• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Historia kuandikwa Mwafrika akiongoza WTO

Historia kuandikwa Mwafrika akiongoza WTO

Na CHARLES WASONGA na AFP

ABUJA, Nigeria

UONGOZI wa Shirika la Biashara Ulimwengu (WTO) unaelekea kupata sura mpya kwa Mwafrika kuwa kileleni kwa kushikilia wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu.

Aliyekuwa Waziri wa Fedha nchini Nigeria Dkt Ngozi Okonjo-Iweala anaelekea kuteuliwa katika wadhifa huo wa hadhi baada ya raia wa Korea Kusini Yoo Myung-hee kujiondoa kinyang’anyironi.

Myung- hee, ambaye alikuwa anapendelewa na Amerika, Ijumaa aliripitiwa kujiondoa, kulingana na taarifa kutoka Korea Kusini, hatua ambayo inampa nafasi Dkt Okonjo-Iweala, 66, kuliongoza shirika la WTO na kuwa mwanamke wa kwanza na Mwafrika wa kwanza kuwa Mkurugenzi wake Mkuu.

Kupitia taarifa kutoka Wizara ya Biashara, Myung-hee “aliamua kwa hiari yake kujiondoa katika kinyang’anyiro cha kuwa Mkurugenzi Mkuu wa WTO.”

Mchakato wa kumtaja mrithi wa mkurugenzi mkuu wa WTO anayeondoka, Robert Azevedo, umekwamba tangu Oktoba mwaka jana, wakati mabalozi wa shirika hili walimteua Okonjo-Iweala kama anayefaa kuliongoza shirika hilo.

Waziri wa Michezo Kenya Amina Mohammed pia aliwania wadhifa huo lakini akashindwa kuorodheshwa miongoni mwa wawili bora.

Mnamo Oktoba 28, mwenyekiti wa Baraza la WTO David Walker alitangaza kuwa baada ya mashauriano, walikubaliana kuwa “waziri huyo zamani wa fedha nchini Nigeria ndiye anapaswa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Saba wa WTO.”

Lakini utawala wa aliyekuwa Rais wa Amerika Donald Trump uliendelea kupinga uteuzi wake.

Mkurugenzi Mkuu wa WTO huteuliwa kwa njia ya muafaka, na pingamizi zilizoibuliwa na Amerika zilikwamisha shughuli hiyo.

Duru zilisema kuwa kujiondoa kwa Myung-hee kulitokana na mabadiliko katika uongozi wa Amerika baada ya Rais Joe Biden kushika usukani Januari 20, 2021 kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba 3, 2020.

Amerika imekuwa mshirika wa Korea Kusini kwa kutuma wanajeshi 28,500 kuilinga dhidi ya mashambulio kutoka Korea Kaskazini inayojivunia silaha za kinuklia.

You can share this post!

Koma kulia, pambana kama mwanamume, hakimu amwambia Sonko

Rais wa Masumbwi yasiyo ya malipo duniani kuwasili Kenya...