• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Mwendwa aidhinishwa kuwania nafasi ya haiba katika Baraza Kuu la FIFA

Mwendwa aidhinishwa kuwania nafasi ya haiba katika Baraza Kuu la FIFA

Na CHRIS ADUNGO

RAIS wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa, ameidhinishwa na Shirikisho la Soka Kimataifa kuwania mojawapo ya nafasi za uanachama katika Baraza la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati Tendaji ya FIFA, wagombezi wanne walikuwa wamepata kibali cha kuwania kiti cha Naibu Rais wa shirikisho hilo kutoka Afrika (Confederation of African Football president) huku wawaniaji 13 wengine wakiidhinishwa kuwania nafasi za uanachama katika Baraza la FIFA.

Mukul Mugal ambaye ni mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya FIFA, alisema shirikisho lilikuwa limetema wagombezi wanne waliokuwa wamefichua azma ya kuwania nafasi inayopiganiwa na Mwendwa na wengine.

FIFA hutengea bara la Afrika nafasi saba kwenye Baraza lake – nafasi mbili huwa ni kwa ajili ya mataifa yaliyo na wazungumzaji wa Kiingereza (Anglophone), mbili kwa ajili ya nchi zenye wazungumzaji wa Kifaransa, moja kwa rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf), moja kwa mataifa yenye wazungumzaji wa Kiarabu na nafasi moja kwa minajili ya uanachama wa jumla.

Mwendwa, 41, anaendea mojawapo ya nafasi za kuwakilisha mataifa yaliyo na wazungumzaji wa Kiingereza katika uchaguzi huo utakaofanyika Machi 12 jijini Rabat, Morocco.

“Nimewasilisha stakabadhi zangu tayari na nitakuwa nikielekea Morocco hivi karibuni kupiga kampeni. Wapo wagombezi wengine nitakaoshindana nao kuwania nafasi mbili za kuwakilisha mataifa yenye wazungumzaji wa Kiingereza. Nina matumaini ya kushinda,” akasema Mwendwa.

Miongoni mwa washindani wakuu wa Mwendwa ni Wallace Karia ambaye ni Rais wa Shirikisho la Soka la Tanzania, Walter Nyamilandu ambaye ni Rais wa Shirikisho la Soka la Malawi na Rais wa Shirikisho la Soka la Zambia, Andrew Kamanga.

Wengine ni Amaju Pinnick ambaye ni Rais wa Shirikisho la Soka la Nigeria na Rais wa Shirikisho la Soka la Gambia, Kaba Bajo.

Hii ni mara ya pili kwa Mwendwa kuwania nafasi hiyo baada ya kuanika azma hiyo mnamo 2018 kabla ya kujiondoa mbioni.

Iwapo atashinda, basi Mwendwa atakuwa Mkenya wa kwanza kuwahi kushikilia nafasi hiyo ya haiba kubwa katika FIFA.

Kati ya wawaniaji ambao FIFA imeidhinisha kuwania nafasi ya Naibu Rais wa shirikisho hilo kutoka Afrika ni Patrice Thlopane Motsepe ambaye ni Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika Kusini, Bernard Daniel Anouma ambaye ni Rais wa Shirikisho la Soka la Ivory Coast, mwanakamati mkuu wa zamani wa FIFA, Ahmed Yahya kutoka Mauritania na Augustin Emmanuel Senghor wa Senegal.

You can share this post!

Kiungo wa Santos Soccer aonyesha dalili za kuwa staa wa...

TAHARIRI: Vijana wasitumiwe na viongozi kuzua fujo