akikosa kuhesabu bao lake baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kwamba lilifungwa baada ya Firmino kuunawa mpira.

Liverpool kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne jedwalini kwa alama 37, nne nyuma ya viongozi Manchester City ambao wana mechi moja zaidi ya kutandaza ili kufikia idadi ya michuano iliyosakatwa na washindani wao wakuu wakiwemo Liverpool, Manchester United, Leicester City na West Ham United wanaofunga mduara wa tano-bora kwa alama 35.

Spurs walisalia katika nafasi ya sita kwa pointi 33 sawa na Everton ambao wana mechi moja zaidi ya kusakata. Chelsea na Arsenal wanashikilia nafasi za nane na tisa mtawalia kwa alama 30 kila mmoja.

Liverpool walijibwaga ugani wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya msururu wa matokeo duni katika mechi za awali kuwashuhudia wakishuka kwenye msimamo wa jedwali la EPL na pia kubanduliwa na Man-United kwenye raundi ya nne ya Kombe la FA msimu huu.

Liverpool kwa sasa wameshinda jumla ya mechi sita mfululizo dhidi ya Spurs ligini kwa mara ya kwanza katika historia.

Liverpool kwa sasa wanajiandaa kuwaendea West Ham United uwanjani London mnamo Jumapili huku Spurs wakitarajiwa kuvaana na Brighton uwanjani Amex.

You can share this post!

DOMO KAYA: Tuseme kajitakia mwenyewe

Kane kusalia nje kwa muda mrefu baada ya kupata jeraha la...