• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Koma kulia, pambana kama mwanamume, hakimu amwambia Sonko

Koma kulia, pambana kama mwanamume, hakimu amwambia Sonko

Na RICHARD MUNGUTI

KAMA kuna wakati wenye changamoto tele kwa aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ni sasa.

Maji yalizidi unga hata akabubujikwa na machozi akiwa kizimbani na kumweleza Hakimu Hkuu Douglas Ogoti “nikiwaza na kuwazua yanayonikabili sina budi ila kulia tu.”

Bw Ogoti, anayesikiza kesi ya ufisadi dhidi ya Bw Sonko, alimshauri , “Jipe moyo. Pambana kama mwanamume. Kulia kwa wakati huu hakutasaidia. Nieleze tu unachotaka nami nitakusaidia niwezavyo.”

Bw Sonko alimtazama hakimu na kuangazia macho huku na kule kortini kisha akaanza kulia tena. Aliongea lakini maneno yake yalikuwa yanakataa kumtoka akivuta kamasi.

Alikuwa anatoa barakoa kujipanguza kwa mkono machozi hadi pale hakimu alimwonea huruma baada ya kuguswa na machozi ya gavana huyo wa zamani.

Alimweleza,“Naelewa unachopitia lakini jikaze, mwanamume ni kupambana.”

Alipotulia Bw Sonko alisema, “Masaibu yangu yanatokana na afidaviti niliyowasilisha kortini nikimtaja dada yake Rais Uhuru Kenyatta, Christine Pratt Kenyatta kuhusiana na mtafaruku wa uteuzi wa naibu wa gavana Kaunti ya Nairobi.”

Aliendelea kusema, “…kumtaja kwangu Christine Pratt Kenyatta katika kesi niliyomshtaki Bi Anne Kananu Mwenda niliyekuwa nimemteua kuwa naibu wa gavana kuliniletea haya yote.”

Alisema polisi walimtaka afutilie mbali afidaviti hiyo ndipo wasimfungulie kesi ya kupiga na kujeruhi watu sita mtaani Buruburu.

Bw Sonko azungumza na mmoja wa wandani wake kortini baada ya mahakama kuahirisha vikao akome kulia. Picha/RICHARD MUNGUTI

Akiwasilisha ombi apewe muda kujiandaa kukabiliana na mashahidi katika kesi ya ufisadi ya Sh14m Sonko alisema mawakili aliokuwa nao wamemtoroka.

Alisema hayo huku akianza kulia tena.

“Koma kulia. Tulia kwanza Bw Sonko. Jipe nguvu ndipo ueleze mahakama kile unachotaka ikusaidie,” Bw Ogoti alimbebeleza.

Bw Sonko aliomba apewe fursa ajiandae kukabiliana na kesi ya matumizi mabaya ya mamlaka na upokeaji hongo.

“Naomba hii mahakama inipe muda nijiandae kwa vile mawakili Cecil Miller, George Kithi na wengine wamejiondoa katika kesi hii. Sina wakili wa kujitetea. Naomba siku 14 nijiandae na pia niwatafute mawakili wengine kuniwakilisha,” alisema Bw Sonko.

Akiendelea kulia, wakili Dkt John Khaminwa aliingia kortini na kuomba mahakama amwakilishe Sonko katika kesi za ufisadi zinazomkabili akiwa na mawakili Assa Nyakundi na Wilson Nyamu.

Mawakili hao wapya waliomba wapewe muda kujiandaa kwa kesi hiyo. Bw Ogoti aliwaamuru Mabw Miller na Kithi wawakabidhi faili za ushahidi walizo nazo za kesi hiyo ya ufisadi dhidi ya Sonko.

Hakimu huyo pia aliamuru tume ya kupambana na ufisadi nchini iliyomshtaki Bw Sonko iwakabidhi Dkt Khaminwa na wenzake wawili nakala za ushahidi huo.

Bw Ogoti aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 10, 2021.

You can share this post!

Ghost ataja 28 kuanza maandalizi ya Harambee Stars ya AFCON...

Historia kuandikwa Mwafrika akiongoza WTO